Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) Kambi ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kimesema kinakwenda Mahakama ya Rufani kumpinga Jaji Sekieti Kihiyo baada ya kugoma kujitoa kwenye kesi yao.
Kesi hiyo imefunguliwa na sehemu ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho, wanaoungwa mkono na Maalim Seif dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na msajili, Profesa Ibrahim Lipumba.
Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho, ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya na wanachama wengine tisa waliosimamishwa uanachama. Mwingine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016, bodi ya wadhamini CUF inaiomba mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kuwa ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CUF.
CUF iliwasilisha maombi ikimtaka Jaji Kihiyo ajitoe kusikiliza kesi hiyo Desemba 6 mwaka jana, licha ya mambo mengine ikidai haina imani naye.
Katika uamuzi wa Desemba 14 mwaka jana, Jaji Kihiyo aligoma kujitoa katika kesi hiyo akidai kuwa sababu zao hazina msingi na wadai wanachokifanya ni kumtafuta jaji wanayemtaka wao.
Hata hivyo, jana kesi hiyo haikuendelea na Jaji Kihiyo aliahirisha baada ya wadai kusisitiza kutokumkubali. Wakili wa wadai hao, Juma Nassoro aliieleza Mahakama kuwa wameamua kwenda Mahakama ya Rufani kukata rufaa kupinga uamuzi wake.
No comments :
Post a Comment