dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, May 18, 2015

Yako wapi matendo mema na maisha bora kwa watanzania kutoka kwa serikali ya CCM?

Image result for flag of ccm
Na Fred Mpendazoe
SIKU moja jamaa mmoja alikuwa amekaa peke yake jangwani akitafakari. Mtawala aitwaye Daruweshi alipopita jamaa huyo hakusimama wala kuinamisha kichwa chake kuonyesha utii. Daruweshi mwenye majivuno alikasirika sana na kusema; “Hawa watu wenye majoho yenye viraka na nguo zilizochakaa hawako tofauti na wanyama,” na hapo msaidizi wa Daruweshi alimkaripia yule mtu akisema; “Kiongozi mkuu wa nchi anapopita kwa nini huinamishi kichwa chako kuonyesha utii kwake? Kwa nini umekuwa jeuri kiasi hiki?”
Yule jamaa alijibu; “Mwambie mfalme wako Daruweshi atarajie kupata heshima kutoka kwa watu wenye matumaini ya kupata hisani kutoka kwake. Mwambie pia kwamba viongozi wapo ili kuwalinda watu wao.
“Watu hawakuumbwa ili kazi yao iwe kuwatii watawala wao. Mtawala ni mlinzi wa watu maskini, ingawa yeye ndiye mwenye nguvu na utukufu mkubwa. Kondoo hawakuumbwa kumtii mchungaji, bali mchungaji ndiye aliyeumbwa kuwahudumia kondoo”.
Yule mtu aliendelea kusema; “Tazama ulimwengu uliokuzunguka leo utamuona mtu mmoja mzembe, lakini amefanikiwa, wengine wakihangaikia maisha bila mafanikio. Ngoja umauti utakapofika, si maskini wala tajiri hakuna wa kuzuia, au fukua makaburi ukachunguze ile mifupa iliyofunikwa kwa udongo: Je, unaweza kuitofautisha ipi ni mifupa ya tajiri na ipi ni ya maskini?”.
Mfalme Daruweshi alishikwa butwaa baada ya kusikia maneno yale, akamuuliza yule jamaa; “nikupe zawadi gani kwa ushauri wako mzuri?” Yule jamaa akajibu; “Jambo pekee ninaloweza kukuomba ni kwamba usinisumbue tena”.
Baada ya kusikia maneno ya jamaa mwenye joho, mfalme Daruweshi akaomba msaada akisema; “nipe ushauri wowote.” Yule mtu akajibu; “ingawa sasa una mali na mamlaka, kumbuka kabla hujachelewa, mali na mamlaka hutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine”.
Mfano wa simulizi hiyo unatueleza kwamba; lengo la kwanza na lengo pekee la serikali yoyote makini duniani na inayoendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia, ni ulinzi wa maisha ya wananchi wake na furaha yao na si uharibifu wake. Kulinda maisha ya wananchi wake ni lengo pekee kwa serikali ya kidemokrasia kwa sababu ipo kwa ajili ya wananchi na inapata madaraka kutoka kwa wananchi.
Watanzania walipiga kura na kuichagua serikali iliyopo madarakani. Serikali inao wajibu wa kusikiliza maoni, ushauri na malalamiko mbalimbali ya Watanzania. Penye uhuru ni pale wananchi wanapoweza kutoa maoni yao, ushauri wao, na malalamiko yao bila hofu, lakini penye demokrasia ni pale serikali inaposikiliza maoni, ushauri na malalamiko ya wananchi na si vitisho.
Kitendo kinachofanywa na Serikali kwa wananchi wake, mfano kutosikiliza kilio cha madereva nchini ni dalili za kufifia kwa demokrasia nchini kwani jukumu la kwanza la kiongozi ni kuwapa watu wake matumaini na si kuwatisha.
Vurugu zinazotokea katika nchi zote duniani – migomo, maandamano na mashambulizi ya kiraia, hazisababishwi na wananchi, bali husababishwa na kukosekana kwa utawala bora na hasa viongozi waliopewa madaraka na mamlaka kutokuwa na maadili.
Viongozi wanaodhani kwamba nafasi walizonazo, vyeo walivyonavyo na madaraka waliyonayo ni nyenzo za kujinufaisha badala ya nafasi za kuwatumikia wananchi waliowaweka madarakani bila upendeleo, ni viongozi walio katika hatari kubwa. Tanzania si nchi ya kipekee hapa duniani, yaliyojitokeza Kenya, Zimbabwe, Guinea, Tunisia, Misri na kwingine Afrika; yanaweza kutokea pia Tanzania.
Aidha, ridhaa ya serikali yoyote kuendelea kukaa madarakani haitokani tu na katiba na sheria iliyoiweka madarakani, bali ridhaa ya wananchi kutawaliwa inatokana zaidi na matendo mema ya serikali hiyo kwa wananchi wake. Mfano wa mfalme Daruweshi unatufundisha kwamba viongozi wa serikali wanapaswa kuwalinda watu.
Kama ambavyo kondoo hawakuumbwa kumtii mchungaji bali mchungaji ndiye aliyeumbwa kuwahudumia kondoo, vivyo hivyo serikali yetu nayo ina wajibu wa kusikiliza na kuhakikisha Watanzania wakiwemo madereva, wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyakazi, wastaafu wananufaika na utajiri wa nchi. Pengo kati ya masikini na matajiri lipungue, si suala la hesabu, ni suala la kuondoa matabaka.
Serikali ina changamoto ya kuhakikisha ufisadi nchini unaondolewa ili utajiri wa nchi yetu uwanufaishe wananchi wakiwemo madereva, wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyakazi. Mapato ya nchi yanayopotea kutokana na ufisadi kwa mwaka nina hakika yangewezesha serikali kuwalipa wafanyakazi na wastaafu mishahara mizuri na mafao mazuri. Pia kuwakopesha wanafunzi wa vyuo vikuu na kuboresha mazingira ya shule za msingi na sekondari.
Kwanini serikali haijaonyesha ghadhabu kali kwenye suala la Escrow? Ziko wapi ghadhabu za serikali kwa waliohusika na rushwa katika ununuzi wa rada? Ziko wapi ghadhabu za serikali kwenye viongozi wa taasisi zilizoshindwa kuchunguza kampuni ya Kagoda iliyoiba mabilioni ya Benki Kuu?
Ziko wapi ghadhabu za serikali kwa ubadhirifu unaofanyika ndani ya Wakala wa Barabara (Tanroads)? Ziko wapi ghadhabu za serikali kwa upotevu wa mabilioni ya fedha kwenye halmashauri zetu nchini? Ziko wapi ghadhabu za serikali kwa waliohusika na mikataba mibovu kwenye sekta ya madini? Ziko wapi ghadhabu za serikali kwa wale waliohusika na mkataba wa uendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania?
Serikali inayoghadhibika kwa wananchi wake mfano madereva wanapoomba kuongezewa maslahi yao, lakini serikali hiyo ipo tayari kujadiliana na mafisadi na kuendelea kushirikiana nao kama ilivyofanya kwa baadhi ya waliohusika na wizi wa fedha za EPA. Serikali ya aina hiyo haiwezi kuheshimiwa na wananchi wake sawa na mfalme Daruweshi.
Niwakumbushe Watanzania wenzangu kwamba uhalali wa serikali yoyote ya kidemokrasia kuendelea kukaa madarakani haitokani tu na katiba na sheria iliyoiweka madarakani, bali zaidi hutokana na ridhaa ya wananchi kuendelea kutawaliwa au kuongozwa nayo.
Aidha, ridhaa hiyo hutokana na matendo mema ya Serikali hiyo kwa raia wake. Hili ni muhimu sana kwa kila Mtanzania aliye makini, tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu mwezi oktoba. Watanzania tujiulize:
Yako wapi matendo mema ya Serikali ya CCM kwa madereva nchini wanaodai mishahara na maslahi yao mengine, wakati serikali ya CCM inawapuuza wanapodai haki zao za msingi?
