Mgombea wa ubunge Korogwe Vijijini (CCM), Timotheo Mzava amepita bila kupingwa katika uchaguzi wa mdogo wa marudio.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mzava kujikuta pekee yake muda wa kurudisha fomu ambao mwisho ulikuwa jana Agosti 20, 2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa Korogwe, Dk George Nyaronga ambaye ndio msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo amesema, “mgombea wa CCM amepita bila kupingwa.”
Awali Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alilalamika 'rafu' iliyochezwa baada ya mgombea wake katika jimbo hilo kuenguliwa kwa kushindwa kurejesha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi huo.
Golugwa, amesema alifika katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi huo akiwa na mgombe wao, Amani Saguti majira ya saa 5:38 asubuhi kwa lengo la kurudisha fomu.
Amedai kuwa walipofika katika ofisi hiyo, walimkuta msimamizi wa uchaguzi, Samia Guram, lakini alikataa kuzipokea fomu hizo kwa madai kuwa muda wa kurudisha fomu ulikuwa haujafika.
Jana ilikuwa siku ya mwisho ya kurudisha fomu kwa waliotia nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo ambalo limelazimika kufanya uchaguzi kutokana na kufariki dunia kwa aliyekuwa mbunge wake, Steven Ngonyani 'Prof. Maji Marefu' mwezi uliopita.
"Alituambia tusubiri hadi saa 10 jioni ndipo atapokea fomu za mgombea wetu," Golugwa alisema na kueleza zaidi:"Tulihoji kisheria lakini hatukupata majibu sahihi, ndipo tukaamua kwenda kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Korogwe."
Hata hivyo, Golugwa alisema hawakufanikiwa kuonana na Mkurugenzi wa Wilaya ya Korogwe, wakielezwa kuwa alikuwa amekwenda kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo.
Golugwa aliendelea kueleza kuwa kutokana na kushindwa kuonana na kiongozi huyo, waliamua kurejea kwenye ofisi ya msimamizi wa jimbo, lakini walikuta mlango umefungwa na hapakuwapo ofisa yeyote wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
"Tulilazimika kukaa nje ya hiyo ofisi kusubiri. Wakati tunasubiri, CUF (Chama cha Wananchi) walifika kuleta fomu," Golugwa alisema.
"Hata ACT-Wazalendo nao walifika, na ilipofika saa tisa alasiri, CCM (Chama Cha Mapinduzi) nao walifika kurudisha fomu, hivyo wote tukawa nje tunasubiri."Alisema kuwa ilipofika saa 10:30 jioni, mgombea wa CCM na wafuasi wake waliondoka bila ya kuwapo kwa taarifa yoyote kutoka ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo.
Hata hivyo, Golugwa alisema ilipofika saa 11:15 jioni, alifika mtu katika eneo hilo na kujitambulisha kuwa ni ofisa utumishi akifuatana na askari polisi wenye silaha, akabandika karatasi iliyoonesha mgombea wa CCM amepita bila kupingwa.
Golugwa alisema kuwa walipojaribu kuhoji hatua hiyo, askari polisi hao waliwazuia na kuwatisha kuwapiga risasi.
Awali, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema wagombea wao katika majimbo mengine mawili, Yonas Laizer (Monduli) na Asia Msangi (Ukonga) walifanikiwa kurejesha fomu za kuwania ubunge jana. Uchaguzi huo umepanga kufanyika Septemba 16.
No comments :
Post a Comment