dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, November 19, 2015

Waziri Mkuu ni Kassim Majaliwa?

Rais Dk. John Magufuli.
Wakati kitendawili cha nani atakuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli, kikitarajiwa kuteguliwa leo, kuna kila dalili mteule wa nafasi hiyo anatarajiwa kuwa Mbunge wa Ruangwa (CCM), Kassim Majaliwa.
Majaliwa alikuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa serikali ya awamu nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Latest news hizi hapa:
Siyo jina kubwa kwenye medani ya siasa na aliingia katika medani hiyo mwaka 2010 baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Ruangwa na kuteuliwa kushika wadhifa huo serikalini na kudumu nao hadi Rais Kikwete alipong’atuka.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya duru za serikali zinasema Rais Magufuli anataka kuteua mtu mpya atakayetekeleza kauli mbiu yake ya `Hapa kazi tu’.
Rais Magufuli atamkabidhi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, jina la Waziri Mkuu leo asubuhi, ambaye atalitagaza na baadaye jioni kupigiwa kura.
Uchunguzi wa Nipashe kupitia vyanzo vyake mbalimbali umebaini kuwa Waziri Mkuu huyo, ambaye atalazimika kupitishwa na bungeni kupitia kura zitakazopigwa leo kabla Magufuli hajalizindua Bunge hilo kesho, umebaini kuwa jina la mteule huyo halijawa wazi kwa watu wengi, tofauti na  walioteuliwa kushika nafasi hiyo katika serikali iliyopita ya awamu ya nne.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, watu wengi walitabiri kwa usahihi kuwa angemteua Edward Lowassa, kuwa Waziri Mkuu. 
Na hicho ndicho kilichotokea, kwani siku chache baadaye, jina la Lowassa liliwasilishwa bungeni na mwishowe akapitishwa na wabunge kwa kishindo kuwa Waziri Mkuu.
Kadhalika, inaelezwa vilevile kuwa hata baada ya Lowassa kujiuzulu kufuatia sakata la mitambo ya kufua umeme ya Richmond, wengi walitabiri kuwa Mizengo Pinda, angeteuliwa na Rais Kikwete kuwa Waziri Mkuu. Na ndivyo ilivyokuwa.
Hata hivyo, Nipashe imebaini kuwa hivi sasa tetesi kuhusiana na jina la Waziri Mkuu wa Serikali ya Dk. Magufuli, ziko tofauti sana kulinganisha na vile ilivyokuwa katika uteuzi wa Lowassa ambaye sasa yuko Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Pinda.
Hata hivyo, Nipashe imethibitishiwa na chanzo cha uhakika kuwa Majaliwa ndiye anayepewa nafasi kubwa kushika wadhifa huo.
Majaliwa anaaminika kuwa ameonekana kuwa ana uwezo wa kuendana na kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli katika kuhakikisha kuwa ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni zinatimizwa.
Kwanini karata dume itamwangukia Majaliwa?
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua viashiria kadhaa ambavyo vinadokeza kuwa Majaliwa ndiye atashika nafasi ya Waziri Mkuu.
Kwanza, ni kitendo chake cha kushika wadhifa wa Naibu Waziri kwenye ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka mitano, kumemfanya kuvuna uzoefu wa kufanya shughuli za taasisi hiyo na kukidhi vigezo vya kuaminiwa kupewa nafasi hiyo.
Pia ukizingatia kuwa Majaliwa ndiye aliyekuwa na jukumu la kusimamia masuala ya elimu kwenye Tamisemi, ambayo ni miongoni mwa ahadi kubwa za Rais Magufuli.
Ikumbukwe kuna suala la utekelezaji wa ahadi ya elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Kutokana na uzoefu wake wa kuongoza masuala ya elimu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, kunamwongezea sifa ya kushika nafasi hiyo.
Kutokana na ukweli kuwa sifa mojawapo ya Waziri Mkuu anatakiwa kuwa mtu ambaye anaujua mfumo wa serikali, ndiyo maana kunafanya jina la Majaliwa kutajwa kushika nafasi hiyo.
Nipashe pia limedokezwa uwezekano wa Majaliwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo umeongezwa na taarifa kuwa hata staili yake ya maisha katika siku za karibuni imebadilika.
