dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, October 21, 2015

Kama iko hata chembe ya mabadiliko, chembe hiyo itakuwa Ukawa!


Na Jenerali Ulimwengu.
KICHWA cha makala ya wiki hii nimekiteua kwa makusudi kabisa kwa sababu kadhaa. Kwa umri wangu na kutokana na uzoefu wangu katika siasa za nchi hii, ninajua kwamba siasa zetu karibu siku zote ni siasa za ubabaishaji na ulaghai.

Mara zote tumesikia watu wakijiapiza kutenda hili au lile iwapo watachaguliwa, lakini tukija kuwapima baada ya muda tunagundua kwamba yote waliyokuwa wakiahidi si tu kwamba wameshindwa kuyatimiza, bali ukweli ni kwamba hata wakati wakiyaahidi hawakuwa na nia ya kuyatenda bali waliyatumia kama chambo cha kuvulia kura za kuwawezesha kuingia madarakani, basi.

Baada ya kuingia madarakani mambo yanakuwa ni yale yale. Tunaishi ndani ya utamaduni wa kihafidhina kiasi kwamba ni vigumu kutaraji kwamba yeyote katika hao tunaowasikia wakiahidi mabadiliko wanao uwezo wa hata kufikiria mabadilko yoyote tunayoweza kuyaamini. Jamii yetu imekuwa ni jamii ya kutenda mambo kwa mazoea na kuchelea kufanya mabadiliko, hata pale mabadiliko yanaonekana bayana kwamba hayaepukiki.

Anayetaka kulisaili hili ninalosema na aangalie vielelezo vichache tu: Baada ya miaka izidiyo 40 bado hatujakamilisha kuhamia “Makao Makuu Dodoma”, na gharama za riwaya hiyo tunaendelea kuzilipa. Mradi wa “mabasi yaendayo kasi” unatembea kwa mwendo wa kinyonga (kwa miaka takriban 20) katika jitihada za kujenga kilometa 30 za barabara wakati wenzetu Ethiopia wanatengeneza reli ya zaidi ya urefu huo katika miaka mitatu.
Kauli-mbiu ya “Kilimo Kwanza’ imegeuzwa kuwa utani, na hivi sasa inatumika kuyasema magari yanayoitwa “mashangingi” ambayo yanapendwa sana na watawala wetu. Ule msemo wa “Big Results Now” ni kichekesho kingine tulichokwenda kukiazima kwa ndugu zetu wa Malaysia bila hata kuelewa wao walikuwa na maana gani. Sasa tunajua kwamba hatukua na mnasaba nao.

Hii ni mifano michache tu, lakini msomaji anaweza kuchunguza na kutafakari miradi na ahadi mbalimbali katika maeneo anayoyajua vyema.

Chunguza maeneo yote ya juhudi za kuleta maendeleo, iwe ni katika kilimo, uvuvi, elimu, viwanda, mazingira, utawala bora, utalii, michezo, na kadhalika. Kila mahali kinachoonekana ni kasi ndogo mno ya kufanya mabadiliko, na mahali pengine ni ishara za kurudi nyuma na kufuta hata kile tulichokuwa tumefanikiwa kukijenga.

Baada ya miaka 50 ushey, kiwango cha maendeleo tulicho nacho hakifanani na muda wote huo. Kwa kasi tunayokwenda nayo katika utendaji hivi sasa, itatuchukua miaka 300 kufikia kiwango cha maendeleo kitakachokuwa kimefikiwa na nchi kama Kenya, Ethiopia, Rwanda na Botswana katika kipindi cha miaka 30 ijayo, iwapo mambo yataendelea kama yalivyo hivi sasa. Na hiyo itatokea iwapo hatukumbani na rabsha za kisiasa zinazoweza kuturudisha nyuma zaidi.

Nimewasikia wazee wakisema kwamba wanasiasa wa upinzani wanawakosea adabu viongozi waliotangulia kwa kusema kwamba miaka hii 50 iliyopita hakuna kilichofanyika. Nakubaliana na lawama hiyo kwani hatuwezi kusema kwamba hakuna kilichofanyika. Lakini vile vile hicho kilichofanyika hakifanani na muda huo mrefu na wala hakifanani na uwezo tuliokuwa nao ambao ungeweza kutupeleka mbali zaidi kama tusingekuwa na uongozi mbovu na mifumo ya utawala mibovu.

Kwa muda mrefu mno tumekuwa kama watu tuliokubaliana kwamba ili kupata watawala wa kuendesha mambo yetu ni lazima tupate wale wabovu kiasi kinachowezekana na tuepukane kabisa na watu wenye ujuzi, weledi na maono. Huu ndio utamaduni uliojengwa na chama-tawala kwa muda mrefu. Kwa muda wa miaka takriban 25 sijawahi kuacha kulisema hili, na sikulisema hilo kwa sababu nilikuwa mtu wa upinzani.

Chama tawala kimekuwa kikijishughulisha sana na kuziba kila mwanya uliojitokeza kuleta mabadiliko ya kweli ya kuisukuma nchi hii mbele, kikiwa zaidi kina shauku ya kulinda maslahi binafsi ya wakuu hao na washirika wao. Hii haina maana kwamba kila mtu ndani ya chama hicho ni muovu, la hasha. Hili ni suala la kimfumo, na mfumo ndio unaotawala na kuwalazimisha hata watu wema kupoteza uwezo na/au utashi wa kukemea uovu, uzembe na ufisadi.

Ndiyo maana suala kuu tunalohitaji kulishughulikia ili tupate maendeleo ya kweli, maendeleo ambayo angalau wajukuu wetu wataweza kunufaika nayo, ni kubadilisha mifumo, miundo na mikondo ya utawala wetu katika mabadiliko yatakayoondosha kabisa uchafu uliojaa katika jinsi tunavyojitawala.

Hili haliwezi kufanywa chini ya chama-tawala tulicho nacho hivi sasa kwa sababu CCM imekwisha kudhihirisha kwamba haitaki kuandika Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi. Katiba inayotakiwa na CCM ni ile iliyoandikwa na Samuel Sitta na Andrew Chenge na washirika wao, ambao wanajulikana hawawezi kuitaka Katiba itakayowabana katika yale wanayotaka kuyafanya, ambayo ni muendelezo wa ufisadi.

Jukwaa pekee ambalo mimi naliona lina uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli ni lile lililotangaza waziwazi kwamba limedhamiria kuondoa utawala mbovu uliopo kwa kung’oa mizizi yake ya kimfumo na kimuundo kwa kuandika Katiba mpya. Jukwaa hilo linapatikana ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi, Ukawa.

Angalau ndilo jina lao, Ukawa, na angalau wao wamekwisha kutuambia kwamba hiyo ndiyo dhamira yao, na tunaweza baadaye kuwavuta shati na kuwauliza imekuwaje mpaka wakatelekeza ahadi yao. CCM hatuwezi kuwauliza hilo kwa sababu hawajaliahidi hilo na wala si jambo lao hata kidogo. Walikwisha kulikataa mara nyingi.

Ukawa wametoka mbali. Tukumbuke kwamba jukwaa hili lilianza pale Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema, kilipoanza kutangaza kampeni ya M4C, Movement For Change, chama hicho kilikuwa kinatoa mwito wa kufanya mabadiliko ya kweli nchini, na mabadiliko hayo kilitaka yafanyike kwa kuandika Katiba mpya.

Baadaye, Rais Jakaya Kikwete, kwa kudhani kwamba ajenda ya Katiba mpya ingemjengea mtaji wa kisiasa, akaiteka na kuifanya yake kwa kumteua Joseph Warioba, aliyekuwa na heshima yake ndani ya jamii, na wajumbe wazito. Chama chake kilipomgomea, Rais Kikwete akageuza mwelekeo na kumwacha Warioba anyanyaswe na wahuni wa chama chake. Haiwezekani chama hicho hicho kikawa ndilo chimbuko la Katiba mpya, na mabadiliko ya kweli yatakayokuja kwa njia ya amani hayawezi kupatikana bila kuandika Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi.

Inaeleweka ni kwa nini CCM haiwezi kukubali iandikwe Katiba mpya. Madai ya wananchi wakati wa mchakato ulionyongewa njiani yalihusu kujenga mfumo unaowapa mamlaka zaidi wananchi na kupunguza mamlaka ya watawala, na kuweka utaratibu utakaohakikisha kwamba hili linatendeka. 

Bila shaka mamlaka ya rais kuteua watu asiowajua yangepunguzwa, mamlaka ya serikali za mitaa yangeongezwa na wakuu mbalimbali wangetakiwa wathibitishwe/wapitishwe na kamati za Bunge.

Haya yote ni mambo ambayo CCM haiwezi kuyakubali kwa sababu yanafinya mianya ya “patronage”, yaani utaratibu wa kuwazawadia watu wasio na sifa lakini wanapendwa na mkuu fulani. CCM haiwezi kuutaka utaratibu usiowapa uwezo huo kwa sababu huko ndiko wanakoponea mamia ya watu wasio na uwezo na sifa pekee waliyonayo ni kujipendekeza.

Siwezi kujidai kuwa na uwezo wa kubashiri ni nini Chadema/Ukawa watafanya iwapo watashinda uchaguzi huu, kwani nawajua wanasiasa wanavyofanya pindi wakiingia madarakani. Lakini angalau tutakuwa na maswali ya kuwauliza iwapo watashindwa kutekeleza yale wanayotuahidi.
 
Wengine hatuwezi hata kuwauliza.

Hata hivyo, ninaweza kusema kwamba chembe chembe za mabadiliko zimeanza kujionyesha kwa jinsi wanavyoenenda. Mwaka mmoja uliopita haikuwa rahisi kuwaona viongozi wa vyama vya upinzani wakishirikiana kufanya jambo lolote. Kuna wakati uhusiano baina ya baadhi ya vyama vya upinzani ulikuwa na aina fulani ya uhasama na kutoaminiana.

Safari hii wamepata hoja ya kuwaunganisha, na hoja hiyo ni katiba ya wananchi. Walianzia katika Bunge lililokuwa limeundwa kwa ajili ya katiba lakini likaishia patupu. Viongozi wakuu wa vyama hivyo walianza kuratibu maoni yao na ilipofika mahali wakaona kwamba wanaburuzwa, wakajitoa katika Bunge hilo.

Kutokana na kazi ya wakati ule, na kwa kuzingatia lengo lao kuu, umoja huo ukaendelea na kuchukua hatua mpya, ambayo ilkuwa sasa ni kuunganisha nguvu zao katika madai yao ya Katiba mpya, ila kwa sasa ikawa ni katika ngazi mpya, yaani ile ya kufanya kampeni ya kisiasa katika Uchaguzi Mkuu.

Hii ni hatua mpya na yenye umuhimu mkubwa. Imeonyesha kwamba vyama hivyo vinaweza kujenga umoja kuhusu hoja za msingi. Nimeewahi kuandika wakati si mrefu uliopita kwamba huko tuendako itabidi tujifunze kujenga “coalitions,’
 yaani miundo inayounganisha vyama kadhaa kwa sababu si kila uchaguzi utatoa mshindi wa moja kwa moja. Wakati mwingine itabidi iundwe serikali ya mseto. Ukawa wameanza kwa kuonyesha kwamba hili linawezekana.

Kwamba wana-Ukawa wameweza kuachiana majimbo, na hata kuachiana nafasi ya kugombea urais, si jambo dogo. Kwa bahati mbaya vyombo vya habari vimekuwa vyepesi kuonyesha pale waliposhindwa kuafikiana juu ya mgombea katika nafasi za ubunge na udiwani. Lakini hizo nafasi ni chache mno zikilinganishwa na mwafaka uliopatikana kote nchini, na nadhani huu ni mwanzo mwema katika kujifunza kufanya kazi ndani ya mseto (coalition).

Kazi hii inatakiwa kuendelezwa. Iwapo Ukawa watashinda, wataunda serikali ya pamoja. Iwapo watashindwa, wataendelea na kampeni ya kudai katiba mpya itakayojali maoni ya wananchi. Kwa vyovyote vile, Ukawa itakuwa imeandika historia mpya ya kisiasa Tanzania.

Kama kuna chembe yoyote ya mabadiliko ya kweli, chembe hiyo itapatikana Ukawa na si kwingineko.


No comments :

Post a Comment