Mwenyekiti wa tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Nyanduga.
Dar es Salaam. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka mawakala wa vyama vya siasa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu katika kulinda kura za wagombea wa vyama vyao, ili Uchaguzi Mkuu umalizike kwa amani na utulivu.
Pia, THBUB imeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wasimamizi wa uchaguzi na mawakala kuhakikisha mchakato mzima wa kupiga kura, kuhesabu, kubandika na kutangaza matokeo unafanyika kama sheria inavyotamka ili kuepuka manung’uniko.
Taasisi hiyo imetoa tamko hilo wakati Watanzania wakipiga kura leo kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani.
Upigaji kura unaanza saa 1:00 asubuhi na utakoma saa 10:00 jioni na kura kuanza kuhesabiwa. NEC imeahidi kukamilisha kuhesabu matokeo ya urais ndani ya saa 72.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa ni jukumu la vyama vya siasa kuhakikisha mawakala wake wanatimiza wajibu wao kwa uaminifu kwenye vituo walivyopangiwa.
Nyanduga alisema kwa kuwa mawakala wa vyama hivyo wanatajwa kisheria kuwa ndio walinzi wa kura za wagombea, hakuna haja ya wananchi kuwa na wasiwasi kuhusu suala la ulinzi wa kura.
“Mawakala watambue wajibu wao na wahakikishe wanazingatia taratibu za uchaguzi, kwa kuwa wamekula kiapo cha uaminifu basi ni jukumu lao kufanya kazi kwa uaminifu ili watimize wajibu wao kwa weledi,” alisema.
Nyanduga pia alilitaka Jeshi la Polisi, NEC, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na wadau wengine wanaohusika kisheria, kutimiza majukumu yao kwa kufuata kanuni za uchaguzi ili kudumisha misingi ya utawala bora. Alisema polisi wanatakiwa kutumia weledi katika kutoa ulinzi kama lilivyofanya wakati wa kampeni za uchaguzi zilizomalizika jana.
Nyanduga aliongeza kuwa tume hiyo inaamini kuwa utawala wa sheria ni lazima uheshimiwe na kila mtu, hasa vyombo vya dola na mamlaka za Serikali, ili misingi ya utawala bora na haki za binadamu ifuatwe.
“Ni wajibu wa Jeshi la Polisi kutoa ulinzi mahsusi, bila vitisho ili kuhakikisha kazi ya kupiga kura inafanyika kwa amani na kwa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora,” alisema.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati wa wote wa uchaguzi, kuanzia hatua ya kupiga kura na kusubiri matokeo kwa amani.
Kuhusu wagombea na viongozi wa vyama vya siasa, Nyanduga alisema wanatakiwa kuepuka lugha zinazoweza kusababisha hofu, vurugu na uvunjifu wa amani wakati zoezi la uchaguzi linapoendelea na kupokea matokeo.
Tume hiyo imewataka wananchi watakaobaini uvunjifu wowote wa haki za binadamu au uvunjifu wa sheria ya uchaguzi, kuzijulisha mamlaka zinazosimamia uchaguzi.
Hata hivyo, aliwapongeza wananchi kwa jinsi walivyoonyesha utulivu wakati wa mikutano mikubwa ya kampeni, ambayo ilikuwa ikiwavutia watu wengi.
No comments :
Post a Comment