dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, October 25, 2015

JK: Hakuna kama Magufuli


Rais Jakaya Kikwete amesema uteuzi wa Dk. John Magufuli kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulifanywa kwa umakini na kuzingatia vigezo ikiwamo uadilifu wake.


Alisema Kamati ya Maadili ya CCM ilijiridhisha kuwa Magufuli anafaa agombee urais ili aiongoze serikali ya awamu ya tano.

“Tulijiridhisha kwa sifa uadilifu, utendaji wake wa kazi, maana kila wizara aliyopitia alifanya kazi kwa uhodari mkubwa, umakini, uhodari, ubunifu na mfuatiliaji wa mambo, hatukutaka mgombea mwenye manukato ya rushwa,” alisema.

Rais Kikwete amesema hayo jana wakati akimnadi mgombea urais kupitia CCM, Dk. Magufuli wakati akihitimisha kampeni zake jijini Mwanza.

Naye Magufuli, akiomba kura kwa wananchi  alisema ametumia usafiri wa barabara kuomba kura ili kujionea changamoto  inazowakabili wananchi hasa matatizo ya huduma za maji na umeme.

 “Nimepata ushauri mwingi kutoka katika makundi mbalimbali, hivyo nitaufanyia kazi pindi itakapochaguliwa na wananchi kuongoza nchi hii,” alisema.

Alisema katika kampeni zake, amebaini Watanzania asilimia 75 ni wakulima hivyo ataboresha sekta hiyo, kujenga viwanda, kuimarisha sekta ya uvuvi, kupunguza ushuru kwa wavuvi wadogo na kuwapatia zana za kisasa.

Naye mgombea mwenza wa urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, alisema suala la mabadiliko haliji kwa kuzungusha mikono bali ni kwa vitendo.

“Uchaguzi unaweza ukadhoofisha au kuboresha maendeleo ikiwa mtachagua viongozi wanaofaa au wasiofaa, hivyo nawaomba vijana msitumike vibaya kwa mambo ya kishabiki,” alisema Samia.

JK AIKANA RICHMOND

Takribani miaka nane tangu kuibuliwa kashfa ya mkataba wa kifisadi kati ya Shirika la Umeme  (Tanesco) na Kampuni ya Richmond Development (LLC); Rais Kikwete amejitokeza hadharani akiikana na kusema hana ‘shirika’ nayo.

Kashfa hiyo ilitokana na hatua ya  Richmond LLC ya Houston, Marekani kushinda zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura mwaka  2006.

Ndio iliyosababisha Bunge la Tisa kuunda Kamati Teule iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk Harisson Mwakyembe na kusababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, mwaka 2008 huku ikidaiwa kuliingiza taifa hasara ya Sh. milioni 152 kila siku.

Tangu kujiuzulu kwake Lowassa alikuwa akisisitiza kwamba uamuzi wake ulifikiwa ili kuilinda serikali ya CCM, lakini baada ya kuingia upinzani, alimkariri afisa mmoja wa Ikulu akisema ‘bosi wake’ alimzuia asiuvunje mkataba wa Richmond.

Pia suala hilo likaibuka katika kampeni za urais za Lowassa pale Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alipomhusisha Rais Kikwete na umiliki wa Richmond.

Hata hivyo, pasipo kumtaja mmiliki wake, Rais Kikwete ‘alijibu mapigo’ na kusema anayeimiliki Richmond ni yule anayenadiwa na Lissu kuwa Rais wa nchi. Kauli hiyo ilitafsiriwa kumlenga Lowassa.

Lakini katika mkutano wa jana, Rais Kikwete akionekana kukerwa alithibitisha kushiriki mjadala kuhusu haja ya kuwapo uzalishaji wa dharura wa umeme, lakini si katika uteuzi wa kampuni ya kufua nishati hiyo.

Rais Kikwete alisema kanuni na taratibu za manunuzi zilikiukwa katika mchakato wa kuipa zabuni Richmond na kwamba hata malipo yalipocheleweshwa mara kadhaa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha alimfuata kuomba msaada ili zilipwe.

“Tatizo kwenye Richmond ni kanuni hazikuzingatiwa, ilipatikana kampuni isiyokuwa na uwezo ndio tatizo lilipoanzia hapo,” alisema na kuongeza:

“Tulikubaliana tutafute namna ya kupata nishati mbadala baada ya bwawa la Mtera kukauka, ila taratibu za manunuzi za kuipata kampuni ya kufua umeme ya Richmond zilikiukwa licha ya kutoa angalizo kuwa manunuzi yaheshimiwe, lakini kanuni zilivunjwa,” alisisitiza.

Aidha, Rais Kikwete alisema wapinzani wanaodai kampuni hiyo ni mali yake, wanatakiwa waache kusema hivyo kwani ni kuwapotosha wananchi.

“Nimeshiriki kuamua kuwapo uzalishaji umeme wa dharura, lakini sikushiriki kuamua kampuni gani,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment