dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, February 12, 2016

Hamad akaribia Umakamu Zanzibar!

Hon. Hamad Rashid Mohamed.
1st Vice-President of Zanzibar-in-waiting!

Raia Mwema
Toleo la 444
10 Feb 2016
CHAMA
kipya cha siasa nchini, Alliance for Democratic Change (ADC), kinakaribia kuweka historia mpya ya kisiasa Zanzibar endapo mgombea wake wa urais, Hamad Rashid Mohamed, atafanikiwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Zanzibar unafanyika Machi 20 mwaka huu, huku chama kikuu cha siasa cha upinzani visiwani humo –Chama cha Wananchi (CUF) kikiwa tayari kimetangaza kuususia kikidai kuwa ni batili. 


Hata hivyo, chama hicho cha Hamad; ambaye kwa takribani miaka 30 iliyopita alikuwa swahiba wa kisiasa wa aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Seif Shariff Hamad, kabla ya kutofautiana mwaka 2010, kimetangaza kushiriki katika uchaguzi huo. Uchaguzi huo unarudiwa baada ya ule uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana kufutwa kutokana na kile kilichoelezwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa ni ukiukwaji wa taratibu kadhaa za uchaguzi huo. 

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar, chama kilichoshinda katika Uchaguzi Mkuu kinatakiwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na chama kilichoshika nafasi ya pili, ilimradi chama hicho kimepata walau asilimia tano ya kura zilizopigwa kinashika nafasi ya makamu wa rais. 

Kwa kawaida, chaguzi zilizopita za Zanzibar zilikuwa na upinzani mkali; huku tofauti kati ya mshindi na aliyeshindwa ikiwa ni chini ya asilimia tano na katika hali ya kisiasa ya sasa ya Zanzibar, vyama hivyo viwili ni CCM na CUF.
Lakini, kujitoa kwa CUF kwenye uchaguzi huo (na hiyo ni kama itabaki hivyo hadi Machi 20 mwaka huu), Zanzibar inaweza kujikuta ikiwa na Makamu wa Rais kutoka katika chama ambacho hakikuwa kinapewa nafasi ya kupata wadhifa huo. 

Hamad Rashid Mohamed ni nani? 
Hamad ni mzaliwa wa Wawi, Pemba na ni mmoja wa wanasiasa wakongwe walio katika vyama vya upinzani hivi sasa. Amewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Jimbo la Wawi. 

Alijenga jina lake akiwa miongoni mwa waliokuwa wakifahamika kama “The Young Turks”, ambalo lilikuwa ni kundi la wanasiasa vijana na wenye elimu waliopata fursa ya kusomeshwa na kupata maarifa wakati wa uongozi wa Rais Aboud Jumbe Mwinyi wa Zanzibar. Wakati wa enzi ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume, watu hawakuruhusiwa kusoma kufikia kiwango cha chuo kikuu visiwani humo (ikielezwa kuwa wahafidhina walikuwa na hofu ya wasomi) na amri hiyo iliondolewa wakati wa Jumbe. 

Hamad Rashid Mohamed na Seif Shariff Hamad walikuwa miongoni mwa vijana ambao hatimaye waliunga mkono hatua ya Jumbe kuvuliwa urais na nyadhifa zake zote kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa Zanzibar na mara kwa mara walikuwa wakielezwa kutoelewana na wahafidhina wa Mapinduzi ya mwaka 1964 kama vile Kanali Seif Bakari, Abdallah Natepe, Said Washoto na Brigedia Yusuf Himidi. 

Mwishoni mwa miaka ya 1980, Hamad na Maalim Seif walifungwa pamoja jela kwa madai ya kupanga njama za kuipindua Serikali ya Rais Idris Abdul Wakil na wote walipotoka jela walikuwa waanzilishi wa umoja ulioitwa KAMAHURU uliokuja kuzaa CUF baadaye. Wakati Maalim Seif alijenga ngome yake ya kisiasa Zanzibar, Hamad mara nyingi alikuwa akitafuta uhusiano na kutengeneza mtandao wa chama hicho Tanzania Bara na mara nyingi ilikuwa ikionekana kuwa yeye ndiye aliyekuwa namba mbili ndani ya CUF. 

Pamoja na urafiki wao huo; Maalim Seif na Hamad Rashid ni watu wawili tofauti. Wakati Maalim ni mwanasiasa unyayoni mpaka utosini, Hamad ni mwanasiasa-mjasiriamali; ambaye uwezo wake wa kupenya kwenye sekta binafsi ulikuwa muhimu kwa CUF. Kwenye mojawapo ya mahojiano ambayo Hamad Rashid amewahi kufanya katika miaka ya nyuma, aliwahi kusema kwamba yeye na Maalim wamefahamiana tangu wangali na umri wa chini ya miaka 20. 

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ndiyo uliovuruga uhusiano wao; baada ya Hamad Rashid kudai kwamba Maalim Seif alikiuza chama chao kwa kukubali matokeo ya uchaguzi huo yaliyoipa ushindi CCM. Hadi sasa, Hamad Rashid anaamini kwamba CUF ilishinda katika uchaguzi ule na kwamba kama si “makubaliano binafsi” baina ya Maalim na vigogo wa CCM, huenda chama chao kingetangazwa mshindi. Misimamo hiyo kinzani, ya Maalim Seif kukubali matokeo hayo na Hamad kupinga hatua hiyo ilikuwa mwanzo wa mgogoro wao na ilifikia wakati CUF kikaamua kumvua mbunge huyo wa zamani wa Wawi uanachama wa chama hicho. 

Hamad azungumzia Umakamu Katika mahojiano na gazeti hili yaliyofanyika wiki hii, Hamad alisema ana uhakika wa kupata asilimia tano ya kura katika uchaguzi huo wa marudio kwa sababu ‘hatachezewa rafu’ zilizochezwa katika uchaguzi uliofutwa. “Nina matumaini kwamba nitapata zaidi ya asilimia tano kwenye uchaguzi huu wa marudio. Sababu ziko nyingi na nitataja chache. Mosi ni kwamba kwenye uchaguzi uliofutwa, nilichezewa rafu nyingi.

 “Kule Pemba nilikozaliwa, watu walisambaza karatasi za kupigia kura zilizoonyesha kuwa mimi nawania nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, jambo ambalo halikuwa la kweli. Watu waliofahamika kuwa wananiunga mkono walifanyiwa vitisho. Ushahidi wa yote huo ninao. “Sasa kwenye uchaguzi huu hakutakuwa na vitendo hivyo. Watu hawatapewa taarifa za kudanganywa na wafuasi wangu watanipigia kura. Lakini pia, wananchi wa Zanzibar wanajua hasara za kususia uchaguzi. 

“Wazanzibari, hasa hasa wale wa Pemba, wanajua hasara za kuiacha CCM ishiriki uchaguzi yenyewe. Watafanya wanalolitaka na wanavyotaka. Wale waliokuwa nasi tangu mwaka 1985 wakati tulipopiga kura za ukuta kule Pemba, wanajua kuwa kususa hakufanyi kazi. “Unapomsusia nguruwe shamba lako unategemea nini? Ukirudi kesho utakuta kala mimea yako yote. Kususia uchaguzi si suluhisho na Wazanzibari wanaojua hilo watapiga kura kwa ADC,” alisema. 

Katika hatua nyingine, Hamad alisema anaunga mkono uamuzi wa CUF kususia uchaguzi huo wa marudio kwa vile unaendana na msimamo wao wa awali wa kususia uchaguzi. Alisema kama CUF ingekubali kushiriki katika uchaguzi huo, ingekuwa inakubali kuwa uchaguzi uliofutwa ulifutwa kihalali. 

Alisema wao ADC watashiriki katika uchaguzi huo kwa sababu msimamo wao tangu awali ulikuwa kwamba uchaguzi ule ulikuwa batili kwani ulikiuka taratibu nyingi. Alipoulizwa na Raia Mwema kuhusu hali hii ya Zanzibar, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema hana la kuzungumza kuhusu jambo hilo. “Mimi sina cha kusema kwenu,” alisema Jussa kwa ufupi.
 - See more at: http://raiamwema.co.tz/hamad-akaribia-umakamu-z%E2%80%99bar#sthash.JldVctz7.dpuf

No comments :

Post a Comment