dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, September 2, 2015

Gesi na mafuta yatasaidia uchaguzi huru?

Image result for gas and exploration

Image result for gas and exploration

Na Ahmed Rajab
MADOLA ya Magharibi yanauangaza kwa makini mchakato mzima wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 pamoja na namna kura zitavyopigwa na kuhesabiwa siku hiyo. Inatazamiwa kwamba Muungano wa Ulaya pekee utaleta waangalizi wasiopungua 128 kuangalia namna kura zitavyopigwa.

Jumuiya na taasisi nyingine za kimataifa nazo pia zitaleta waangalizi wao.

Tukisema “mchakato wa uchaguzi” hatuna maana ya kampeni za uchaguzi na upigaji kura tu. Mchakato wa uchaguzi una maana pana zaidi. Unajumlisha mambo yanayofanyika, au yanayopaswa kufanyika, kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Miongoni mwa mambo yanayofanywa kabla ya uchaguzi ni uteuzi wa Tume ya Uchaguzi inayotakiwa iwe huru, usajili wa wapiga kura na kukamilishwa kwa Daftari la Wapiga kura kwa njia za haki sio, kwa mfano, kupachikwa majina ya watu waliokwishafariki katika Daftari hilo au kuwazuia wenye haki ya kusajiliwa wasisajiliwe.

Mambo mengine ya kabla ya uchaguzi ni pamoja na kuchapishwa kwa karatasi za kura, kutangazwa kwa ilani za vyama vya siasa, kuwaelimisha polisi na wanajeshi kuhusu dhima yao katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Muhimu ni kwamba polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama visiwe vinatumiwa na upande wowote. Serikali, kwa jumla, na polisi na wanajeshi wake hawatakiwi kuwatisha wapigaji kura kwa njia yoyote ile.

Kumekuwako na mtindo Zanzibar tangu uanze mfumo wa vyama vingi vya siasa wa kumiminwa vikosi vyenye silaha nzito nzito kila Uchaguzi Mkuu. Utadhani kuna vita na wananchi wanapigana wenyewe kwa wenyewe. Au utadhani kama nchi imezungukwa na maadui kutoka nje waliokaa chonjo kuipindua serikali ya CCM.

Hali hiyo, ya kumiminwa majeshi yenye silaha nzito wakati wa uchaguzi, huwa inawatia hofu wapigaji kura na inahatarisha amani. Ikiwa kwa kufanya hivyo, viongozi wa serikali ya Muungano na wa Zanzibar wanafikiri kuwa ndio wanahakikisha “Mapinduzi Daima” basi inafaa wafikirie tena.

Na ikiwa wanafikiri kwamba wanaweza maisha kuzuia mabadiliko yasitokee basi kwanza, wanajidanganya na pili, ya nini kufanya uchaguzi?

Ukweli wa mambo ni kwamba wananchi wanataka mabadiliko; wamechoka kudanganywa. Wakati wa utawala wa mabavu umekwisha. Watu hawakubali tena kuonewa na wala hawatokubali amani iliyopo ichafuliwe na yeyote, hata na vyombo vya dola.

Vyombo vya habari vya umma kama vile vya Shirika la Utangazaji la Tanzania Broadcasting Corporation (TBC) na lile la Zanzibar Broadcasting Corporation (ZBC) vinatakiwa visiwe na upendeleo wowote, kinyume na ilivyo sasa ambapo ni wazi kwamba mashirika ya TBC na ZBC yanaelemea upande mmoja kwa kukipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachotawala.

Hata kabla ya waangalizi wa uchaguzi kutoka nje kufika Tanzania, tayari jumuiya kadhaa za kimataifa pamoja na serikali zao zimekuwa zikiufuatilia huu mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu. Katika siku za hivi karibuni, mabalozi wa nchi kadhaa za Magharibi wamekuwa na mazungumzo na wakuu wa vyama vya siasa pamoja na viongozi wa serikali zote mbili, ya Muungano na ya Zanzibar.

Wote wamekuwa wakiwahimiza wanasiasa na wakuu wa serikali wahakikishe kwamba uchaguzi ujao utakuwa huru na utafanywa katika mazingira ya amani na utulivu. Wameonesha kuvunjwa moyo na matamshi ya baadhi ya wanasiasa kama yale ya yule aliyesema kwamba chama chake lazima kishinde hata kama ni kwa kutia “goli la mkono”.

Baadhi ya wanasiasa wa Zanzibar kutoka CCM nao pia wamekuwa wakitoa matamshi ya kutisha kama, kwa mfano, kwa kusema ya kuwa hawatoitoa serikali kwa kura ila labda wapinduliwe. Yote hayo ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakitajwa mara kwa mara na wawakilishi wa serikali au taasisi za kigeni wanaofuatilizia mchakato wa uchaguzi unavyoendelea Tanzania.

Wanayataja pia matukio kadhaa ya polisi na vyombo vingine vya dola kutumia nguvu Bara na Visiwani. Kuna mifano kadhaa ikiwa pamoja na kushambuliwa waliokwenda kwenye vituo vya kuwasajili wapigaji kura katika sehemu mbalimbali za Unguja.

Na kuna ile kadhia ya waangalizi wawili wa Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Kuangalia Chaguzi Tanzania (TACCEO) walivyoingiliwa na askari sita wa polisi waliokuwa wamejizatiti vilivyo kwa silaha katika chumba cha hoteli waliofikia huko Makambako.

Tukio hilo lilitokea saa tano kasorobo za usiku Machi 7, mwaka huu, na lilihatarisha maisha ya waliohujumiwa. Polisi waliwapiga vibaya sana wakijidai kwamba wakiwadhania kuwa majambazi. Vitendo kama hivi havikubaliki kabisa katika utaratibu wa kidemokrasia.

Kiasi Mtandao wa TACCEO uwe unakitia homa chama kinachotawala na serikali yake. Mtandao huo umekuwa macho ukitekeleza wajibu wake wa kuangalia kama mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaendeshwa kwa njia za haki. Mwishoni mwa wiki iliyopita tu ulikemea kauli iliyotolewa siku chache zilizopita na Rais mstaafu Benjamin Mkapa kuwahusu wapinzani.

Mkapa aliwaita watu wanaosema kuwa wanapigania ukombozi wa Tanzania kuwa ni “wapumbavu na malofa”. Mtandao wa TACCEO uliielezea kauli hiyo kuwa isiyo na staha. Mkapa alijikwaa ulimi vibaya sana kwa kutumia lugha kama hiyo ya kiburi na ufidhuli.

Kwa hakika, lugha za matusi na kejeli hazifai kutumika wakati wa kampeni za uchaguzi. Muda wa kampeni ukimalizika na ifikapo siku ya kupiga kura waangalizi wa uchaguzi huwa na kibarua kikubwa cha kuthibitisha kwamba haki inatendeka kwenye vituo vya kupiga kura, kwamba polisi na majeshi hayatumiwi kuwatia hofu wapigaji kura na kwamba kura zinahesabiwa katika mazingira ya haki na haziibiwi. Kwa ufupi, kwamba hakuna upendeleo au ubaguzi wa aina yoyote ile.

Uchaguzi huu ujao utakuwa na changamoto nyingi. Iliyo kubwa ni ile ya kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanywa kwa amani. Watanzania wote, Bara na Visiwani, wanataka amani na utulivu. Hawataki patokee vurugu, umwagaji wa damu wala kamatakamata. Wanataka pawepo amani sasa, siku ya kupigakura na baada ya kura kupigwa.

Inasikitisha kuona kwamba yale maovu yaliyokuwa yakitokea Zanzibar siku za uchaguzi hivi sasa yanajitokeza Bara vilevile. Na kwa Zanzibar inasikitisha kwamba utaratibu wa utawala tangu uchaguzi uliopita wa 2010 haukuwa wa ushirikiano wa dhati baina ya Rais Ali Mohamed Shein na Makamu wake wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamadi.

Ushirikiano huo umekosekana hasa kuhusu suala nyeti la Muungano ambalo ufumbuzi wake ni muhimu kwa Wazanzibari wote na kwa mustakbali wa Visiwa vyao. Pengine Shein mwenyewe atakataa lakini ukiiangalia kwa undani Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) anayoiongoza ni sawa na serikali ya CCM. Sababu moja ni kwamba Rais mwenyewe amekuwa akiendesha shughuli zake kama mkereketwa wa CCM.

Kuhusu suala la Katiba, kuna baadhi ya viongozi wa CCM/Zanzibar ambao hawakusimamia maslahi ya Zanzibar. Hawa wanaonekana kwao kuwa kama mahaini; barazani wanaitwa “ahli maslahi”, yaani watu wenye kuyapendelea maslahi yao na, kama wasemavyo wenyewe, ya chama chao.

Kwa hakika, moja ya matatizo ya Zanzibar ni kwamba watawala wake wanayafikiria zaidi maslahi yao binafsi. Hawazijali shida zinazowakabili wanyonge katika mfumo wa uchumi wa kibepari ambao chini yake asiye nacho huwa analala na njaa.
Hali hii ni kinyume na dhamira za Mapinduzi ya 1964, ambayo moja ya malengo yake lilikuwa ni kuondosha njaa, kuleta usawa na kunyanyua maisha ya wanyonge.

Baadhi ya viongozi hawa wa CCM/Zanzibar wanatubabaisha kwasababu matamshi wanayoyatoa katika shughuli zao za kichama na hotuba zao za hadharani hazifanani kabisa na wanayoyazungumza faraghani, hasa kuhusu Muungano.

Kwa mujibu wa Salim Rashid, katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi na aliyefanya kazi kwa karibu sana na Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ni kwamba Karume akiufikiria Muungano kuwa ni jambo la muda.
Anahoji kwamba hii ndio maana sheria zote zilizotungwa zikaifanya Zanzibar iwe mshirika mdogo katika Muungano hazikutungwa wakati wa uhai wake Karume.

Uchaguzi huu unaotukabili unawapa Watanzania fursa ya kuleta mabadiliko katika mfumo wa utawala. Hali ni nzuri kwa wananchi lakini inaonesha kuwa ni mbaya kwa watawala. Ndio maana wamemahanika.
Ninaamini kwamba kitachoinusuru Tanzania na kuhakikisha kwamba uchaguzi utafanyika kwa njia za uwazi na uhuru kuliko zamani ni rasilmali yake ya maliasili. Hayo madola ya nje yanayoiangaza Tanzania kwa macho mawili yanafanya hivyo kwa maslahi yao.

Yanatambua kwamba katika muda wa miaka michache tu ijayo Tanzania itakuwa na uchumi utaokua kwa kasi kubwa na utaovuma katika ukanda wa Afrika ya Mashariki. Uchumi huo utapata msukumo mkubwa kwa mafuta na gesi asilia inayoendelea kugunduliwa nchini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati na Madini hadi Mei mwaka huu, kiwango cha akiba ya rasilmali ya gesi asilia kilikuwa futi za ujazo trilioni 55.08. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea kufanya utafiti kubaini kiwango cha akiba ya rasilmali hiyo kilichopo nchini. Uwekezaji katika mradi mmoja tu wa gesi asilia unafika dola za Marekani bilioni 30.

Yote hayo yanaashiria mustakbali mwema kwa uchumi wa Tanzania iwapo serikali itasimamia vyema miradi iliyopo. Kuna uwezekano mkubwa kwamba katika muda wa miaka isiyozidi mitano hata sarafu ya shilingi ya Tanzania inaweza ikapata nguvu na kuwa na thamani ya kuheshimika, kinyume na ilivyo sasa.

Madola ya Magharibi ambayo wawekezaji wake wameingiza rasilmali zao nyingi katika sekta ya mafuta na gesi asilia hayataki pazuke vurugu nchini zitazohatarisha mali na biashara zao. Ndio maana wawakilishi wao wamo mbioni kuzisihi serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar zisiichezee amani ya nchi kwa kuuvuruga Uchaguzi Mkuu.

Pakizuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu za uchaguzi basi miradi ya mabilioni ya dola za Marekani itaingia hatarini. Na hilo ndilo wanalotaka kuliepuka.

Safari hii, kushinda mara zilizopita, serikali za madola hayo pamoja na taasisi zao na hata wawekezaji wao, wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba Uchaguzi Mkuu ujao utakuwa wa haki na wa amani.

Mara nyingi, kwingi Afrika, vyombo vya ulinzi ndivyo vinavyolaumiwa kwa kuvuruga amani wakati wa uchaguzi. Hufanya hivyo, ingawa ni serikali na vyombo vyao vya ulinzi kama vile polisi, jeshi na mahakama vyenye jukumu kubwa kuhakikisha kwamba mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa amani. Na kuna wadau wengine wa daraja ya pili wenye dhima hiyo pia. Nao ni pamoja na asasi za kiraia, nchi wafadhili na jumuiya ya kimataifa.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/gesi-na-mafuta-yatasaidia-uchaguzi-huru#sthash.kAEghMnn.dpuf

No comments :

Post a Comment