dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, February 3, 2016

Jaji Mkuu: Mahakama ya mafisadi ni kipaumbele

Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman.
By James Magai, MWANANCHI.
Dar es Salaam. Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman amesema suala la uanzishwaji wa Mahakama maalumu ya kushughulikia makosa makubwa ya ufisadi, rushwa na uhujumu uchumi ndicho kipaumbele kikuu na cha kwanza kwa mhimili huo wa dola mwaka huu.
Jaji Mkuu alisema hayo jana alipozungumza na mwandishi wa Mwananchi kuhusu mchakato wa uanzishwaji wa mahakama hiyo ambao unatokana na ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni zake katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na vitendo vya ufisadi.
Novemba mwaka jana, Jaji Kiongozi, Shaban Lila alikaririwa na gazeti hili akisema tayari mchakato wa uanzishwaji wa mahakama hiyo umeshaanza kwa wadau wa haki jinai kujadili iwapo ianzishwe kama kitengo ndani ya Mahakama Kuu au iwe Mahakama huru.
Lakini jana, Jaji Mkuu alisema wamekubaliana kuwa itakuwa chini ya Mahakama Kuu.
Alisema mchakato huo unafanywa na Mahakama kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria , Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (CAG), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Polisi.
“Hii ni kipaumbele chetu cha hali ya juu sana, ni ‘top top top priority,’” alisema kwa msisitizo.
Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya kushughulikia kesi nyeti za jinai Novemba mwaka jana, Jaji Kiongozi Lila alisema kesi za makosa makubwa ya jinai za ufisadi, utakatishaji fedha, usafirishaji dawa za kulevya, usafirishaji nyara za Serikali na ugaidi zimekuwa zikizidi kuongezeka.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema mchakato wa uanzishwaji wa Mahakama hiyo unakwenda vizuri na kwamba muda si mrefu atatoa taarifa.
Wakati wa kampeni, Dk Magufuli alikuwa akisisitiza kuwa atapambana na rushwa na ufisadi kwa kuanzisha Mahakama maalumu ya kushughulikia makosa hayo na kwamba hatakuwa na mzaha jambo ambalo alilirejea wakati akizindua Bunge, Novemba 20, 2015.
Alisema wananchi wamechoshwa na rushwa na ufisadi na kwamba hata yeye ni miongoni mwa wanaoachukizwa na vitendo hivyo vinavyoendelea kukithiri nchini.

No comments :

Post a Comment