Kada mkongwe na muasisi wa chama Cha Mapinduzi (CCM) , Pius Msekwa.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya CCM kuadhimisha miaka 39 tangu kuzaliwa kwake, kada mkongwe na muasisi wa chama hicho, Pius Msekwa amesema kuna haja ya kufanya mabadiliko ndani ya chama hicho hasa muundo wa halmashauri kuu ya taifa.
Katika chapisho lake kuhusu tathmini ya miaka 39 ya chama hicho itakayochapwa kesho katika gazeti hili, Msekwa amesema mabadiliko hayo yanahitajika kufanywa kabla ya mwenyekiti wa sasa wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete kukabidhi kijiti hicho kwa Rais John Magufuli.
Msekwa ambaye ni katibu mkuu wa kwanza wa Tanu alisema uzoefu unaonyesha kwamba mageuzi yaliyofanyika kwenye chama hicho mwaka 2011 katika muundo wa ngazi ya Taifa, hususan wa halmashauri kuu, hayakuleta tija iliyokuwa imetegemewa.
“Kwa ajili hiyo, ingefaa sana kama chama kingerejea kufanya mabadiliko mengine ya muundo wake, ili kumuwezesha mwenyekiti mpya aweze kuanza na muundo mpya ulioboreshwa,” alisema. Msekwa ambaye pia ni makamu mwenyekiti mstaafu wa chama hicho alibainisha kuwa muundo huo ulibuniwa katika kipindi cha utawala wa chama kimoja kwa lengo maalumu la kutekeleza sera iliyokuwapo wakati huo ya “chama kushika hatamu za uongozi” wa nchi.
“Lakini katika hali iliyopo sasa, ni dhahiri kwamba halmashauri kuu ya taifa imekuwa ni kubwa mno, yenye wajumbe zaidi ya 480... Kwa sababu zote hizo, inafaa kabisa kwamba chama kitumie fursa hii ya mabadiliko ya mwenyekiti wake, kufanya mabadiliko ya kupunguza ukubwa wa halmashauri kuu.”
Mbunge huyo wa zamani wa Ukerewe alisema athari zake ni kwamba mbali na gharama kubwa za kuhudumia vikao vyake, wajumbe walio wengi hawafanyi kazi za chama katika wilaya zao, bali wanatumia muda wao mwingi kujiandaa kugombea ubunge huku akisema utunzaji wa siri za kikao hicho muhimu umekuwa mgumu.
Alisema Katiba ya mwanzo ya CCM, toleo la mwaka 1977 ilikuwa na halmashauri kuu ya Taifa ndogo tu, na pia kamati kuu ndogo, na haikuwa na kikao cha sekretarieti kama ilivyo sasa.
Alisema mabadiliko makubwa yalikuja kufanyika baada ya kupitishwa kwa “Mwongozo wa CCM wa mwaka 1981” ambao ulikomalia kwelikweli suala la chama kushika hatamu za uongozi.
Alisema kutokana na mwongozo wa 1981, kikao cha halmashauri kuu ya Taifa kilifanywa kuwa kipana na chenye wajumbe wengi kwa kuongeza kundi jipya la wajumbe 90.
Miongoni wajumbe hao ni wa kamati kuu, sekretarieti ya halmashauri kuu ya Taifa na makatibu wa mikoa.
Kuhusu kamati kuu, Msekwa alisema Katiba ya mwanzo ilikusudia iwe ni kikao kidogo cha kumshauri mwenyekiti wa chama katika mambo ya uendeshaji wa shughuli za kila siku.
“Kamati hii mwanzoni ilikuwa ni ndogo sana, yenye wajumbe 15 tu. Na ndiyo sababu iliwekewa vikao vya mara nyingi zaidi, ili iweze kutekeleza wajibu huo kwa ufanisi,” alisema.
Kuhusu sekretarieti, Msekwa alisema katiba ya mwanzo haikuwa na sekretarieti, lakini ilikuja kubuniwa baadaye katika vuguvugu la utekelezaji wa sera ya chama kushika hatamu za uongozi.
Alisema kamati kuu ilifananishwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ambalo wajumbe wake lazima watoke miongoni mwa wabunge.
Lakini alisema, mabadiliko hayo yote yalifanyika katika kipindi cha utawala wa chama kimoja kwa lengo la kukifanya kionekane dhahiri kwamba kinashika hatamu za uongozi wa nchi.
Alisema chini ya mfumo uliopo sasa wa vyama vingi vya siasa, kazi ya kushika hatamu za uongozi kwa maana ya kusimamia na kuishauri Serikali ni kazi ya Bunge kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
“Kwa maneno mengine, msingi wa majukumu ya chama umebadilika kabisa,” alisema.
Akielezea kuhusu suala la kura za maoni katika chaguzi za ndani ya chama, Msekwa alisema jambo hilo pia linahitaji kuangaliwa upya. “Hii ni kwa sababu kuna wasiwasi kwamba kura za maoni hivi sasa zimekuwa ni chanzo kikubwa cha rushwa ndani ya chama. Kwa kifupi, faida iliyokusudiwa kupatikana kutokana na utaratibu huu wa kura za maoni kupigwa na wanachama wote, ikawa imepotea. Ndiyo sababu kuna haja ya kuangalia utaratibu huu upya.”
No comments :
Post a Comment