Yako wapi matendo mema ya serikali ya CCM kwa vijana vyuoni wanaodai mahitaji ya msingi ya kielimu, wakati tunashuhudia vijana wakinyanyasika kwa mikopo yenye kubagua mpaka wagome ndio mikopo itoke?
Yako wapi matendo mema ya Serikali ya CCM kwa walimu, wakati tunashuhudia walimu mpaka wagome ndipo wasikilizwe?
Yako wapi matendo mema ya serikali ya CCM kwa wastaafu waliolitumikia taifa hili kwa uadilifu, wakati tunashuhudia mateso makubwa kwa wastaafu wazee wetu wakidhalilika mitaani?
Yako wapi matendo mema kwa wafugaji, wakati tunashuhudia wafugaji wakinyanyasika kana kwamba wao si raia wa nchi hii?
Yako wapi matendo mema kwa wauguzi, polisi na wananchi wanaoishi karibu na migodi yenye utajiri mwingi, wakati tunashuhudia wakiishi maisha duni?
Yako wapi matendo mema kwa watoto wa kike wanaoteseka kwa kupata mimba wakati tunashuhudia viongozi wakiwakebehi kwamba wanaponzwa na viherehere vyao, badala ya kuwapa mazingira bora ya elimu?
CCM iliwaahidi Watanzania maisha bora kwa kasi mpya na nguvu mpya iliyoambatana na ari mpya.
Yako wapi maisha bora kwa Watanzania leo, wakati bei ya mchele kwa saa ni shilingi 1900 kutoka shilingi 800, bei ya nyama kwa sasa ni shilingi 6000 kutoka shilingi 2500 kwa kilo, sembe kutoka shilingi 250 hadi shilingi 2500 kwa kilo na bati kutoka shilingi 7500 hadi shilingi 16,000.
Yako wapi maisha bora kwa watoto wa shule wanaosoma wamekalia mawe badala ya madawati? Yako wapi maisha bora kwa wanafunzi wa vyuo wanaoishi kwa mlo mmoja kwa siku?
Yako wapi maisha bora kwa akina mama wajawazito wanaolala wanne kwenye kitanda kimoja ? Yako wapi maisha bora kwa wastaafu wanaolipwa mafao kidogo yasiyokidhi mahitaji ya msingi?
Katika miaka mitano iliyopita ya Serikali ya CCM, ni bayana kwamba kwa kiasi kikubwa kumekuwepo upungufu mkubwa wa matendo mema kwa raia wake na hakuna maisha bora walioahidiwa Watanzania. Hivyo, CCM haina ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi. Nawaomba Watanzania wa rika zote mwaka huu katika uchaguzi huu wachague mabadiliko.
Niwakumbushe tena kwamba serikali yoyote inayotokana na rushwa ni serikali inayotumwa na matajiri walionunua kura na huabudu matajiri hao. Serikali ya aina hiyo haisikilizi kilio cha watu wake.
Hukumbatia mafisadi na kujifanya viziwi kuhusu kilio cha wananchi wake. Tumeshuhudia miaka kumi ya Serikali ya CCM, jinsi ambavyo imeshindwa kufanya maamuzi kwa maslahi ya taifa na kubaki ikitumikia matajiri wachache.
Ninapohitimisha makala hii napenda kusisitiza: Pasipo mashauri, taifa huanguka, bali kwa wingi wa washauri huja wokovu; Mema hushinda mabaya; Ukweli hushinda uongo na Upendo hushinda uovu; Harakati zetu zitafanikiwa. TUTASHINDA.
Aidha, sehemu za utenzi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwenye kitabu chake Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania, utahitimisha makala hii. “Ole wake Tanzania Tusipoisaidia! Niwezalo nimefanya; Kushauri na kuonya. Nimeonya; Tahadhari! Nimetoa ushauri: Nimeshatoka kitini: Zaidi nifanye nini? Namlilia Jalia Atumlikie njia; Tanzania ailinde.

Mwandishi wa makala hii alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga kupitia CCM kuanzia Novemba 2005 hadi Machi 2010 alipojiuzulu kutokana na kutoridhshwa na mwenendo wa chama hicho. Anapatikana kwa namba 0762 92 6556. 



No comments :

Post a Comment