Saturday.
Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) leo imewaonesha waandishi wa habari na waangalizi wa uchaguzi matayarisho ya tume hiyo pamoja na namna watakavyohesabu matokeo katika kituo cha kurushia matokeo hayo hapo Bwawani Hoteli..
Matangazo hayo yanatarajiwa kurushwa katika kituo cha Hoteli ya Bwawani yalioneshwa na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Salum Kassim Ali na kuwataka waandishi wa habari na waangalizi kuwa makini na kupokea matangazo hayo huku wakizungatia matangazo hayo yatatolewa katika kituo kikuu cha Bwawani pekee.
“Nataka tuwe makini hapa katika kutangaza haya matokeo tutakapotangaza haya matokeo mseme ni matokeo ya awali na sio matokeo ambayo yameshajumlishwa kabisa tunaomba sana hilo mlijue” alisema Kassim.
Hata hivyo aliwaambia waandishi kwamba kurushwa kwa matokeo hayo iwe ni mfano na isichukuliwe kama ndio matokeo halisi ambayo yameshatolewa na tume hiyo.
“Jamani huu ni mfano wa kutangaza matokeo msije mkasema tumepika matokeo tunakuombeni sana kwamba matokeo haya ya wagombea ni matokeo ambayo ni mfano tu na sio matokeo halisi” aliongeza.Kassim akiongea tahadhari aliwakumbusha waandishi kufanya kazi kwa uadilifu na kujiepusha na kutoa matangaza ambayo wamepokea katika vituo mbali mbali vya wapiga kura ambayo hubandikwa vituoni baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la upigaji uhesabuji wa kura litakapokamilika hii leo.
“Pia tunawakumbusha mtakapotoa matangazo mseme kwamba haya ni matokeo ya awali na sio matokeo sahihi kwa sababu kunaweza kutokea kura kuharibika kuna kura ambazo zilikuwa hazijahesabiwa na mambo kama hayo kwa hivyo tunakuombeni sana msije mkatangaza mkasababisha kuleta uvunjifu wa amani” alitahadharisha Mkurugenzi huyo ambaye hakutaka kupigwa picha wala kurikodiwa.
Katika hatua nyengine tume hiyo inalalamikiwa kwa kuchelewa kutoa vitambulisho vya mawakala ambao watasimamia vyama vya siasa katika zoezi zima la upigaji kura na kuhesabu kura hizo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya vyama vya siasa wamesema kukosekana kupewa vitambulisho mapema ni udhaifu wa tume hiyo kwa kuwa suala la vitambulisho lilitakiwa likamilke mapema iwezekanavyo na kila mtu awe ameshajua kituo chake cha kusimamia upigaji kura mapema.
“Tume ya uchaguzi imeonesha udhaifu hadi sasa kutowapa mawakala vitambulisho ni tatizo kwa sababu khofu yetu hapo kesho inaweza kuleta kmanganyiko iwapo watachelewa kutoa hivyo vitambulisho” alisema Mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF, Mhene Said Rashid.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa ACT- Mzalendo Juma Said Sanani amesema kukosekana kupewa vitambulisho mapema mawakala kutasababisha watu wengi kukosa haki yao ya kupiga kura kwa kuwa asubuhi muda wa pirikapirika.
“Mawakala wetu wanaweza kuchelewa kupewa vitambulisho mchakato wa upigaji kura uanweza kuendelea na kusiwepo na mawakala mle ndani” amesema Sanani.
Wanasiasa hao wamesema tatizo kubwa la kuchelewa kupewa vitambulisho linaweza kusababisha usumbufu asubuhi wakati wa upigaji kura.
“Khofu yetu ni kwamba ikifika asubuhi hatuna vitambulisho tutakosa kuingia ndani ya vituo na tukikosa kuingia ndnai inaweza ikawa ni sababu moja ya kufanyiwa hujuma vyama vyetu” amesema mmoja wa mawakala.
Akizungumzia suala hilo Mkurugenzi wa Uchaguzi Salum Kassim alisema hakuna sababu ya kuwa na khofu kwa kuwa suala la vitambulisho hutolewa asubuhi siku ya upigaji kura na kila wakala atapewa kitambulisho chake.
Source: Salma Said / Zanzibari Yetu.
No comments :
Post a Comment