dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, March 18, 2016

Rais wangu Magufuli, mafanikio ya Vietnam ni ‘udhalilishaji’ kwetu


Rais wa Vietnam, Truong Tan Sang na mkewe Mai Thi Hanh wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  huku wakiwapungia mkono wananchi walipokuwa wakiwaaga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kumaliza ziara ya siku tatu nchini, jijini Dar es Salaam. Picha na PMO 
Rais wangu John Magufuli wiki opita ulipokea ugeni wako wa kwanza mzito wa kimataifa kutoka Taifa la Vietnam.
Ni ujio wa Rais wa nchi hiyo, Troung Tan Sang, akiambatana na ujumbe wa watu 51 wakiwamo mawaziri na wafanyabiashara.
Rais wangu Magufuli natumaini ulipomuona mgeni wako huyo kaja na msururu mkubwa wa watu huenda ulimuuliza, “mbona mwenzangu unatumia  fedha nyingi za nchi yako?”
Waswahili wanasema “ukitaka uzuri sharti udhurike”, wenzetu hao hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya wanajua faida watakayoipata kwa ujio wao huo wa watu wengi.
Rais wangu mara baada ya kuongea na mgeni wako huyo katika mazungumzo yenu ya faragha  ndani ya Ikulu yako, ulijitokeza mbele ya vyombo vya habari kuuambia umma nini mmeongea huko.
Kwa upande wangu jambo kubwa lililonifurahisha na kuendelea kuamini huenda ni kweli  sasa umedhamiria taifa letu lisonge mbele kimaendeleo ni jinsi ulivyo badili utaratibu wa baadhi ya viongozi waliokutangulia.
Utaratibu wa kuacha kujigamba na kujipa sifa tele mbele ya umma kama tulivyozoea kwa baadhi ya viongozi waliopita, utawasikia: “Ujio wa wenzetu hawa umetupa faida kubwa, wenzetu wameahidi kutukopa dola billioni kadhaa, hivyo Watanzania tusibeze ujio huu” na mbwembwe kibao.
Kwa upande wako, umetoka hadharani na sura ya masikitiko kama mtu anayeona aibu na haukutaka sifa za ‘kuidhalilisha’ nchi.
‘Haukuidhalilisha’ nchi kwa kutwaambia ‘wenzetu wameahidi kutukopesha na kuleta wawekezaji, bali  ukaenda mbali ukatuambia nasi tuyatafakari mafanikio yao kisha tujifunze kwao.
Ukasema iweje wao wafanikiwe kwa kiasi kikubwa kutupita sisi wenye rasilimali nyingi ikiwa wao wamepitia changamoto nyingi huko nyuma kuliko sisi.
Ukashangaa  tena iweje wenzetu hao walichukua samaki na korosho zetu miaka ya 1970 na kupeleka kwao kuzalisha na leo hii wao ni miongoni mwa wauzaji wakubwa duniani wa zao hilo wakizalisha tani laki tatu kwa mwaka.
Hakika inatia aibu. Sasa hivi hapa kwetu zao la korosho halipewi kipaumbele, wakulima huko Mtwara wamebaki wakizalisha zao hilo pasipo kuwa na faida kubwa kama inavyotakiwa.
Siyo kwamba zao hilo halikuwa na tija katika Taifa letu, la hasha, kwani kwa mujibu wa takwimu za msimu wa mwaka 1999/2000 na zilizalishwa tani 121,207 zinaonyesha kuwa zao hilo liliingizia Taifa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni kuliko zao lingine lolote lile katika msimu huo.
Inaonyesha kuwa Tanzania ilijipatia dola 90.2 milioni za Marekani kwa kuuza zao hilo katika nchi ya India huku wakulima wakijipatia  Sh70.5 bilioni.
Wapi tulishindwa?
Mpaka leo hii wenzetu hao wametuzidi katika mauzo  na hali hii ni kutokana na Serikali kuacha kusimamia ipasavyo zao la korosho na soko lake, ikaliachia soko huria lishike hatamu.
Tukasahau kuwa kwa kufanya hivyo tulikuwa tunaliacha zao hilo mikononi mwa watu wasio waaminifu, zao na soko lake likaporomoka, hatimaye tukawakaribishia Watanzania wenzetu ukosefu wa ajira na umaskini.
Vietnam miongoni mwa vinara wa uzalishaji wa korosho walizozichukua hapa nchini ni aibu kubwa na udhalilishaji.
Natumaini wenzetu hao wanatuona sisi ni watu wa ajabu kama vile viumbe viitwavyo ‘Aliens’ au UFOs (an Unidentified Flying Objects) vinavyosadikiwa kuishi katika sayari ya Mars kwamba ipo siku vitakuja kuitawala dunia.(rejea kitabu cha Sydney Sheldon, The Doomsday Conspiracy).
Rais wangu Magufuli hukugusia suala la korosho tu, ila ulishangaa iweje nchi iliyodumu katika vita kwa muda wa miaka 31 itupite kimaendeleo tuliokuwa huru kipindi chote hicho.
Historia ya vita
Ni kweli kabisa Rais wangu hebu tuitazame vita yao kwa ufupi, halafu tujiulize kama sisi siyo watu wa ajabu ambao huenda hata Mwenyezi Mungu huko mbinguni akatuadhibu vilivyo kwa kushindwa kutumia vizuri neema zake nyingi kwa ajili ya wengi.
Nchi ya Vietnam iliingia vitani na Ufaransa mwaka 1945 mara baada ya Wafaransa kutotaka kutambua uhuru wa nchi hiyo na hivyo kuamua kuanzisha vita ili kuzidi kuikandamiza.
Hata hivyo, mara baada ya miaka tisa mwaka 1954, Wavietnam walifanikiwa kuitandika Ufaransa na kuwafurusha nchini humo.
Baada ya Wafaransa kuangushwa na nchi hiyo changa, kiongozi mkuu wa mabepari na mabeberu Marekani wakaanza kukodolea macho rasilimali za nchi hiyo za mafuta, mpira na nyinginezo.
Hivyo, mwaka 1954 ambao Vietnam waliishinda Ufaransa nao Wamarekani wakaingia vitani dhidi ya nchi hiyo kwa kuunda viongozi vibaraka katika Vietnam ya Kusini ili kuigawa nchi hiyo.
Katika vita hiyo iliyodumu kwa muda wa miaka 21 Taifa hilo lilifanikiwa kuwashinda mabeberu wa Marekani.
Vita zote mbili ziliiathiri nchi hiyo, kwani iliharibu miundominu na rasilimali zake nyingi ikiwamo kusababisha vifo.
Kuharibiwa kwa rasilimali za nchi hiyo hakukuja kwa bahati mbaya, ila ulikuwa mpango maalumu wa kuhakikisha nchi hiyo ya kisosholisti inaharibiwa kwa kila hali.
Mpango huo unasimuliwa na mwanajeshi mmoja wa Ufaransa aliyekamatwa  wakati wa vita nchini humo mwaka 1951,
Mwanajeshi  huyo anasema: “Tulipewa amri na uongozi wa juu wa kijeshi wa nchi yetu tuharibu kila kitu ili kuibadili nchi hii kuwa jangwa.
“Amri hiyo ilitekelezwa ipasavyo. Nyumba zilichomwa moto. Wanyama na ndege waliuawa. Bustani, mimea na miti iliharibiwa. Mashamba ya mchele na mazao yalichomwa moto.”
Baada ya kumaliza vita vyao hivyo, nchi hiyo ilitengwa na nchi za Magharibi kutokana na misimamo yake katika utawala wa Khmer  Rouge huko Kampuchea
Pamoja na misukosuko yote hiyo mikubwa  ya Taifa lao kuharibiwa rasilimali zake, Wavietnam ndani ya  miaka 41 baada ya kumalizika kwa vita mwaka 1975 wameweza kupiga hatua kubwa za maendeleo.
Kwa mfano tukiangalia takwimu zao za miaka ya mwanzoni zinaonyesha kuwa mwaka 1987 Taifa hilo lilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni 17.5 za chakula na mpaka mwaka 2004 waliweza kuzalisha tani milioni 39.
Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu ya mwaka 2014 ikinukuu ripoti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaonyesha kuwa kati ya hekta milioni 14 za ardhi inayofaa kwa kilimo ni asilimia 23 ndiyo iliyotumika.
Ikumbukwe kuwa nchi hiyo ilikuwa ikiingiza mazao hayo kutoka nje ya nchi, kwa mfano walikuwa wakiingiza tani  takriban milioni moja za mchele kwa mwaka. 
Ukizungumzia kiwango cha upunguzaji wa umaskini, ndani ya miaka 7 tu tangu  kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 1993 Taifa hilo lilikuwa limefanikiwa kupunguza kiwango cha umaskini  kwa asilimia 17 kutoka asilimia 70 ya mwaka 1986 mpaka asilimia 58ya mwaka huo wa 1993. (Rejea ripoti ya Poverty Working group mwaka 1999).
Pia, wenzetu hao hawahangaiki na suala la elimu ya awali na kati, kama sisi. Kwa sasa wao wanapigana zaidi kuhakikisha kila Mvietnam anapata elimu ya chuo kikuu.
Mwandishi wa makala haya ni mwaandishi wa habari wa kujitegemea, simu 0658010594 na baruapepe: ahmadi.yusufu6@gmail.com au maoni@mwananchi.co.tz

No comments :

Post a Comment