dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, August 4, 2015

Mbowe afunguka aliko Dokta Slaa.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akizungumza katika kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana. PICHA: SELEMANI MPOCHI
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amevunja ukimya juu ya kinachomsibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, ambaye amekuwa haonekani kwenye shughuli za chama hicho.
Akifungua mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Mbowe alisema kuwa Dk. Slaa ameamua kupumzika shughuli za chama baada ya kutofautiana na wenzake juu ya ujio wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye atapeperusha bendera ya Chadema kupitia Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwania urais katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Mbowe alisema kuwa Dk. Slaa alitofautiana na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho juu ya kuteuliwa kwa Lowassa ambaye alijiunga na chama hicho, na kwa pamoja wameamua kumwacha apumzike na kama ataona inafaa atawaunga mkono mbele ya safari.
Alisema kwa muda mrefu sasa kumekuwa na minong’ono, manung’uniko, malalamiko na nderemo kuhusiana na kujiunga kwa Lowassa katika chama hicho.
“Dk. Slaa tunampenda sana na yeye anatupenda na kwa hulka yake, Katibu Mkuu wetu hawezi kupingana na maamuzi ya chama ya kumkaribisha Lowassa, tunamuombea kwa Mungu ampe ujasiri kwa kuona kuwa ujio wa Lowassa ni mipango ya Mungu,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema kabla ya Lowassa na wenzake kujiunga na chama hicho, vilifanyika vikao vya mashauriano ya muda mrefu na kujiridhisha kuwa hakuna shaka kuhusiana na mwanasiasa huyo kujiunga na Chadema.
Aliongeza kuwa katika hatua zote hizo, Dk. Slaa alishiriki. 
Hata hivyo, Mbowe alisema katika hatua za mwisho, Dk. Slaa alitofautiana na baadhi ya watu, lakini chama kinaendeela kuzungumza naye ili kufikia muafaka.
“Hata jana (juzi) niliongea naye na kimsingi, Dk. Slaa amekubaliana kwamba sisi tuendelee na mchakato huu, tukifikia sehemu atatu-join (ataungana nasi) mbele ya safari, ifahamike kuwa katika suala la maamuzi siyo lazima kila mmoja akubali kwa asilimia 100,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema mtu anaweza kujiunga na chama chochote cha siasa, lakini Chadema hakiwezi kufanya udalali kwa sababu chama kimefika hapo kilipo kutokana na kuungwa mkono na Watanzania wengi.
“Ni dhahiri kuwa CCM ndio adui yetu mkuu, na ukipata nafasi ya kumjeruhi adui yako usipoitumia lazima utakuwa mwendawazimu,” alisema na kuongeza:
“Ilijengeka imani kuwa hatuwezi kuwa na chama cha upinzani cha kuwa na uwezo wa kupambana na chama tawala.”
Mbowe aliwaeleza wajumbe kuwa yamejitokeza makundi ya watu wengi toka ndani ya CCM ambao wanataka kujiunga na Chadema na katika makundi hayo aliyekuwa anabinywa zaidi ni Lowassa.
Alisema katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu, lakini ndani ya Chadema kinachoangaliwa ni maslahi ya Taifa ya kudumu.
Mbowe alisema kumezuka hofu ndani ya Baraza Kuu, wagombea ubunge na wagombea udiwani na hofu hiyo inapokelewa kwa hisia tofauti na kwamba chama kitahakikisha hofu hiyo inapatiwa ufumbuzi ili kupata nguvu ya kuishinda CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. 
“Hofu ambazo zinatokana na minyukano ya kisiasa lazima tuishinde, na mimi kama kiongozi mkuu wa chama nitahakikisha hofu hii tunaishinda,” alisema.
Mbowe hata hivyo, alisema Dk. Slaa aliomba kwenda likizo kwa mapunziko na baadaye ataungana nao.
Dk. Slaa alipotafutwa katika simu yake ya kiganjani jana kuzungumzia hatma yake hakupatikana.
Kwa takribani wiki mbili sasa kumekuwa na hofu ambayo imetanda ndani ya Chadema na wananchi kwa ujumla kutokana na kutoonekana kwa Dk. Slaa, katika matukio ya kisiasa yanayohusu mustakabali wa chama hicho. 
Dk. Slaa hakuonekana siku ya kihistoria Jumanne wiki iliyopita iliyokuwa maalum kwa Lowassa kutangaza kujivua uanachama wa CCM  na kujiunga Chadema.
Kadhalika, Dk. Slaa hakuonekana makao makuu ya chama siku wakati Lowassa alipofika kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho akitarajiwa kuwakilisha Ukawa.
Mbali na kutokuonekana Chadema, Dk. Slaa pia hakuonekana kwenye mkutano wa Ukawa, uliofanyika makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), ambao wenyeviti wenza wa umoja huo walimkaribisha Lowassa kujiunga nao.
Baada ya hapo kumekuwapo na taarifa mbalimbali ambazo Dk. Slaa hakuwahi kuzithibitisha kwamba ameachana na siasa.
Lowassa aliamua kujiunga Chadema baada ya kuchoshwa na siasa zilizojaa chuki za kumzuia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya kuwania urais kupitia CCM.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment