Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, October 8, 2018

Serikali yafungia maduka ya madini Dar!


Serikali imeyafunga maduka matano ya kuuza vito jijini Dar es Saalam kutokana na sababu mbalimbali.

Sababu za kufungwa kwa maduka hayo ni kubainika kutokuwa na leseni, kumbukumbu za mauzo, kutokulipa kodi na kukutwa na madini ya fedha.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanyika kwa operesheni ya ukaguzi ya siku tatu mwishoni mwa wiki kwenye maduka hayo eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

“Operesheni ilikuwa na lengo la kuangalia maduka ya sonara katika eneo la Kariakoo kama yana leseni na tumebaini maduka matano hayana na tumeyafunga maduka hayo,” alisema Waziri Kairuki.

Aliongeza kuwa katika operesheni hiyo walimkamata mfanyabiashara wa vito, Al Hassan ambaye hakuwa na leseni ya kuuza madini, pia hajawahi kulipa kodi tangu mwaka 2004.Waziri Kairuki alisema katika operesheni hiyo pia waliwabaini wafanyabiashara wa vito wengi kutokuwa na utunzaji wa kumbukumbu wa madini waliyonunua na kuyauza.

“Utakuwa mfanyabiashara hamjui mtu aliyemuuzia madini wala yeye mwenye hajui madini alinunua kwa nani, wakati kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi,” alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki aliwataka wafanyabiashara wa madini nchini kuwa na leseni ambazo zinatolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na kufuata sheria.

Naye Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa, alisema wale wote waliobainika kutokuwa na leseni watafikishwa mahakamani.

Alisema kwenye operesheni hiyo wafanyabiashara wengi wa vito wamebainika na upungufu mwingi ikiwamo kutojaza taarifa zao za mauzo na manunuzi ya madini.

“Mtu kabla hajapatiwa leseni ya biashara ya madini anapaswa kupewa orodha ya vitu vinavyohitajika kulingana na biashara yake, zoezi la ukaguzi litaendelea kila mara,” alisema Mhandisi Mulabwa.

Kwa upande wake Meneja Ukaguzi Mkoa wa Kodi wa Kariakoo kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hashimu Ngoda, alisema wafanyabiashara wa vito eneo la Kariakoo si watoaji wa risiti.

Alisema kwenye operesheni hiyo walifanikiwa kumkamata mfanyabiashara ambaye kwa kipindi cha mwaka mmoja alitoa risiti mbili.

“Huyu mfanyabiashara risiti ya kwanza alitoa mwezi wa Januari, na risiti ya pili ameitoa Septemba, tutamfikisha mahakamani,” alisema Ngoda.

Aliongeza kuwa ukaguzi wa maduka ya vito unakuwa ni mgumu kwa sababu maduka yao mara nyingi yanakuwa yamefungwa.

No comments :

Post a Comment