Kuna taarifa zimedokeza kuwa familia yake yote kwa sasa iko mjini Dodoma huku kukiwa na ulinzi mkali kwenye nyumba ya serikali anayoishi eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa na familia yake wamekwenda Dodoma tangu Jumapili iliyopita. Nyumbani kwake hakuna mtu kwa sasa,” alidokeza mmoja wa wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ambaye hata hivyo, siyo msemaji wake rasmi.
Mmoja aliye karibu na Majaliwa, naye aliiambia Nipashe hajawasiliana na kwa njia ya simu na Majaliwa tangu Jumapili iliyopita.
“Unajua ninafahamiana na Mheshimiwa Majaliwa kwa miaka mingi. Huwa ninamsaidia shughuli zake nyingi. Siyo kawaida yake kutojibu simu. Hata kama hatapokea, basi ni mwepesi kupiga baadaye. Nadhani kuna kitu hapa. Nina wasiwasi. Ila yote kheri kama mambo yatamnyookea,” alidokeza rafiki yake wa karibu, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.
Pia kutajwa kutokana na ukweli kuwa Majaliwa anatoka Mkoa wa Lindi ambao Kanda ya Kusini kunafanya awe na nafasi kubwa.
Kutokana na ukweli kuwa suala la jiografia huzingatiwa ingawa siyo la kikatiba, lakini uwezekano wa Waziri Mkuu kutoka Kanda ya Ziwa ni mdogo.
Wengine wanaopewa nafasi kubwa
Chanzo kimoja kiliidokeza Nipashe juzi kuwa awali waziri mkuu huyo atakayetajwa leo, ana ishara kubwa nne zinazomwezesha yeyote kumtambua.
Sifa hizo ni pamoja na mahali atokako ambako siyo Kanda za Magharibi, Ziwa wala Kaskazini. 
Sifa ya pili ya mtu huyo ni kutowahi kujitokeza katika mbio za kuwania urais ndani ya CCM; sifa yake ya tatu ni kwamba hajawahi kudhaniwa kushika nafasi hiyo na sifa ya nne amewahi kushikilia nafasi ya uwaziri/naibu waziri katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete iliyomaliza muda wake Novemba 5, mwaka huu.
Pamoja na Majaliwa, wengine wanaoangukia kwenye kundi hilo ni Mbunge wa Peramiho aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama, Mbunge wa Kibakwe aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene na Mbunge wa Bagamoyo aliyekuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Wengine waliomo katika orodha hiyo ya wabunge saba wanaotajwa kuwa wanaweza kupewa nafasi hiyo ni Mbunge wa Newala, Kapteni George Mkuchika, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na pia Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Juma Nkamia.
Majina mengine yanayotajwa 
Pamoja nao hao, wengine ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitajwa tajwa ni William Lukuvi, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu; aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na pia aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu. 
YANAYOJIRI BUNGENI
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, jina la Waziri Mkuu litajulikana leo baada ya Rais Magufuli kuliwasilisha ili wabunge walipigie kura.
Baadhi ya wabunge walisema hivi sasa ni vigumu, bali kila mbunge kwa sifa anazozijua atataja mtu anayefikiri kuwa anafaa kuwa Waziri Mkuu na siyo rasmi kutoka ndani ya Chama.
"Ninachokiona Rais huyu amerudisha hadhi ya Ikulu kama taasisi, mambo yanakwenda kwa siri sana, ni vigumu sana kuvuja tofauti na serikali iliyopita, yapo yaliyovuja mapema, hii inatokana na kwamba Rais huyu aliingia madarakani kwa nguvu zake na Chama na siyo mtandao wa watu ambao analazimika kuwasikiliza," alisema mmoja wa wabunge hao.
Kwa mujibu wa ratiba, leo asubuhi itakuwa ni kupiga kura za Naibu Spika, baada ya wabunge wote kumaliza kula viapo vya kuthibitisha kuutumikia umma na kuilinda na kuitetea Katiba.
Mbunge wa kuteuliwa, Dk. Tulia Ackson ndiye anayewania nafasi hiyo kupitia CCM wakati Mbunge wa Urambo Magharibi (CUF), Magdalena Sakaya, atapeperusha bendera ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). 
Vyama hivyo ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment