Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, August 15, 2016

RAIS MAGUFULI KUTANGAZA URAIA PACHA AKIFUNGA KONGAMANO LA SIKU MBILI LA DIASPORA HAPA ZANZIBAR!

  • Siku 10 kabla ya kufunga kongamano la Diaspora, siri nzito ya Rais Magufuli yafichuka hadharani hapa Zanzibar!
Juu ni Rais Magufuli, je, ni kweli atalitangazia Taifa kukubalika kwa uraia pacha Tanzania?

Na Muandishi wetu, Mazizini, Zanzibar.

Habari zisizokuwa za kuaminika na ambazo bado ni tetesi tu mpaka hivi sasa zimejaa na kuzagaa katika hiki kitongoji kidogo cha kisiwa cha Unguja kiliopo katika ufukwe wa Kusini-Magharibi ya Zanzibar kiitwacho Mazizini, ambako Zanzibar Beach Resort Hotel ipo na ambako kutafanyika kongamano la Diaspora la mwaka huu wa 2016.

Habari hizo au tetesi hizo zinazungumzia kuwa Rais Magufuli atakapofunga kongamano hilo tarehe 25 Augosti ambalo litakuwepo kwenye kitongoji hicho kwa muda wa siku mbili huenda akalitangazia Taifa kuwa Tanzania sasa nayo ni nchi yenye kukubali uraia pacha.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hutayarisha makongamano haya ambayo hutoa fursa ya kujadili masuala ya kimaendeleo ya nchi yetu kwa nia ya kuukuza uchumi wetu na kuboresha maisha ya wananchi wetu kupitia Watanzania wa nyumbani na wale waliopo kwenye Diaspora tofauti kule nje.

Kongamano hili litakuwa la mwanzo kufanyika nje ya Dar Es Salaam na la mwanzo kufanyika Zanzibar pia. Makongamano mawili kama haya yalifanyika huko nyuma katika mji wa Dar Es Salaam.


"Hakuna atakaestaajabu kama Rais Magufuli atalitangazia Taifa kuwa sasa na sisi tumeukubali uraia pacha. Wewe mwenyewe iangalie kauli mbiu ya hili kongamano na utajua kuwa tunaelekea huko huko", alielezea mkaazi mmoja wa Mazizini ambae hakutaka jina lake litajwe. 

Kauli mbiu ya kongamano hili ni 'MTU KWAO NDIO NGAO’ inafuatana na ujumbe mzito wa mwaka huu ambao ni “Mtizamo mpya wa Kuimarisha Utalii wa Tanzania na uekezaji”.
Kongamano hili litafanyika Zanzibar kwa muda wa siku mbili kati ya tarehe 24 na 25 Augosti na linatarajiwa kufunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, AlHajj Dr Ali Mohammed Shein na kufungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mazizini, mjini Unguja.

"Hizi sio habari za kusadikika, sio habari zilizozuka hapa Mazizini tu. Ni habari zenye ukweli kabisa. Rais Magufuli ni mtu wa maamuzi magumu na hatutashangaa kama akilitangazia hivyo Taifa letu siku hio", aliendelea mkaazi mwengine wa Mazizini.


"Hebu wewe mwenyewe pima kwenye akili yako, majirani zetu wote kama vile Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, etc wote hawa wamekubali kuwa na uraia pacha. Hivyo sisi Watanzania ndio peke yetu wenye akili nyingi zaidi yao kuupinga uraia pacha? Hata Msumbiji, Eritrea, Angola, Djibouti n.k wanatushinda"?, aliuliza mkaazi huyo.


"Benin jamani nao wanaona mbali kuliko sisi Watanzania?", sauti kali ilisikika ikiuliza kutoka nyuma ya Daladala tulilopanda wakati tunapita karibu na ile shule ya Kiembe Samaki kuelekea mjini Unguja.

Jumla ya kama nchi 23 katika Bara la Afrika zimekubali uraia pacha na nchi kama Zimbabwe na Zambia tayari misuada hivi sasa ishapelekwa kwenye bunge zao kwaajili ya kupitishwa. Kama desturi yetu sisi Watanzania tutakuwa wa mwisho na kama uraia pacha utakuja kukubalika nchini kwetu basi hio labda itakuwa katika karne ya 22 au 23.

"Ndani ya roho yangu siamini kama kweli Rais Magufuli atakuwa na ujasiri huo wa kutenda lile aliloshindwa JK kwa miaka 10. Lakini, tayari tushaona Rais Magufuli ametenda mengi yaliomshinda JK na kama akilitenda na hili basi sio tutamvulia kofia tu bali itakuwa keshatubwaga chini sisi wapinzani 'uchwara', kwasababu sasa atakuwa anapendwa ndani na nje ya nchi kwa umahiri wake na kuona kwake mbali. Lililobakia ni kuwa tuweke masikio yetu wazi, kwani wahenga walisema, 'lisemwalo lipo'", alimalizia raia mmoja!

Wachunguzi wa ndani wa siasa za Tanzania kutoka Dar Es Salaam wanaelezea kuwa Rais Magufuli juu ya pupa na kasi yake yakutaka kuleta mabadiliko ya kweli Tanzania kwa muda mfupi, lakini hawezi kabisa kutangaza kukubalika kwa uraia pacha nchini, kwasababu kafungwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - hii ya sasa na hio iliyopendekezwa. "This is a constitutional matter and cannot be decided by Magufuli alone. Dual citizenship has already been rejected by the proposed constitution which is soon going to be adopted by our country and Magufuli can do nothing about it.The better way is to have a referendum on the issue", gwiji moja la DSM lilitamka hivyo kwa kimombo kama vile kiswahili hakijui.

"Bwana wewe usisikie, Rais akitaka lolote lile litakuwa hata sasa hivi. Huyo JK hakushindwa bali hakutaka tu, mangapi ya Katiba mbona yanavunjwa litakuwa hili?", aliongezea gwiji jengine la sheria kutoka mji wa Arusha.

Kwa hakika hapana pahala pengine panapostahiki kutolewa taarifa ya kukubalika kwa uraia pacha nchini kuliko Zanzibar - nchi ambayo inayo watu wengi nje kuliko Tanzania Bara - %wise.

Kama alivyosema yule mkaazi wa Mazizini, tusianze kubishana bali tuweke masikio yetu wazi na tungojee hio tarehe 25 Augosti ifike, ili tujue mbichi au mbivu!

2 comments :

  1. Wazanzibari mmelogwa na hao wamanga wenu. Bado mnataka waludi tu ili mpate kutawaliwa!

    ReplyDelete
  2. Lazima tuwe na upeo wa kuona mbali mafanikio ya nchi nyengine a mbao wana uraia pacha wsmefikia hatua kubwa za uchumi ma maendeleo hii sio karne ya kusitisha mafanikio ya uchumi KW watanzania wote. Na amini Mhe Rais atlitatua hili na kwa hekima zake sifikiri kabisa atakuwa na kipingamizi kuzuia maendeleo ya watanzania KW kuwapa fursa ya uraia pacha ili Tanzania inudaike kimarndeleo. T utafika mwanzo mgumu

    ReplyDelete