Rais Paul Biya wa Cameroon
Wagombea wawili wa upinzani nchini Cameroon wamekubaliana kuungana siku moja tu kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi wake mkuu wa urais Octoba 7.
Taarifa hii inathibitisha uvumi uliokuwepo wa vyama vya upinzani kuungana kujaribu kumuangusha rais Paul Biya kwenye uchaguzi wa Jumapili, lakini muungano huu hautamjumuisha kinara wa upinzani kutoka chama cha Social Democratic Front, Joshua Osih.
Akere Muna kiongozi wa chama cha People's Development Front FDP ametangaza kukubali kumuunga mkono mgombea mwenzake Maurice Kamto wa chama cha Movement for the Rebirth of Cameroon MRC.
Siku ya Ijumaa chama cha Kamto kilitoa madai kuwa tayari mpango kubwa wa udanganyifu wa kura unafanyika kuhakikisha rais aliyeko madarakani anashinda, madai ambayo hata hivyo yamekanushwa na tume ya uchaguzi.
Mkuu wa timu ya kampeni ya mgombea Maurice Kamto, Paul-Eric Kingue yeye amesema tayari udanganyifu uliopangwa kufanyika siku ya Jumapili umepewa baraka na maofisa wa tume ya uchaguzi.
“Hatutakubali matokeo yoyote ikiwa udanganyifu huu utaendelea,” amesema Kamto wakati wa mkutano wake na wanahabari mjini Yaounde.
Mamlaka nchini Cameroon mara zote zimekuwa zikishutumiwa kwa kumpendelea Biya ili asalie madarakani.
Rais Biya alishinda kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2011 kwa asilimia 78 ya kura, uchaguzi ambao ulikashifiwa vikali na upinzani pamoja na waangalizi wa kimataifa.
Haya yanajiri wakati huu kukiripotiwa watu watatu kupoteza maisha kwenye jimbo linaloshuhudia machafuko la kaskazini mwa Cameroon ambako raia wake wanazungumza kingereza.
Kwa mujibu wa maofisa usalama nchini humo wamesema watu hao waliuawa kwenye mji wa Kumba kati ya siku ya Jumatano na Ijumaa wakatio wa makabiliano na vyombo vya usalama.
Uchaguzi wa Jumapili hii unafanyika huku kukiwa na wasiwasi wa kufanyika kwenye eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ambako wapiganaji wenye silaha wamekuwa wakiwalenga wanajeshi wa Serikali na kushinikiza eneo lao kujitenga.
Kwa mujibu wa tangazo la ikulu ya Yaounde, mpaka wa taifa hilo lenye watu takribani milioni 24 itafungwa kuanzia leo kuelekea kwenye uchaguzi wa Octoba 7.
No comments :
Post a Comment