dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, June 28, 2020

HOTUBA YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, MWENYEKITI WA ACT WAZALENDO TAIFA KWA WAANDISHI WA HABARI, TAREHE 28/06/2020 KATIKA UKUMBI WA HOTEL YA VERDE, ZANZIBAR!



Ndugu Waandishi wa Habari,

Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa asubuhi hii tukiwa wazima wa afya na kutuwezesha kuifanya shughuli yetu hii kwa salama na amani.

Pili, nikushukuruni waandishi wa habari kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuhabarisha umma juu ya mambo mbali mbali yanayohusu jamii yetu.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Tarehe 25 Oktoba, 2020 tunatarajia kuwa na Uchaguzi Mkuu wa nchi yetu ambapo wananchi wa Zanzibar tutapata fursa nyengine muhimu ya kuchagua Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani kwa upande wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar. Kwa upande mwengine, Wazanzibari pia tutaungana na Watanzania wengine kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge.

Nyote mnafahamu kuwa mimi, Maalim Seif Sharif Hamad, nimekuwa nikigombea nafasi ya Urais kwa chaguzi tano mfululizo tokea kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla mwaka 1992. Kwa sababu hii, kadiri siku zinavyokaribia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, nimekuwa nikiulizwa mara kwa mara na watu mbali mbali wenye shauku, mkiwemo nyinyi waandishi wa habari, wanachama na viongozi wenzangu, watu wenye vyama na wasio na vyama. Kila mmoja anataka kujua kama nitagombea au sitogombea.
Muda wote huo nimekuwa nikiwaeleza kuwa bado sikuwa nimefanya maamuzi kuhusu jambo hilo. Nilihitaji kwanza kufanya tafakuri ya kina, lakini pia nilitaka kupata ushauri wa viongozi wezangu, familia yangu na wazee wa busara ninaowaheshimu.

Baada ya kufanya tafakuri ya kina na kupata ushauri wa makundi niliyoyataja hapo juu, nina furaha kubwa leo kuwaambia wananchi wa Zanzibar kupitia kwenu kuwa sasa nimeshafanya maamuzi na maamuzi yangu ni KWAMBA INSHA ALLAH NITAGOMBEA nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa mara nyengine tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2020.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Kwa nini nimefikia uamuzi huo?

Nina sababu tano (5) zilizonisukuma kufikia uamuzi huu ambazo ni hizi zifuatazo:-

1. Hata kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, mimi na wenzangu kadhaa tulikuwa haturidhishwi na jinsi nchi yetu inavyoendeshwa. Kwa pamoja, tulianzisha vuguvugu (movement) la kuweka shinikizo kwa dola kuruhusu mfumo wa vyama vingi. Vuguvugu hilo lililoongozwa na KAMAHURU kwa upande wa Zanzibar na makundi mengine yenye madhumuni kama hayo kwa upande wa Tanzania Bara yaliweza kufanikiwa kuifanya nchi kuingia katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Hivi sasa, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi upo hatarini kutoweka kutokana na Watawala wa Tanzania kuamua kwa makusudi kuvunja misingi ya demokrasia. Kwa kuzingatia hatari hii, nimeona ni hekima kukubali ushauri wa watu wengi kwamba huu siyo wakati wa kuacha mapambano bali nina wajibu wa kusaidiana na Viongozi Vijana kuwavusha katika wakati huu mgumu katika historia ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

2. Mimi na wenzangu, mwaka 1992, tuliamua kuanzisha chama cha siasa (Chama Cha Wananchi – CUF) na kuwashawishi wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kukiunga mkono. Kwa kuwa CUF ilikuwa na malengo ya wazi ya kurejesha haki kwa wananchi wote bila ya ubaguzi, kikipinga ubaguzi, ukandamizaji na hali ya nchi kukwama kama si kurudi nyuma kimaendeleo, ilikuwa ni desturi tulipozungumza ilikuwa tunawasemea wananchi. Hili lilikuwa ni mwiba kwa watawala wasiopenda kuiona Zanzibar ikikwamuka na Wazanzibari wakipiga hatua kubwa za maendeleo. Hivyo, walipoona njama na hila zao za miaka takriban 27 zilizolenga kukikosesha imani ya Wazanzibari hazifanikiwi, wakaamua kutumia Dola na Taasisi zake, na hasa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mahkama, kukiingilia chama kile na kukidhoofisha kwa kukikabidhi kwa vibaraka wao ambao walipewa kazi ya kutufukuza uanachama mimi pamoja na wenzangu kinyume na matakwa ya wanachama. Baada ya hatua hiyo, ndipo mwaka jana tulipoamua kushusha tanga na kupandisha tanga na kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaongoza Wazanzibari maelfu kwa maelfu kutuunga mkono. Katika hali hii, nimeona haitakuwa busara, nikiwa nahodha mzoefu, kuwaongoza watu kuingia katika jahazi jipya na kisha kuwaacha mkondoni. Nimekubali ushauri kuwa niongoze juhudi za pamoja za kuleta Mabadiliko Zanzibar kupitia ACT Wazalendo hasa wakati huu nchi yetu inapoelekea kuandika historia mpya katika zama mpya. Jahazi jipya linahitaji Nahodha mwenye uzoefu mkubwa aweze kuivusha nchi yetu kupisha dhoruba kali na mawimbi mazito yanayoikabili.

3. Viongozi na wanachama wenzangu waliniamini na kunikabidhi dhamana ya kupeperusha bendera ya chama tulichokuwepo awali katika kuwania kiti cha Rais wa Zanzibar katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015. Katika chaguzi zote hizo, Wazanzibari walinipa imani zao na katika kila uchaguzi uliofuata, Wazanzibari wengi zaidi walinipa imani zao kwa maana ya kuongeza idadi ya kura nilizopata. Nimeona si uungwana hata kidogo kudharau imani hiyo isiyokwisha kwangu na ambayo imekuwa ikiongezeka kadiri siku zinavyokwenda; na badala yake napaswa kuiheshimu kwa kuwaongoza Wazanzibari kuifikia ndoto ya Zanzibar wanayoitaka.

4. Katika chaguzi zote zilizotangulia, nguvu za giza za watawala (Deep State) kupitia CCM zilitumika kupuuza maamuzi ya wananchi na kulazimisha wagombea wa CCM kutangazwa washindi licha ya kukataliwa na Wazanzibari. Nimeona kuwa wakati umefika kwa nguvu hizo za giza za watawala kutambua kuwa nguvu ya umma inapoamua kamwe haiwezi kushindwa na kwamba uchaguzi huu tutaulinda ushindi wetu katika hali yoyote ile na kisha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama masharti ya Katiba ya Zanzibar yanavyotaka.

5. Uchaguzi Mkuu wa 2015 ulikuwa ni tukio la kubadilisha historia Zanzibar (Waingereza huita ‘watershed’) kwa maana kwamba Wazanzibari walio wengi zaidi walikataa kuongozwa na CCM. Lakini ‘Deep State’ haikujali kuwa CCM imeshapoteza imani ya Wazanzibari na iliwatumia JWTZ na vyombo vyengine vya ulinzi na Jecha Salim Jecha ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kupindua matokeo ya uchaguzi huo na kulazimisha kumpandikiza Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar kinyume na matakwa na ridhaa ya Wazanzibari. Nimeona kuwa ni wajibu wangu kuwapa Wazanzibari kile walichokitaka mwaka 2015 kwa kurudi tena kwao na kuwaomba wadhihirishe tena chaguo lao la mwaka 2015 na kuionesha dunia kuwa maamuzi ya wananchi ni yale yale. Kitakachokuwa tofauti ni kwamba mwaka 2020 mshindi wa Urais atakuwa Rais, Inshallah.
Licha ya sababu hizo tano (5) nilizozitaja hapo juu, ilibidi nijiulize sana suala la JE, BADO WAZANZIBARI WANA IMANI NAMI?

Ikabidi niwaombe baadhi ya wataalamu kufanya utafiti wa kimya kimya ili kujua kuwa imani ya wananchi kwangu ikoje? Imeshuka, au imebaki pale pale, au imepanda?

Nilishangaa kwa furaha wataalamu hao waliponiletea matokeo ya utafiti wao kuwa imani ya Wazanzibari kwangu haijameguka ingawa wako wachache waliosema sikutimiza ahadi yangu ya kuwarejeshea haki yao ya 2015.

Pia utafiti umeonesha kuwa hata hao wachache waliosema kuwa sikutimiza ahadi ya kuwarejeshea haki yao, walipoulizwa zaidi walisema kwa mazingira ya sasa, pamoja na kuwepo kwa wana-ACT wengi wenye uwezo wa kushika nafasi hiyo, Maalim Seif anabaki kuwa turufu yao. Wengine walitishia ikiwa Maalim Seif hatagombea ama wataandamana au hawatapiga kura.

Hivyo, nimejiona sina jinsi isipokuwa kukubali matakwa ya wapiga kura kuwa niingie tena katika kinyang’anyiro hicho kwa mwaka huu wa 2020. Ukiwa muungwana ukipewa imani na wenzako huna budi urejeshe imani hiyo kwa imani. Mimi Maalim Seif nimekuwa na Wazanzibari katika muda wote wa maisha yangu; wamekuwa na imani kubwa juu yangu, na kwa hivyo, sijaona sababu ya kuvunja imani hiyo.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Ukiacha hayo, naumia moyoni kuona Zanzibar inavyorudi nyuma kimaendeleo mwaka hadi mwaka. Ubaguzi chini ya Serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein umekubuhu na kurasimishwa. Wananchi wananyimwa haki za msingi kwa itikadi zao ikiwa ni pamoja na kunyimwa haki yao ya kuchagua viongozi wawatakao, haki ya elimu ya juu, haki ya ajira n.k. 

Inanisikitisha na kuniumiza sana kuwa kazi nzuri tuliyoifanya kwa pamoja Mhe. Dk. Amani Abeid Karume na mimi, tukisaidiwa na Kamati ya Maridhiano, ya kuwaunganisha Wazanzibari kupitia Maridhiano, leo Viongozi wa SMZ chini ya Dk. Ali Mohamed Shein wameibeza. Badala yake wamejitahidi sana kutugawa Wazanzibari kwa njia za ubaguzi. Viongozi wa CCM Zanzibar wa leo wanamkashifu Rais Mstaafu Amani Karume eti kwa kuwaletea matatizo. Yaani kuwaunganisha Wazanzibari kwao ni matatizo. Udhalimu huu lazima ukomeshwe. Na mimi najiona nina dhima hiyo.

Rushwa na uhujumu wa uchumi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa sasa wa serikali iliopo madarakani umezidisha umasikini na nchi kutosonga mbele kimaendeleo. Kuna mifano mingi tu:-

Baadhi ya Mawaziri wamefikia hadi kupelekewa pesa majumbani kwao kwa makapu, watu kunyang’anywa viwanja walivyovipata kihalali na kisha kupewa wengine wenye fedha, miradi inayogharamiwa na ZSSF ni miradi ya ulaji kwa wakubwa, miradi inayonuka rushwa na ufisadi. Zanzibar inahitaji Kiongozi shupavu atakayeifanya nchi yetu na Serikali yake iwe na ZERO TOLARENCE dhidi ya rushwa. Najiona ninayo sifa hiyo, na Wazanzibari ni mashuhuda wa hilo.

Heshima, hadhi na haiba ya Zanzibar kila uchao inashuka na kuporomoka. Zanzibar inazamishwa kwa nguvu. Zanzibar iliyokuwa maarufu kwa mambo mengi mema na mazuri leo inasikitisha kuwa hata kutajika haitajiki tena duniani. Bila ya kwenda mbali, hapo Kenya tu kuna watu ukiwauliza Zanzibar iko wapi hawajui tena. Tunahitaji Muungano wenye usawa, haki na heshima baina ya nchi mbili zilizoungana. CCM wameshindwa kulinda heshima, hadhi na haiba ya Zanzibar. CCM imeshindwa kutetea haki za Zanzibar katika Muungano.

Tunahitaji kiongozi anayejiamini, anayetambua uhalali wake unatokana na Wazanzibari na ambaye ataweza kukaa na viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa misingi ya usawa, haki na heshima kuweza kupigania haki za Zanzibar kwa hoja na mazungumzo. Najiona kiongozi huyo ni mimi.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Sote tunajua kuwa mgombea yeyote wa CCM atakayeletwa hatakuwa na ujasiri na uthubutu wa kudai haki za Zanzibar wakati anajua waliomuweka madarakani wanaweza wakati wowote kumuondosha.

Niseme wazi kabisa kuwa pamoja na imani iliyooneshwa kwangu kama nilivyoeleza hapo juu, nitakaposhinda uchaguzi na kuongoza Serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar nitaingiza timu ya kizazi kipya cha vijana katika nafasi nyingi Serikalini. Wengi kati ya vijana hao tayari mnawajua na mmeonesha mapenzi na imani kubwa kwao. Tutakwenda na Timu Kabambe yenye Vijana weledi watakaojumuika na wazee wazoefu kuleta Pambazuko Jipya litakalotupa Zanzibar yenye haki, ustawi na utajiri kwa kila mmoja wetu.

Mwisho:

Ni nini nakusudia kuifanyia Zanzibar na Wazanzibari nitayaeleza kwa kirefu siku za mbele Inshallah.

Kwa leo nakuombeni turidhike tu kuwa ule uamuzi mliokuwa na hamu na shauku kuujua nimeuweka wazi; na kwamba nitajaza fomu za chama chetu cha ACT Wazalendo kuwania Urais wa Zanzibar, na kama chama chetu kitanikubali na kuniteua basi nitagombea nafasi hiyo.

Namuomba Mwenyezi Mungu Anisaidie.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.


No comments :

Post a Comment