WAFUASI wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, wametangaza kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuwasilisha malalamiko yao ya kupinga utaratibu uliofanywa na wajumbe wa Mkutano Mkuu cha chama hicho.
Wakati wanachama hao wanaomuunga mkono Prof. Lipumba wakidai hayo, CUF imetoa msimamo wake na kusema kuwa imeshamalizana na kiongozi huyo na kilichobaki sasa ni kujiandaa kujaza nafasi za uongozi zilizo wazi.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani, ilieleza kuwa wajumbe wengi wa Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika juzi walipiga kura ya kuridhia kujiuzulu kwa Prof. Lipumba na kwamba mchakato wa kujaza nafasi hizo utafanyika.
“Ni muhimu kukumbuka kwamba ajenda ya kwanza ya msingi katika Mkutano Mkuu imekamilika kwa wajumbe wengi kukubali kujiuzulu kwa mheshimiwa Prof. Lipumba.“Mchakato wa kukamilisha zoezi la kujaza nafasi wazi za uongozi wa chama taifa upo palepale na baada ya kukamilisha taratibu za ndani ya chama, tutatoa taarifa kwa Watanzania wote.
“Chama kinapenda kuwataarifu na kuwahakikishia wanachama, wapenzi wa chama chetu na marafiki zetu wote kuwa hii ni taasisi kubwa ya kisiasa nchini iliyo na viongozi makini na mahiri,” alisema Bimani.
Mkurugenzi huyo wa uenezi, alisema kuwa mchakato wa kumwondoa rasmi Prof. Lipumba katika nafasi yake ulifanyika kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
Alisema kura zilipigwa baada ya kutimia kwa akidi ya wajumbe halali waliopaswa kuhudhuria mkutano huo, na kwamba kwa mujibu wa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 ibara ya 79(3) toleo la mwaka 2014, walipaswa kumchagua mwenyekiti atakayesimamia zoezi hilo.
“Baada ya kuona akidi imetimia, wajumbe walimchagua Julius Mtatiro kusimamia suala la upigaji wa kura, ambapo waliotaka Prof. Lipumba aondoke walikuwa 476 na waliopinga walikuwa wajumbe 14, huku wengine wakikataa kupiga kura,” alisema Bimani.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, Prof. Lipumba si mwenyekiti tena wa chama hicho, na kwamba wanachama wanapaswa kuwa watulivu katika kipindi hiki, na kuzipuuza taarifa zote zenye lengo la kupotosha usahihi wa suala hilo.
WATETEZI WA LIPUMBA
Kutokana na uamuzi huo, wafuasi wanaomuunga mkono Prof. Lipumba, wamepinga uamuzi huo na kutangaza kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kueleza kilichotokea ikiwamo kuvunjwa kwa utaratibu.
Akizungumza na MTANZANIA nje ya Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Serengeti, Joseph Magoiga, alisema kura zilizopigwa si halali kwa sababu hazikuwa za siri kwa mujibu wa Katiba ya CUF.
Alisema kitendo hicho ndicho kilichosababisha vurugu, huku wajumbe wengine wakisusia utaratibu huo na kutoka nje ya ukumbi wa mkutano.
“Mtatiro aliwaambia wajumbe wanaomtaka Profesa Lipumba kunyoosha vidole juu ili aweze kuwahesabu, lakini sisi tulisimama wote na kusema hatutaki kwa sababu katiba ya chama inataka kupiga kura za siri na si ya kunyoosha vidole juu,” alisema Magoiga na kuongeza:
“Pamoja na wajumbe kugoma kupiga kura, lakini Maalim Seif (Sharif Hamad, Katibu Mkuu CUF) alimwambia Mtatiro aendelee kuhesabu wajumbe walionyoosha mkono na akatangaza matokeo katika hali ya vurugu. Kutokana na hali hiyo jana (juzi) tuliorodhesha majina zaidi ya 300 ya wajumbe wa Tanzania bara, tutakwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ili tuweze kumweleza kilichotokea ndani ya mkutano huo.
“Suala hili tutalifanya pamoja na kumwandikia barua ya kupinga uamuzi uliotolewa na Maalim Seif pamoja na watu wake,” alisema Magoiga.
MTATIRO AELEZA
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa Mkutano Mkuu huo, Mtatiro, jana alitoa taarifa huku akieleza mambo 15 yaliyotokea.
Alisema akidi ilitimia kwa pande zote – bara na Zanzibar, na alichaguliwa kwa kura zaidi ya 500 kuwa mwenyekiti wa muda. Aliyemfuatia alikuwa ni Ridhiwani wa Morogoro aliyepata kura 170.
“Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF wapatao 10 kutoka Tanzania Bara walitoa hoja zao kwa kutaka kikao kimwite Prof. Lipumba ili aje ajieleze kuhusu kujiuzulu kwake jambo ambalo lilipingwa na wajumbe wengine,” alisema.
Alisema alipowataka wajumbe wanaotaka Lipumba aletwe kueleza kifungu cha katiba au kanuni kinachotaka hivyo walishindwa kueleza.
Kwa upande wa wajumbe waliokataa Prof. Lipumba kufika mkutanoni, alisema walinukuu ibara ya 117(2) ambayo inataka taarifa ya kujiuzulu kwake ndiyo ipelekwe kwenye mkutano mkuu na si yeye mwenyewe.
Alisema aliujulisha mkutano kuwa Prof. Lipumba si mjumbe wa kikao, kwa hiyo hawezi kuitwa na kwamba mkutano ujadili barua zake na ufanye uamuzi wa kumrudisha au kutomrudisha.
“Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu kutoka Tanzania Bara walikataa mkutano usifanye maamuzi yoyote, huku wengine wakitaka maamuzi yafanyike.
“Kwa hiyo Tanzania Bara iligawanyika nusu kwa nusu kwenye jambo hilo. Hofu ya wajumbe wa Bara waliokataa maamuzi yasifanywe ilikuwa ni kuwa yakifanyika yataathiri mipango yao,” alisema Mtatiro.
Alisema wakati wakijadiliana suala hilo, Prof. Lipumba alijitokeza akiwa na kundi la mabaunsa wapatao 30 wakisindikizwa na ofisa wa polisi aliyekuwa na ‘radio call’.
Chanzo Mtanzania.
No comments :
Post a Comment