dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, November 6, 2016

Taarifa kwa Vyombo vya Habari – CUF!

Image result for cuf zanzibar flag

Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya. Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia nchi yetu kuendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu licha ya matatizo mengi yanayowakabili wananchi wan chi yetu.

Pili, nitumie fursa hii kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa mashirikiano yenu adhimu munayotupatia. Kwa hakika, tunatambua umuhimu wenu katika kutimiza wajibu wa taaluma yenu na tunathamini kwa kiwango cha hali ya juu mashirikiano yenu kwetu kwa kuitikia wito na kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazoandaliwa na Chama chetu The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi).


Mchango wenu na kazi kubwa mnayoifanya ya kuwapasha habari wananchi wetu kuhusiana na mambo mbali mbali umesaidia kwa kiasi kisichomithilika kuimarisha na kukuza demokrasia nchini kwa mustakbali wa utu wa wananchi wan chi yetu na hadhi ya nchi yetu.

Ndugu waandishi wa habari,
Kama mnavyojua, leo ni tarehe 5 Novemba, 2016. Tarehe kama ya leo, mwaka 2009 (yaani miaka saba iliyopita) nchi yetu tuipendayo, Zanzibar, iliandika historia mpya pale viongozi wawili: aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Zanzibar, Dr. Amani Abeid Karume, na Katibu Mkuu wa CUF-Chama Cha Wananchi, Maalim Seif Sharif Hamad, walipokutana Ikulu mjini Zanzibar na kufanya mazungumzo na baadaye, kwa pamoja, kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kwamba katika mazungumzo yao hayo ya faragha, kwa takribani masaa mawili, walikubaliana kuanza ukurasa mpya na kumaliza kabisa miongo ya migogoro ya kisiasa iliyoikabili Zanzibar kwa muda mrefu.

Uamuzi huu wa viongozi hawa kukutana na kutangaza hadharani nia yao haukuwa rahisi, hata hivyo kwa kuongozwa na dhamira njema, na hisia za mapenzi kwa nchi yetu na wananchi wenzetu, Dr. Karume na Maalim Seif waliamua kujitolea kujenga misingi ya enzi mpya za siasa.

Kwa kutambua kwamba katika vyama vyao viwili, CUF na CCM, wapo watu waovu wasiopendelea umoja na masikilizano miongoni mwa Wazanzibari ambao wasingewaunga mkono na pengine wangeyatumia MARIDHIANO yale kutaka kuwahujumu kisiasa viongozi hao, Dr. Karume alipendekeza kwa shujaa mwenzake Maalim Seif Sharif Hamad kukubali rai ya kufanya kura ya maoni ili kupata ridhaa ya Wazanzibari kuhusiana na mwelekeo huo mpya wa siasa na hasa kuhusu haja ya kuanzisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa nia na dhati ya dhahiri, hatua mbalimbali zilichukuliwa na kudhihirisha umakini na utayari wa hali ya juu na nia ya kweli kuleta na kusimamia maridhiano. Kwa mfano, tafauti na miafaka kadhaa iliyowahi kusainiwa, maudhui ya muswada wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) uliwasilishwa kwa wananchi, na kujadiliwa kupitia semina na vyombo mbalimbali vya habari kabla ya kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi kwa kusomwa na kupitishwa Mnamo tarehe 28 Januari, 2010 Kiongozi wa kambi ya upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Abubakar Khamis Bakar aliwasilisha muswada wa kuruhusu mabadiliko ya Katiba kutoa fursa ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2010. Tarehe 30 Machi, 2010 muswada huo ulipitishwa kwa kuridhiwa na wajumbe wote wa Baraza hilo na baadae kutiwa saini na Rais wa Zanzibar.

Kuridhiwa na kupitishwa kwa muswada huu na Wawakilishi wa Wananchi kulidhihirisha namna na jinsi wazanzibari walivyochoshwa na mifarakano ya kisiasa na kumaanisha kuwa wananchi wa zanzibar walichagua kuzika na kusahau kabisa tafauti zao za kisiasa na kuwa tayari kufanya kazi pamoja na kwa umoja na kujiweka mbali na migawanyiko.
Aidha, kura ya maoni ya kwanza katika historia ya Zanzibar ya tarehe 31 Julai, 2010 na matokeo ya asilimia 66.4 ya Wazanzibari kuchagua MARIDHIANO na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa yalibainisha uamuzi na khiari ya wazanzibari kukataa chuki na kuchagua upendo, kukataa khofu na kuchagua matumaini. Kwa kura hiyo ya maoni tulichagua amani na kukataa fujo.
Ndugu waandishi wa habari,

TAATHIRA ZA MARIDHIANO
Kufuatia Maridhiano ya tarehe 5 Novemba, 2009 na juhudi kadhaa zilizopelekea kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, amani, umoja na mapenzi baina ya raia wa nchi yetu Zanzibar vikaanza kujengeka siku hadi siku. Maelewano miongoni mwa watu wetu yaliimarika na masikizano kushamiri kila uchao.

Vurugu na Mitikisiko ya kisiasa hasa kabla na kila baada ya Uchaguzi, ikaondoka na kuanza kusahaulika miongoni mwa wananchi wa nchi yetu. Kwa mara ya kwanza, michakato ya kabla ya Uchaguzi, ikiwa ni pamoja na uandikishaji na kampeni za Uchaguzi Mkuu, na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010 ulifanyika kwa utulivu na amani ya hali ya juu. Hali hii kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na utashi wa kisiasa miongoni mwa Mamlaka zenye majukumu mbalimbali kama ilivyodhihirika katika hatua zote za mchakato, matayarisho na utangazaji wa matokeo ya uchaguzi. Kwa mfano, katika kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2010, viongozi wa kisiasa, kutoka katika vyama vyote vya siasa, walijiepusha na kuacha kabisa matumizi ya lugha chafu zenye kuudhi na lugha za kashfa na matusi zinazoweza kupelekea uvunjifu wa amani.
Hali hii ilipelekea hadhi ya demokrasia ndani ya nchi yetu kuanza kuimarika na kusifika kwa jumuiya za ndani, kikanda na kimataifa. Kwa mfano, katika moja ya ya Taarifa za waangalizi wa Uchaguzi wa kimataifa iliyochapishwa mapema mwezi Februari, 2011 ilisomeka kama ifuatavyo:

“the power – sharing agreement reached between the two historic rivals CCM and CUF made the campaign uneventful and free of the violent rivalry seen in past elections”
Kwa hakika, hali hii ilichangiwa na ustaarabu wa hali ya juu na ukomavu mkubwa wa kisiasa wa Maalim Seif Sharif Hamad kwa tamko lake, lililotolewa hadharani, kwamba angekuwa tayari kufanya kazi kama Makamu wa Kwanza wa Rais iwapo yeye na chama kilichomsimamisha angeshindwa katika Uchaguzi huo.
Kutokana na Maridhiano, wachambuzi wa masuala ya kisiasa, taasisi za ndani na Jumuiya ya Kimataifa zilibaini hatua kadhaa muhimu katika kuimarisha na kuboresha utendaji kazi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambayo mara zote imekuwa ikilalamikiwa. Zifuatazo ni hatua zilizobainika kuchukuliwa na Tume yenyewe na Mamlaka mbalimbali katika kuboresha ZEC:
• Kwa msaada wa United Nations Development Programme (UNDP) ZEC ilianzisha kituo cha majumuisho ya kura katika hoteli ya Bwawani. Kituo hiki kilianzishwa kwa madhumuni maalum ya kupokea na kutangaza matokeo kutoka katika majimbo ya Uchaguzi.

• Tafauti na mwaka 2000 na 2005 ZEC ilitoa muda wa kutosha kwa wapiga kura kuhakiki taarifa zao. ZEC ilibandika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) kuanzia 14 Juni hadi 20 Juni, kwa wapiga kura kuhakiki taarifa zao na kutoa taarifa za kasoro zilizobainika. Pia, ZEC walitangaza na kufanya uhamasishaji wa kutosha kuhusu zoezi hilo kupitia vyombo vya habari kama vile televisheni publicized the (TVZ) Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) na gazeti la Zanzibar Leo.

Aidha, katika Uchaguzi wa Oktoba2010, Jeshi la Polisi na vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama walitekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu katika kipindi chote cha Uchaguzi ikilinganishwa na Chaguzi zilizopita. Yafuatayo yalibainika kama utendaji mwema na uliotukuka miongoni mwa vyombo vya Ulinzi na Usalama siku ya kupiga kura:
• Kutoa mssaada kwa waja wazito, watu wazima na vikongwe, wagonjwa na watu wenye ulemavu.
• Kutumia lugha rafiki kwa wapiga kura na wadau wote wa uchaguzi
• Kutoa mashirikiano ya kutosha na maingiliano mema na wadau wote wa Uchaguzi.

CHOKOCHOKO ZA KUVIZA MARIDHIANO
Mbali na ukweli kwamba Maridhiano ya kisiasa yalikuwa na nia njema na kupokelwa na wananchi kwa moyo mkunjufu na furaha kubwa, kulikuwa na ishara za wazi kuwa kulikuwa na kikundi kidogo cha watu waliokuwa hawakufurahishwa na hatua hiyo kama ilivyobainika awali na Dr. amani Karume na Maalim Seif Sharif Hamad.
Kwa mfano, hata baada viongozi wa juu wa kisiasa na juhudi kubwa za Kamati ya Maridhiano kutoa elimu juu ya umuhimu wa Maridhiano na umoja wa Wazanzibari, kuliibuka kundi lililoendesha mkakati na chokochoko za chini kwa chini kwa lengo la kuviza Maridhiano hayo.

Miongoni mwa mifano ya hatua za kuviza maridhiano na mapatano ya wazanzibari, ni kuibuka kwa kundi la watu walioendesha kampeni za kificho kupinga na kushawishi wengine kutokubaliana na mpango wowote wenye dhamira ya kuleta maelewano miongoni mwa wananchi na kuundwa kwa serikali ya pamoja baina ya vyama vitakavyoshiriki Uchaguzi na kufikia matakwa ya Kikatiba kama ilivyowasilishwa na kupitishwa na Baraza la Wawakilishi.

Kundi hili lilianzishwa na kutekeleza mipango yake haramu siku chache kabla ya Kura ya maoni iliyolenga kuwapa fursa wananchi kuamua mustakbali wa umoja na maelewano katika siasa na mfumo wa uendeshaji wa serikali yao.

Kutekeleza mikakati ya mipango yake, kundi hili la watu wachache liliendesha kampeni ya kushawishi watu kwa kusambaza vipeperushi kuikataa serikali ya umoja wa kitaifa. Kwa mfano, moja kati ya vipeperushi vilivyosambazwa na kundi hili vilisomeka ilinde nchi yako Julai 31 kwa Hapana.

Pia, kundi hili lilitumia mbinu za kuandika maneno, katika mbao za matangazo zinazomilikiwa na ofisi za Chama tawala, yaliyolenga kuwachochea wananchi kukataa umoja na maelewano. Mfano wa mabo zilizotumika kutekeleza jukumu hili ni ubao wa maskani ya CCM iliyopo katika eneo la Mwembe Kisonge, mjini Unguja.
Kwa upande mwengine, Maridhiano ya kisiasa ya Wazanzibari yalivizwa na watendaji waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wanasiasa wenye ushawishi mkubwa katika siasa za Zanzibar wanaotoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa mfano, mbali na wale ambao kwa dhahiri walijionesha kuyaunga mkono kwa sababu tu walitaka kulinda ulwa wao kwa kumridhisha Rais aliyekuwa madarakani lakini kwa siri wakiyapinga.
Kwa mipango na mikakati yao waliyoitekeleza kwa kificho kikubwa, kundi hili la wahafidhina wa kisiasa lilifanikiwa kuwarubuni wananchi wa zanzibar kukataa siasa za maelewano na hatimaye 33.6% ya wananchi waliojotokeza kupiga kura ya maoni kuhusu serikali ya Umoja wa Kitaifa walikataa serikali hiyo.

Uamuzi wa wananchi kukubali kushiriki kura ya maoni na kuchagua Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa zaidi ya asilimia 66.4% na kuimarisha umoja wa wananchi hakukulivunja moyo wala kulirejesha nyuma kundi hili thakili na katili kwa mustakbali wa wazanzibar, badala yake likajiimarisha na kubadili mbinu kila baada ya muda na kupambana na kila aliye mstari wa mbele kuimarisha umoja wa wazanzibari.
Baada ya kuondoka madarakani kwa Rais Amani Abeid Karume, ambaye ndiye mmoja wa waanzilishi wa maridhiano ya kisiasa Zanzibar, yaliyopelekea masikilizano na kuwa na Uchaguzi uliofanyika bila ya kumwagika damu ya wananchi, kundi hili lilijidhatiti na kuhakikisha makubaliano ya maridhiano hayatekelezwi na kwa hiyo lengo la maridhiano hayo halifikiwi.

Kukamilika kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2010, kulitoa fursa kwa wahafidhina kuwatumia mawakala wao waliomo katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuandaa na kutekeleza mpango wa uanzishwaji wa makundi na taasisi za kiraia zilizoendesha mkakati wa utekelezaji wa mpango wa kuhubiri mifarakano na utengano katika jamii. Kwa mfano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliruhusu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wazee Wastaafu Wakulima na Wakwezi iliyukuwa ikiratibu, kufadhili na kusimamia kufanyika kwa makongamano na semina zilizochochea chuki baina ya watu wa asili tafauti zilizopo Zanzibar na kualikwa kwa watu mbalimbali waliokuwa wakitoa mada kuhusu historia za uongo na upotoshwaji wa matukio katika historia ya Zanzibar.

Baada ya kuanza kazi kwa Serikali mpya iliyokuwa chini ya mfumo mpya wa Umoja wa kitaifa, iliyoundwa na vyama vya CCM na CUF, dalili za kuikwamisha Serikali hiyo zilionekana waziwazi. Kwa mfano, mbali na ukweli kwamba Serikali hiyo ilipatikana kwa maridhiano, kuwa kwake na idadi zaidi ya mawaziri na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, iliwapa jeuri na kuwajengea kibri cha hali ya juu viongozi wa CCM kufanya wanavyotaka bila ya kujali maslahi ya nchi na mustakbali wa maridhiano yaliyopatikana kwa gharama na juhudi kubwa za wadau mbalimbali.
Kwa kuwa kwao sehemu ya mkakati wa kuviza maridhiano na kukataa kwa makususdi kuchukua hatua dhidi ya inda, kedi na dharau ya hali ya juu dhidi ya umoja wa kitaifa wa wananchi, kulilichochea kundi hili lililoweka mbele maslahi binafsi kuongeza na kuimarisha vitimbi vyake dhidi ya mfumo mpya wa Serikali na viongozi kutoka CUF.

Kwa mfano, katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 25 Oktoba, 2015, kundi hili lilibuni na kuandaa mbinu chafu za kila aina kuhakikisha kuwa mfumo huu wa serikali ya umoja wa kitaifa unaondoshwa kwa gharama yoyote na kwamba maridhiano yaliyolenga kuondoa mifarakano na misuguano katika jamiii yanazikwa rasmi na kurejesha upya siasa za chuki, visasi na mivutano katika jamii ya wazanzibari.


Hatimaye, kwa nia zao mbaya, mikakati yao miovu na kwa kuzitumia Mamlaka za Dola na vyombo vya Serikali, Wahafidhina wa kisiasa walimchochea na kumhakikishia, kwa kumpatia ulinzi, kada wa CCM na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jecha Salum Jecha, kufuta Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kutangaza, kusimamia na kuongoza kufanyika kwa Uchaguzi haramu wa tarehe 20 Machi, 2016.

ATHARI ZA CHOKOCHOKO KWA MARIDHIANO
Athari za chokochoko kwa maridhiano ya kisiasa ya wazanizbari ni wazi na bayana. Matokeo ya matendo ya kulazimisha matakwa na misimamo ya CCM katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ni:
• kutamalaki kwa ukatili dhidi ya ubinadamu,

• kuweka madarakani utawala haramu kwa mtutu wa bunduki na nchi yetu kuendeshwa kiimla kinyume na matakwa ya Sheria na Katiba ya nchi,
• kamatakamata ya raia wasio na hatia na kuwaweka kizuizini kwa kuwanyima haki zao za msingi na kikatiba,
• mateso na vipigo kwa raia wasio na hatia,
• ubakwaji wa wanawake na unyanyasaji kijinsia wa watoto kike na uonevu wa kila aina ikiwa ni pamoja na kuwalazimisha watu kuhama katika maeneo yao ya maisha na kutafutia riziki na jinai nyengine mbalimbali, yamechochea khofu, chuki, uhasama, malumbano na hatimaye migogoro miongoni mwa makundi yenye itikadi tafauti za kisiasa Zanzibar.
Unyama wa aina hii umeshamirisha na kupelekea kuaminika kwamba manyanyaso ya Dola na Mamlaka za serikali, ambazo hujidhatiti kukilinda chama tawala CCM dhidi ya vyama vyenye msimamo wa dhati tafauti na chama hicho, ni halali katika kuangamiza jamii kwa kutumia silaha kuleta maafa na misiba kwa raia wanyonge wasio na hatia na kinyume na Sheria za nchi na matamko mbalimbali ya Haki za Binadamu ulimwenguni, na hivyo kuirudisha Zanzibar nyuma kimaendeleo kutokana na raia wake kuwa na khofu na kugawika kimatabaka. Zaidi ya yote, hali hii imeondoa murua wa watu walio na asili ya historia ya karne na dahari za miaka ya kuishi pamoja kwa umoja, upendo na maelewano makubwa.

MSIMAMO NA TAMKO LA CUF KATIKA SUALA LA UMOJA WA KITAIFA-ZANZIBAR
Katika maelezo tuliyoyatoa na matukio tuliyoyataja hapo juu, na mengi mengine ambayo hatukuyaorodhesha katika taarifa yetu hii, imebainika kuwa kufikiwa kwa Maridhiano na masikilizano ya wazanzibari, kama ilivyoasisiwa na Dr. Amani Karume na Maalim Seif Sharif Hamad hakukupokelewa vyema kwa baadhi ya watu na Mamlaka za kada mbalimbali nchini, hivyo kupelekea hatua kadhaa na juhudi mbalimbali kuchukuliwa kuviza Maridhiano hayo na hatimaye kuyavunja kabisa.

Hata hivyo, mbali na ukweli huo pamoja na juhudi hizo ovu za kuturudisha tulikotoka, ukweli mmoja umeendelea kubaki hai na kwamba Wazanzibari wengi hawako tayari kurudishwa walikotoka kama inavyojidhihirisha katika taarifa yetu hii. Kwamba, mbali na vitimbi, visa na mikakati miovu dhidi ya umoja wetu, Wazanzibari wameendelea kusimamia maamuzi yao ya Maridhiano. Hii imechangiwa na kuonekana kwa faida ya siasa za MARIDHIANO, UMOJA, UPENDO, MATUMAINI NA AMANI miongoni mwa wananchi katika kipindi chote cha mwisho cha Urais wa Dr. Amani Karume. Kwa msimamo huo wa wananchi, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi):

1. kinawapongeza waasisi wa Maridhiano, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dr. Amani Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais-Mstaafu na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad kwa busara zao za kuweka kando misimamo na itikadi zao za kisiasa na kwa ujasiri wao mkubwa wa kuwaunganisha wazanzibari. Uamuzi wao huo, na juhudi kubwa zilizochukuliwa na Kamati ya Maridhiano, chini ya Mzee Hassan Nassor Moyo, ziliwapa fursa kubwa na ya kipekee wananchi wa Zanzibar kuishi katika utulivu mkubwa, maelewano na mashirikiano ya hali ya juu huku wakionja na kufaidi ladha ya udugu wa kweli na maelewano baina yao. Kwa kiasi kikubwa, juhudi zao zimechangia kuwa na watu waungwana, wenye kustahamiliana na kuvumiliana hadi leo hii wakati ambao tunapitia changamoto kubwa za kisiasa na kimaendeleo.

2. kinawaahidi wazanzibari kuwa pamoja nao katika msimamo wao wa kuchagua Maridhiano na kwamba daima kitasimamia Umoja na masikilizano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar na watanzania wote na kamwe hakitarudi nyuma katika kufanikisha malengo ya Maridhiano ya Wazanzibari.

3. Kinawatanabahisha wazanzibari na Watanzania wote kuwa tunayopitia sasa ni majaribu tu ya kututayarisha na kutujenga katika jukumu kubwa na zito la kusimamia, kuendeleza na kufikia malengo ya ZANZIBAR YENYE UHURU NA MAMLAKA YAKE YA KWELI yaliyoletwa na Mapinduzi ya 1964 kwa lengo la kulinda heshima, utu, umoja na maelewano miongoni mwa wazanzibari wa asili zote.

4. CUF-Chama Cha Wananchi kinawanasihi wananchi wote kwamba wasikubali kushindwa na kurudishwa tulikotoka. Tuwaoneshe kwa vitendo wahafidhina kwamba mbinu zao ovu za kuviza Maridhiano hazitafanikiwa na kwamba hali inayoikabili nchi yetu kwa sasa ni ya muda tu, kwani hatimaye kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu batili itashindwa na HAKI SAWA KWA WOTE itasimama katika nchi yetu

HAKI SAWA KWA WOTE
SALIM BIMANI
KAIMU NAIBU KATIBU MKUU-ZANZIBAR

No comments :

Post a Comment