Na Mwinyi Sadallah
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimesema Zanzibar itakuwa na nafasi ya kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) mara baada ya kupatikana kwa Katiba Mpya ya Tanzania mwaka 2014, ikiwa ni hatua mojawapo ya kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Msimamo huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, katika kongamano la siku moja la kumuenzi Rais wa Kwanza wa Zanzibar na muasisi wa Mapinduzi na Muungano, marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, lililofanyika katika chuo cha Afya Mbweni, mjini hapa.
Vuai alisema suala la kujiunga na OIC na mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano, isiwe sababu ya kuzorotesha au kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Vuai ambaye alikuwa akiwahutubia zaidi ya wajumbe 600 kutoka mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba, ambao ni wanachama wa umoja wa vijana UVCCM, alieleza kuwa mabadiliko ya Katiba yanayokuja yana neema kubwa kwa Zanzibar ikiwemo kufanyiwa marekebisho kwa sera ya mambo ya nje.
“Kuna mambo tumekubaliana ndani ya vikao vya juu vya chama yaondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano, kama suala la mafuta na gesi asilia, bandari, takwimu na uhusiano wa kimataifa ili Zanzibar iweze kuwa na nafasi ya kujiunga na OIC au umoja wa nchi za visiwa duniani,” alisema Vuai.
Hata hivyo, Vuai alisema kama mafuta yatakuwa hayapo Zanzibar, wakati Tanzania Bara ikiwa tayari imeanza kufaidika na rasilimali hizo ikiwemo gesi, Zanzibar itakuwa imepoteza mchango mkubwa wa kiuchumi kupitia sekta hiyo kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kama yapo mafuta Zanzibar sawa, lakini kama hakuna tutakuwa tumeliwa wenzetu wameshaanza kuvuna” alisema Vuai huku akishangiliwa na vijana.
Kuhusu mchango wa Marehemu Karume, Vuai alisema kuwa umesaidia kuinua kiwango cha elimu kwa kupatikana bila ya malipo, kujenga umoja wa Wazanzibari, kudumisha misingi ya Muungano, kuwapatia makazi bora wananchi wake.
Alisema miongoni mwa faida za Muungano ni fursa zinazopatikana Tanzania Bara ambapo Wazanzibari wameweza kumiliki ardhi wakiwa raia wa Jamhuri ya Muungano, kupata matibabu sawa, pamoja na kunufaika na elimu ya juu, mbali na suala la ulinzi na usalama.
Hata hivyo aliwataka Wazanzibari kuwa makini na watu wanaotetea Muungano wa mkataba, kwa vile huwezi kuujadili Muungano wa mkataba bila ya kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Endapo mfumo wa Muungano ukibadilika, tutakuwa matatizo makubwa, ya kiuchumi, kijamii na kibiashara, sote tuna fursa sawa ndani ya Jamhuri ya Muungano bila ya ubaguzi wowote,” alisema Vuai.
Alisema bado kuna watu Zanzibar wana kiu ya kuongozwa na Sultan, kinyume na malengo ya Mapinduzi ya kutaka wananchi wajitawale wenyewe na kuwataka wananchi kuwa makini na wanaotumia siasa na dini kutaka kuvuruga amani na umoja wa kitaifa miongoni mwa watanzania.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UVCCM Martin Shigela alisema, watu wanaopandikiza chuki za kidini wana ajenda zao za siri ikiwemo kutaka kujipatia umaarufu kwa maslahi yao binafsi.
Aliongeza kuwa vijana wanapaswa kuwa makini na kujiepusha na siasa za jazba, na kutumiwa na watu wenye malengo binafsi ya kisiasa ya kutaka kuvuruga amani na umoja wa kitaifa, ikiwemo kuwagawa wananchi katika misingi ya kikanda, kama vile kudai rasilimali zinazopatikana katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment