Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, August 14, 2016

Aboud Jumbe: shujaa wa demokrasia tangu asubuhi!

Rais wa Zanzibar (awamu ya pili), Alhaj Aboud Jumbe aliyefungua milango ya demokrasia ambayo sasa imegeuka kuwa sumu kwa Wazanzibari.

SOMA PIA:
http://zanzibarnikwetu.blogspot.ca/2012/10/ilikuwaje-chama-kikampindua-rais-aboud.html#more
Jumapili, Agosti 14, 2016
MWENYEKITI wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar (awamu ll) na ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia. Imethibitishwa kuwa maziko yatakuwa kesho Unguja.
Marehumu Aboud Jumbe alizaliwa tarehe 14 June 1920 (96). Inadaiwa kuwa alizaliwa Mkamasini, mjini Unguja. Alishika u-Rais wa Zanzibar, Aprili 11, 1972 kufuatia kuuawa kwa Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha, Aboud Jumbe aliendelea kushika nyadhifa nyingine za juu kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Afro Shirazi (ASP) na baadaye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), hadi tarehe 30 Januari 1984 alipofukuzwa na Nyerere, kufuatia kile kilichodaiwa kutaka kuvunja Muungano wa Tanzania.

Aboud Jumbe, baada ya kukamata madaraka ya Urais wa Zanzibar, kitu cha kwanza alifanikiwa kuuondosha na kuuzika kabisa utawala wa KIDIKTETA, au niseme utawala wa mabavu na uonevu dhidi ya binadamu wa Abeid Aman Karume.

Aboud Jumbe, haraka haraka mara baada ya kushika madaraka alilifunga ‘Gereza la Mateso ya Binadamu’ maarufu kwa BAMKWE’.

Watu waliyokamatwa kwa tuhuma za kifo cha Karume, Aboud Jumbe alisema: “aliyekuwemo hotoki na asiyekuwamo haingii”.

Kauli hii ya Aboud Jumbe, ilimaanisha kuwa watu wote waliyoshtakiwa kwa madai ya kumuuwa Karume, watatendewa haki na hapana atayedhulumiwa.

Mwenendo mzima wa kesi ya uhani uliweza kuonekana kupitia Televisheni ya Zanzibar (TVZ), watu waliweza kuona kila kilichotendeka mahakamani. Naweza nikasema kuwa ile ilikuwa ni hatua kubwa na ya awali ya demokrasia na haki za binadamu.

Hatua ya pili, aliweza kufanikiwa kulidhibiti na kuling’oa meno Baraza la Mapinduzi (BLM), na kuweza kuingiza damu changa, yaani kuingiza vijana ndani ya BLM na ndani ya serikali.

Pamoja na hatua hiyo, Aboud Jumbe aliendelea kuwabakisha waasisi wa Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Lakini, pamoja na kuendelea kuwemo ndani ya BLM, waasisi wale hawakuwa tena na meno. Nakusudia sauti, nguvu na uwezo.

Aboud Jumbe, kadri siku zilivyosonga mbele ndivyo alivyozidi kuwatenga baadhi ya Waasisi wa Mapinduzi, alionyesha wazi wazi kuwa na hofu nao. Alionekana kutokuafikiana sana katika sera za kiutawala na kundi la akina Seif Bakari.

Watu wake wa karibu na ambao aliwaamini katika shughuli za serikali na chama (ASP), ni Thabit Kombo, Ramadhan Haji Fakih, Said Idd Bavua, Hassan Nassor Moyo na wengine wachache.

Tukiwaacha hao wengine kwa wakati ule wa mapema na walionekana bado ni vijana ni pamoja na Ali Mzee, aliyewahi kuwa Waziri wa nchi katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mohamed Fakih na Aboud Talib.

Katika miaka ya 1980 hadi alipojiuzulu Aboud Jumbe, alipendelea kutumia muda wake mwingi Pemba kuliko Unguja, Makao Makuu ya Serikali. Baadhi ya watu walitafsiri kuwa alikuwa anazikimbia kero za akina Seif Bakari.

Halafu muhimu zaidi, Aboud Jumbe katika mafanikio yake alijaribu kuwaondoshea watu adha ya kupata chakula muhimu, ambacho katika serikali ya Karume, kilitolewa kwa mgao, wiki mara moja.

Katika utawala wa Karume, watu walikuwa wakiuziwa bidha za unga, mchele na sukari kwa kutumia kadi maalumu. Aboud Jumbe, aliondoa utaratibu huo. Ingawa ilichukuwa muda kufanya hivyo.

Aliachana na sera ya Kurume, kujenga majumba kama matreni, yeye alikuja na mpango wake wa ujenzi wa nyumba ndogo ndogo alizipa jina ‘nyumba za vijiji’.

Alikuwa na tabia ya kuiga mambo kutoka sehemu nyingine nje ya Zanzibar. Aliona ujenzi wa nyumba aina hizo alipokuwa katika ziara za mikoa ya Tanzania Bara. Ndipo alipoachana na ujenzi wa nyumba za matreni.

Alipofanya ziara nchini Guinea, aliona utamaduni wa ngoma za BALE, utamaduni wa nchi za Afrika Magharibi, ulimvutia na kuuleta Zanzibar.

Aliwapeleka Guinea, baadhi ya wasanii wa Zanzibar na baadaye akawaleta Zanzibar wa-Guinea kuendelea kutoa mafunzo ya ngoma za BALE kwa wasichana na wavulana wa ki-Zanzibari.

Sherehe za Mapinduzi na zile za elimu bure za kila mwaka ziliweza kuigharimu serikali fedha nyingi kutokana na gharama za kuwasafirisha hasa wanafunzi na walimu kutoka sehemu moja ya visiwa (Unguja au Pemba) na kuwapeleka nyingine.

Sherehe hizo kama zikifanyika Unguja, takriban maeneo mengi ya mji, majumbani watu walikuwa hawapiki, walikuwa wanamiminika uwanja wa Maisara, kupata pilau na chai ya usiku. Kwa Pemba, ilikuwa Machomanne na Madungu. Kwa muda wote wa sherehe hizo.

Miaka ya mwanzo ya 1980, alinza kubadilika na kuonekana mtu mwenye wahka na wasiwasi. Huku, akionekana kuchanganyikiwa hafahamiki anachokifanya. Serikali ilinza kudamirika kifedha. Hata hivyo, pamoja na hali hiyo, suala la ubaguzi kwake lilikuwa mwiko.

Mwishoni mwa miaka ya 1970, alitanua wigo mpana wa demokrasia akaanzisha Katiba ya Zanzibar, akaanzisha Baraza la Wawakilishi na akaanzisha cheo cha Waziri Kiongozi kama mkuu washughuli za kila siku za serikali na ndani ya Baraza la Wawakilishi.

Ndiyo sababu hasa, hadi leo Zanzibar, ina chombo chake cha kutunga sheria na kuwakilisha serikalini mawazo ya wananchi kupitia wawakilishi wao.

Baraza la Wawakilishi (BLW), muasisi wake ni Aboud Jumbe. Na katika kazi hii ya kuanzisha Baraza la Wawakilishi, alipata masaada mkubwa wa ushauri wa kisheria kutoka kwa mwanasheria nguli kutoka nchini Ghana, Bashir Swanzy.

Hapa panahitaji ufafanuzi mdogo: Hatua ya mwanzo iliyoanza kutikisa Mungano, ilikuwa ni pale Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wa siku hizo, Jaji Damian Lubuva aliporejeshwa Tanzania Bara kwa hofu ya kuvujisha siri.

Kupitia hatua hiyo, Aboud Jumbe ndipo alipomteua Bashir Swanzy kuwa Mwanasheria Mkuu, akiamini ataendana na azma ya matwaka yake bila siri zake kuvuja na kumfikia Nyerere.

Nakumbuka ilijitokeza Radio ikitangaza kutokea msituni, iliyopewa umaarufu ‘redio kiroboto’ ambayo matangazo yake yalikuwa yakitokea mafichoni au niseme ‘redio pori’. Watu walionyesha hisia zao dhidi ya Muungano, bila kukemewa.

Mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar na Waziri wa Biashara na Viwanda, Jamal Ramadhan Nassibu ndiye aliyeshika tutu katika kukamia ubaya wa Muungano. Watu wengine waliyokuwa wapigaji upatu wakubwa kupinga Muungano ni Wolfgang Dourado (former AG).

Kwa kupitia Bashir Swanzy, Serikali ya Zanzibar, chini ya Aboud Jumbe iliandaa hati ya mashtaka kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalumu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo, kuna hadithi hadi leo kwamba, kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), uliyofanyika Dodoma kwa takriban wiki mbili kujadili kile kilichoitwa ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Brigadier Ramadhani Haji, alibishana sana na Nyerere kuwa 1+1=3 wala siyo mbili. Kusikia kauli hiyo Nyerere, alipanaki.

Hii inatafsirika kwamba Aboud Jumbe na wenzake waliyomuunga mkono akiwamo Brig. Ramadhani Haji, walikuwa wanatetea mfumo wa Muungano wa serikali tatu na siyo mbili kama ulivyo sasa.

Kuhusu sheria za nchi hasa masuala ya haki za binadamu: Aboud Jumbe, kwa kiasi fulani naweza kusema alizirejesha mahakama katika utaratibu wa sheria na haki. Kidogo mahakama zilipata heshima, kuliko hata ilivyo sasa.

Hakukuwa na mtindo wa kubambikiana kesi kwa misingi ya kukomoana kisiasa na uonevu mwingine. Polisi na taasisi za sheria zilikuwepo kusimamia haki za raia na utawala bora.

Lakini, jambo kubwa na la kupigiwa mfano hadi leo, Aboud Jumbe alizikana siasa za ubaguzi. Hakuupenda ubaguzi si katika majukwaa wala katika mikutano yake ya ndani. Sikuwahi kumsikia kuzungumzia vitisho wala kauli za ubaguzi wa watu au ubagzu wa aina yoyote.

Nathubutu kusema kwamba, Aboud Jumbe alionesha mapenzi zaidi kwa wa-Pemba, aliwapa wa-Pemba madaraka na nyadhifa za juu kabisa, kitu ambacho ma-Rais wa Zanzibar wengine waliyofuta kimewashinda.

Hasa, kuanzia awamu ya 4, 5, 6 na hii (natilia mkazo) na hasa hii iliyopo sasa ya Dk Ali Mohamed Shein na Balozi Seif Ali Iddi. Serikali hii ilipo madarakani nashindwa kuilinganisha kwa aina zote za ubaya dhidi ya wananchi, hii imekubuhu.

Awamu hii imefurutu a’da, imepindukia mipaka ya ubaguzi, uonevyo, choyo, husda, utesaji na kuwafanya wa-Pemba na CUF kuwa Unguja hawana haki ya kuishi.

Aboud Jumbe, alikuwa binadamu na kila binadamu anayo mema na ana mabaya yake. Kwa ufupi ni kwamba alikuwa na mapungufu yake.

Mfano, kwanza alionekana kumuamini Nyerere sana, hakuweza kumfahamu mapemba kuwa ni sehemu ya mtu muovu na mbaya wa Zanzibar na wananchi wake. Hakufanikiwa kupata werevu wa Karume katika hadaa za Nyerere.

Kosa lake kubwa alilolifanya Aboud Jumbe, dhidi ya Wazanzibari ni kukiua chama cha Afro Shirazi (ASP) kwa hadaa za Nyerere kuwa aking’atuka katika madaraka ya u-Rais atakuwa Rais wa Muungano.

Baadhi ya wenzake hasa Seif Bakari, Hafidhi Suleiman (SANCHO) na Ramadhan Haji Fakih walimtahadharisha mno kuhusu kuunganisha ASP na TANU. Nakumbuka ule msemo: ‘shikio la kufa halina dawa’.

Aboud Jumbe ni msomi aliyeweka records nzuri Makerere, lakini si kila msomi ana uwezo wa kuona kila kitu au niseme kupambanua mambo.

Wasomi wengi wanahitaji ushauri na usaidizi katika maamuzi yao. Dr King’waba Hassan (rafiki yake Aboud Jumbe), siku moja alinihadithia anasema Aboud Jumbe alikuwa ‘genius’ (mwenye akili hasa) Makerere.

Nadhani akina Seif Bakari, waliiona hasara iliyoelekezwa kwao siku za mbele watakayokabiliana nayo. Na walimsuta na kumsimanga siku Nyerere, alipowafukuza au bora niseme alipowavua nguo Dodoma.

Nafafanua kidogo hapa: Baada ya kufukuzwa au bora niseme kama ilivyotangazwa katika taarifa ya habari ya saa 12 jioni ya STZ/RTD, siku zile. Kwamba, baada ya kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi Aboud Jumbe, alitaka kwenda Pemba.

Bila ya kujuwa kuwa wasaidizi wake walikuwa tayari wameshapewa maelekezo kutoka ngazi za juu (kwa NYRERE) kuwa wampelekea Dar es Salaam, tena Dar es Salaam Mji-Mwema, Kigamboni.

Akiwa angani baina ya Dodoma na Dar es Salaam, ndani ya ndege (sio Jet ya Rais wa Zanzibar), alimuamuru rubani kuwa ampeleke Pemba:

“Sawa mzee lakini tumeelekezwa kuwa tukupeleke Dar es Salaam kwanza…basi wacha twende Dar es Salaam baadaye tuone tusikilize huko,” kauli wa rubani.

Kuanzia hapo Aboud Jumbe, ameishi Mji-Mwema, Kigamboni na amemalizia umri wake wote huko wa miaka 96. Ingawa baadhi ya watu wanasema alikuwa ‘house arrest’ (kifungo cha nyumbani).

Aboud Jumbe, kuanzia Januari 30, 1984 mpaka anakwenda kaburini kwa safari ya haki, hakusikika tena kuzungumzia siasa, hakuwahi kushiriki matukio ya siasa ya Tanzania, wala hakuwahi kufanya malumbano na mwanasiasa yoyote si wa Tanzania wala nje.

Aboud Jumbe, muda wote wa maisha yake tangu kuwa nje ya ulingo wa siasa za Tanzania, alijikita zaidi katika uislamu na kumtafuta ‘Allah Jalla Jalal’.

Ametunga vitabu vingi, kitabu chake ambacho kimetia fora katika kuusasambua Muungano ni ‘The Partnership’: Kinachozungumzia kwa undani Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Sidhani kwamba, katika uhai wake kutoka siku aliyoondoka Dodoma, baada ya kujiuzulu nyadhifa zake zote hadi mauti yalipomkuta aliwahi tena kukutana na Nyerere.

Nilikutana na Aboud Jumbe, Golders Green, London mwishoni mwa miaka ya 1990 nyumbani kwa rafiki yake, Bashir Swanzy.’Inna lillah wa Inna Ilayhi Raajiun’ Kila roho itaonja mauti.



No comments :

Post a Comment