dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, March 31, 2016

Elimu bure ni majanga.

Wanafunzi darasa la sita (kushoto) na darasa la saba (kulia) Shule ya Msingi Majimatitu, jijini Dar es Salaam wakisoma chini ya mti. Jumla ya wanafunzi 1,025 wa wameandikishwa darasa la kwanza katika shule hiyo mwaka huu.

Wakati baadhi ya shule za msingi zikilazimika kufungwa kupisha ujenzi wa madarasa, kutokana na ongezeko la wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka huu, hali ni mbaya zaidi kwenye maeneo mengine, kutokana na  wanafunzi wa madarasa tofauti kusomea kwenye darasa moja, wakiwa wamegeuziana migongo.
 
Hali hiyo pamoja na mambo mengine, imechangiwa na mpango wa serikali wa elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne na kufuta michango yote iliyokuwa inatolewa na wazazi.
 
Kutokana na madarasa kuwa machache, wanafunzi wengine katika baadhi ya maeneo, wanasomea chini ya mti mmoja zaidi ya darasa moja huku wakiwa wamegeuziana migongo hali inayofanya kuwe na mwingiliano wa walimu wakati wakifundisha.Mbali na upungufu wa vyumba vya madarasa, matatizo mengine shule hizo pia zinakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo, madawati na walimu.
 
Miongoni mwa shule za msingi ambazo zimeelemewa ni Shule ya Msingi Majimatitu, iliyoko Mbagala jijini Dar es Salaam yenye wanafunzi 1,025 wa darasa la kwanza, ambao wanasomea chini ya mti.
 
Nyingine ni Shule ya Msingi Lupemba, iliyoko Magu mkoani Mwanza, ambayo ina wanafunzi 651. Shule hiyo ilifungwa kwa muda usiojulikana mapema mwaka huu, ili kupisha ujenzi wa vyumba walau vinne vya madarasa. 
 
Aidha, kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Zawa, Maswa mkoani Simiyu, wanafunzi wa shule hiyo wanalazimika kusoma darasa moja kwa kupeana migongo.
 
Shule hiyo ina vyumba vitatu vyenye wanafunzi 513, kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, huku wakitumia mbao mbili katika chumba kimoja. Hali hiyo inasababisha wakati mwalimu akifundisha darasani,  kuwapo kwa mwingiliano wa masomo. 
 
Akizungumza na Nipashe hivi karibuni, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, William Timoth, alisema wamegawa madaraja matatu kulingana na idadi ya madarasa saba, ili wanafunzi wote wapate masomo bila kujali uhaba wa vyumba.
 
Kadhalika, wanafunzi wa darasa la tano na la tatu katika Shule ya Msingi Mkapa, Masasi mkoani Mtwara, wanalazimika kusomea chini ya miti, kutokana na shule hiyo kukabiliwa na ukosefu wa vyumba vya madarasa. Shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa walimu, matundu ya vyoo ambayo yako manne wakati mahitaji ni matundu 10 pamoja na samani mbalimbali za ofisi, zikiwamo meza na viti.
 
MBEYA MZIGO MZITO
Kwa upande wake, mkoa wa Mbeya umeandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 84,099, idadi ambayo inadaiwa kuvunja rekodi tangu kuanzishwa kwa mkoa huo.
 
Akizungumza na Nipashe ofisini kwake, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Charles Mwakalila, alisema idadi hiyo ya wanafunzi haijawahi kutokea na kwamba imekuwa chanzo cha upungufu wa vifaa mbalimbali vya kufundishia na kujifunzia.
 
Alisema ongezeko la wanafunzi hao limesababisha pia upungufu wa walimu, madawati, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.
 
Mwakalila alisema mkoa kwa sasa una upungufu wa madawati 81,738 kwa shule za msingi na sekondari, ambayo ni idadi kubwa kuwahi kutokea na kwamba chanzo cha kuongezeka kwa tatizo hilo ni idadi kubwa ya watoto wa darasa la kwanza walioandikishwa kwa wingi kuzidi uwezo.
 
Alisema asilimia kubwa ya upungufu wa madawati ni kwa upande wa shule za msingi na kwamba upungufu kwa shule za sekondari ni madawati 1,773 tu.
 
Mwakalila ambaye kwa sasa anasimamia mikoa miwili, Mbeya na mkoa mpya wa Songwe, alifafanua kuwa ili kumaliza tatizo hilo katika mikoa hiyo, yanahitajika madawati 224,632. Alisema kwa sasa kuna madawati 142,894, hivyo upungufu ni madawati 81,738.
 
Alisema mikoa hiyo pia inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, ambavyo asilimia kubwa pia ni katika shule za msingi.
 
Alisema vyumba vya madarasa vinavyohitajika ni 14,120 kwa shule za msingi huku vilivyopo vikiwa 7,868 na kufanya upungufu kuwa vyumba 6,252.
 
Kwa upande wa matundu ya vyoo katika shule za msingi, alisema yanahitajika 20,838 huku yaliyopo yakiwa hayafikii nusu ya mahitaji.
 
Mwakalila alisema matundu ya vyoo yanayohitajika ni 9,463 na kwamba upungufu ni matundu 11, 375 huku katika shule za sekondari upungufu ukiwa ni matundu 1,795.
 
Kadhalika, alisema mikoa yake ina upungufu wa walimu wapatao 1,773 katika shule za msingi na kwamba mahitaji ni walimu 117,366 huku waliopo wakiwa ni 115,593.
 
SINGIDA VYOO SHIDA
Licha ya kutopatikana kwa taarifa ya mkoa mzima wa Singida, hali ilivyo katika Manispaa ya Singida ni kielelezo kuwa mkoa huo unahitaji jicho la ziada ili kufanikisha elimu bure.
 
Jumla ya wanafunzi 5,101 sawa na asilimia 114.37 wa darasa la kwanza wameandikishwa mwaka huu, tofauti la lengo lililowekwa la kuandikisha wanafunzi 4,460.
 
Pia wanafunzi 4,759 wa elimu ya awali sawa na asilimia 113.09 kati ya lengo la 4,208 lililokusudiwa kuandikishwa, wameandikishwa hadi sasa katika Manispaa ya Singida.
 
Ofisa elimu msingi katika manispaa hiyo, Eugene Shayo, alisema uandikishaji bado unaendelea na wanakusudia kutakuwa na ongezeko kubwa zaidi la wanafunzi kwa madarasa hayo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu.
 
Aidha, alisema upungufu wa madawati ni 3,580 sawa na asilimia 50.22. Mahitaji halisi ni madawati 7,129 na yaliyopo ni 3,549.
 
Hata hivyo, katika kukabiliana na tatizo hilo, alisema manispaa hiyo imetenga Sh. milioni 150 katika mwaka wa fedha 2016/17 kwa ajili ya kutengeneza madawati 2,000.
 
Mbali na upungufu huo, alisema manispaa hiyo inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 275 sawa na asilimia 41.86 ya vyumba 657 vinavyotakiwa. Alisema kwa sasa vilivyopo ni 382.
 
Kuhusu matundu ya vyoo, alisema manispaa ina upungufu wa matundu 541, sawa na asilimia 40.2 ya matundu 1,345 yanayohitajika. Alisema yaliyopo kwa sasa ni 804.
 
Kuhusu mkakati wa kumaliza tatizo hilo, Shayo alisema katika mwaka wa fedha wa 2016/17, zimetenga Sh. milioni 100 kujenga matundu 400, huku wadau wengine likiwamo shirika la Sema, likitarajia kujenga matundu 58 ya vyoo bora. Alisema manispaa hiyo pia, inakabiliwa na uhaba wa walimu 220.
 
DAR YAELEMEWA MADARASA 
Katika ripoti iliyopatikana Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam, inaeleza kuwa uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza mkoani humo umevuka lengo na kufikia watoto 80,276, badala ya 68,820 ambao ni lengo lililowekwa.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watoto 12,000 sawa na asilimia 117, wameongezeka katika uandikishaji kwenye shule za msingi.
 
Kutokana na kukabiliwa na idadi kubwa ya wanafunzi, serikali ya mkoa imeamua kujenga madarasa mapya 500 na shule mpya 32 ili wanafunzi wote wasomee darasani badala ya chini ya mti, kama ambavyo baadhi wamekuwa wakisomea.
 
Shule inayoongoza kwa kuandikisha wanafunzi wengi ni Shule ya Msingi Majimatitu yenye wanafunzi 1,025 wa darasa la kwanza.
 
Kutokana na mwamko huo wa watoto kuitikia mpango wa elimu bure, imelazimu wanafunzi hao kusoma chini ya miti kutokana na kukosa madarasa na wakati huo huo wanakaa chini kwa kukosa madawati.
 
Katika takwimu hizo, manispaa ya Temeke kuna ongezeko la asilimia 126, Ilala asilimia 130 na Kinondoni asilimia 130
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majimatitu, Abdul Mgomi,  aliiambia Nipashe madarasa 10 yameanza kujengwa, lakini bado kutakuwa na upungufu wa zaidi ya madarasa 90.
 
HALMASHAURI YA JIJI LA ARUSHA
Katika Jiji la Arusha, wameandikiashwa wanafunzi 13,643 sawa na asilimia 146.15 ya lengo kujiunga na darasa la kwanza.
 
Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Hossein Mghewa, aliiambia Nipashe hivi karibuni kuwa walitarajia kuandikisha watoto 9,335, lakini idadi imeongezeka hadi 13,643, hivyo kuwapo ongezeko la wanafunzi 4,308.
 
Alisema kwa upande wa elimu ya awali walipanga kuandikisha watoto 8,637, lakini walioandikishwa ni 9,887 sawa na asilimia 122.
 
Kutokana na ongezeko hilo, alisema wana upungufu wa madawati 703 katika shule zilizo na ongezeko kubwa la wanafunzi za Olsunyai na Unga limited.
 
"Lakini upungufu huo ungekuwa mkubwa zaidi kama tusingejipanga. Tuijipanga tangu Desemba mwaka jana, kwani tulinunua madawati 3,833 ambayo yaligharimu zaidi ya Sh. milioni 210 tulizotenga," alisema.
 
Alisema kwa upande wa matundu ya vyoo hakuna tatizo, kwa kuwa jiji limejipanga kujenga vyoo katika shule zote watakazobaini kuna upungufu.
 
DODOMA NAKO  VYOO NI SHIDA
Kwa upande wa Mkoa wa Dodoma, katika kipindi hiki cha elimu bure hususan kwa shule za msingi, unakabiliwa na changamoto ya miundombinu, hususan matundu ya vyoo, madawati na vyumba vya madarasa.
 
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa (kwa sasa Mkuu wa Mkoa wa Songwe), alisema kwa shule za msingi matundu ya vyoo yanayohitajika ni 15,677, yaliyopo ni 6,579 na upungufu ni 9,098 sawa na asilimia 58. Kwa sekondari, mahitaji ni matundu 3,061 wakati yaliyopo ni 1,705 na upungufu ni 1,356 sawa na asilimia 44.
 
Kuhusu upungufu wa vyumba vya madarasa, Gallawa alisema kwa shule za msingi mahitaji ni vyumba 9,909 na vilivyopo ni 5,210 huku upungufu ukiwa 4,699 sawa na asilimia 53. Kwa sekondari mahitaji ni vyumba 2,061, vilivyopo ni 1,725 na upungufu ni 336, sawa na asilimia 16.
 
Kwa upande wa madawati, alisema kwa shule za msingi yanayohitajika ni 135,893, yaliyopo ni 63,903 na upungufu ni 71,990 sawa na asilimia 53 huku kwa sekondari mahitaji ni seti za meza na viti 58,795 na zilizopo ni seti 48,141 huku upungufu ikiwa seti 10,654 sawa na asilimia 18.
 
Kadhalika, alisema upungufu wa nyumba za walimu ni 9,831 sawa na asilimia 86 za walimu katika shule za msingi. Mahitaji ni nyumba 11,436 na zilizopo ni 1,605, huku upande wa sekondari upungufu ukiwa nyumba 2,801 sawa na asilimia 84 ya mahitaji ambayo ni nyumba 3,325 zilizopo kwa sasa ni 524.
 
Aidha, alisema bado kuna mahitaji ya maabara za sayansi katika shule za sekondari na kwamba mahitaji ni maabara 561 wakati zilizopo ni 80 na upungufu ni 481, ambao ni asilimia 86.
 
Ili kumaliza changamoto hizo, alisema mkoa ulikaa na watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali na kukubaliana kila mmoja kwenye taasisi yake kuwashirikisha watumishi kuchangia.
 
Alisema utaratibu huo utapanuliwa zaidi kwa kufanya hafla ya kuchangia maendeleo ya elimu Dodoma na pia kuchangia kupitia mitandao ya simu ili ifikapo Aprili 30, mwaka huu, tatizo la miundombinu liwe limeisha.
 
Kwa upande wake, Ofisa Elimu mkoa huo, Juma Kaponda, alisema mkoa  una wananfunzi wa shule za msingi 427,845 na sekondari ni 55,737.
 
Alisema uandikishaji kwa elimu ya awali, walitarajia kuandikisha wanafunzi 68,357, lakini mpaka Februari 15, mwaka huu, walioandikishwa walikuwa 60,640 sawa na asimia 87 ya matarajio.
 
Kwa upande wa darasa la kwanza, Kaponda alisema walitarajia kuandikisha wanafunzi 74,130 na hadi Januari, mwaka huu walioandikishwa walikuwa ni 74,509, sawa na asilimia 101 ya matarajio.
 
MTWARA NAYO YAELEMEWA
Licha ya wazazi wengi mkoani humo kuwa na mwamko wa kuwaandikisha watoto wao kujiunga na elimu ya msingi mwaka huu na kufikia asilimia 83 hadi sasa, bado kumekuwa na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na uhaba wa walimu, vyumba vya madarasa na madawati.
 
Mchakato wa uandikishaji bado unaendelea na hadi sasa jumla ya wanafunzi 29,812 wameandikishwa huku matarajio yakiwa ni kufikia asilimia 100 ya wanafunzi rika lengwa 35,944 walio na umri kati ya miaka sita hadi saba na nane hadi 13 kwa wale waliokosa fursa ya kuandikishwa miaka iliyopita.
 
Changamoto hizo zimechangiwa kwa kiasi kikubwa na mpango wa elimu bure, unaotekelezwa na serikali ya awamu ya tano, kutokana na kuweka msukumo kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto shule huku walimu wakuu wakitakiwa kutowakataa watoto hata kama mahitaji ya shule yametimia.
 
Taarifa ya Ofisa Elimu Mkoa wa Mtwara, Evarist Masuha, ilieleza kuwa mkoa ulijiridhisha kuwapo kwa changamoto hizo, baada ya kupokea taarifa kutoka katika halmashauri zake.
 
Katika kikao kilichoitishwa Februari, mwaka huu, baada ya kubaini changamoto hizo, alisema wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya waliagizwa kuhakikisha wanashughulikia changamoto hizo hasa  uhaba wa madawati.
 
Alisema, wadau walitoa mapendekezo ya namna gani watashiriki katika utatuzi wa shida hiyo, wakiwamo Jeshi la Magereza ambao waliahidi kuanza kukusanya mbao kutoka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza madawati.
 
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kwa upande wa madarasa, mkoa unakabiliwa na uhitaji wa vyumba 6,565 huku vilivyopo vikiwa ni 3,857. 
 
Kwa nyumba za walimu, zinazohitajika ni 6,726 wakati zilizopo kwa mkoa mzima ni  nyumba 1,630 hivyo kufanya upungufu kuwa nyumba 5,096.
 
Katika matundu ya vyoo, alisema mkoa unakabiliwa na upungufu wa matundu 5,882 huku yaliyopo yakiwa ni 5,253, hivyo kufanya jumla ya mahitaji kuwa matundu 11,135. Kwa upande wa madawati, alisema kuna upungufu wa madawati 35,406.
 
TANGA CHANGAMOTO MADAWATI
Mkoa wa Tanga una mahitaji ya madawati 41,992 kwa ajili ya shule za msingi kwenye wilaya zote nane za mkoa huo, huku kila halmashauri ikiwa imeagizwa yapatikane kulingana na mahitaji halisi ya eneo kabla ya mwishoni mwa Juni, mwaka huu.
 
Ofisa Elimu Mkoa wa Tanga, Mayasa Hashim, alisema  ameshatoa agizo kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha mbinu walizotumia katika kukamilisha ujenzi wa maabara zinatumika kupata madawati kwa muda waliopangiwa.
 
Hashim alisema kwa sasa mkoa huo umefikisha asilimia 76 ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na kumekuwa na mwamko mkubwa kwenye baadhi ya maeneo, hivyo shule zilizozidiwa zimelazimika kugawa muda wa kufundisha kwa siku.
 
Kuhusu upungufu wa walimu, alisema wamepokea mwongozo kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambao wameusambaza kwenye halmashauri zote ili kuainisha mahitaji ya walimu kishule na aina ya masomo wanayohitajika.
 
“Kuna changamoto nyingine ambayo tangu nimeingia Tanga kwa miezi hii miwili, nimeiona. Huwezi kumfukuza mwalimu kazi kwa sababu anaumwa, lakini kwa Tanga Jiji peke yake kuna walimu 80 wanaumwa na wanakuwa na ruhusa za mara kwa mara kwa ajili ya kuhudhuria hospitali za rufani kwa matibabu zaidi. Hali hii inarudisha ile kasi ya ukuaji wa kiwango cha elimu kwa wanafunzi,”alisema.
 
SHINYANGA YAFICHA UKWELI
Licha ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Lewis Kalinjuma, kugoma kuzungumzia suala ya elimu bure ili kupata ufafanuzi wa changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo, bado Mkoa wa Shinyanga una kero kubwa kuhusiana na hilo.
 
Ofisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, James Malima, alisema idadi ya wanafunzi wa shule ya msingi waliotarajiwa mkoani humo, imevuka malengo, hivyo kufanya idadi ya shule kutoendana na mahitaji ya wanafunzi.
 
Alisema mkoa ulitarajia kuandikisha wanafunzi 201,550 lakini hadi sasa walioandikishwa ni 206,809 sawa na asilimia 104.
 
Alisema katika mkoa huo, ambao una shule za msingi 553 huku wilaya ya Msalala ikiwa na shule 91, wanafunzi wa darasa la kwanza  walioandikishwa ni 10,722 huku lengo likiwa 10,550, Kahama shule 72, wanafunzi 18,490 lengo 12,270, Shinyanga Vijijini shule 128, walioandikishwa 12,534 lengo 12,380, manispaa shule 48 walioandikishwa ni wanafunzi 54,001 huku lengo likiwa 51,760.
 
Wilaya ya Kishapu yenye shule 114, wanafunzi walioandikishwa ni 95,770 lengo likiwa 98,380 na Ushetu ikiwa na shule 100, wanafunzi 15,292 lengo 16,210.
 
MWANZA VYOO TATIZO
Baadhi ya shule za msingi na sekondari za jijini Mwanza nazo hazitofautiani na changamoto zinazoukabili mkoa wa Shinyanga na mikoa min gine, lakini upungufu wa madarasa, uchache wa matundu ya vyoo vya wanafunzi na walimu ni tatizo kubwa
 
Meya wa jiji hilo, James Bwire, alisema changamoto hizo zinazikabili zaidi shule za serikali zilizoko katika wilaya ya Nyamagana.
Bwire alisema Jiji kwa mwaka huu, lilikuwa na lengo la kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 10,705 sawa na asilimia 81, lakini walivuka lengo na kuandikisha 17,313 sawa na asilimia 151.
 
BUNDA, MOSHI  KILIO NI MADAWATI
Wilayani Bunda mkoani Mara, shule nyingi za msingi zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati, hali inayosababisha watoto wengi kusoma wakiwa wamekaa sakafuni. 
 
Kwa sasa, wilaya hiyo inja upungufu wa madawati 24,154, kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya, Joshua Mirumbe, ambaye alitoa madawati 461 kwa shule za msingi za halmashauri ya wilaya hiyo na halmashauri ya mji kutoka Tamisemi.
 
Alisema wanafunzi walioandikishwa katika shule hizo kuanza darasa la kwanza mwaka huu ni 26,209.
 
Mkoani Kilimanjaro, wilaya ya Moshi pekee, imeandikisha wanafunzi 10,230 wa darasa la kwanza, sawa na ongezeko la wanafunzi 2,230.
 
Ofisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri hiyo, Simon Mlacha, alisema wanafunzi hao waliandikishwa katika shule za msingi zilizopo katika majimbo mawili ya Moshi Vijijini na Vunjo.
 
“Hadi sasa takwimu zetu kwenye taarifa ya elimu ya halmashauri ambayo tunaiandaa, inaonyesha wanafunzi walioandikishwa ni 10,230. Kwa maana hiyo, kuna uandikishaji wa kupitiliza kwa wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka 2016,” alisema.
 
Kuhusu upungufu wa madawati kwa shule za msingi, taarifa ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Severine Kahitwa, inaeleza kwamba shule hizo zinakabiliwa na upungufu wa madawati 21,000.
 
Imeandaliwa na Moshi Lusonzo, Dar; Nebart Msokwa, Mbeya; Elisante John, Singida; Cynthia Mwilolezi, Arusha; Augusta Njoji, Dodoma; Juma Mohamed, Mtwara; Lulu George,Tanga; John Maduhu, Shinyanga; Winfrida Joseph, Mwanza; Ahmed Makongo, Bunda na Godfrey Mushi, Moshi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment