dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, June 24, 2013

Vita ya urais: Sumaye amvaa Lowassa

NA WAANDISHI WETU

24th June 2013


Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye
Vita ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaelekea kupamba moto kutokana na kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye, akimtuhumu Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya nne, Edward Lowassa.
Sumaye ambaye jana  alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuadhimisha miaka 50 ya Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania (KKKT), alitoa kauli ambayo dhahiri ilionekana kumlenga Lowassa kutokana na tabia yake ya kutoa michango mbalimbali katika nyumba za ibada.
 
 Bila kutaja jina la Lowassa katika ibada hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Makumira kampasi ya Makumira, Sumaye alisema wanaotoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa makanisa wanatoa hongo ili kutafuta madaraka.
 
Alisema taifa sasa linakabiliwa na matatizo mengi na mojawapo ni rushwa na kusema kuwa wapo watu wanapewa sifa za ajabu siyo kwa sababu ya uadilifu wao au wema wao, bali kwa sababu tu wanahonga fedha hata kuchangia ujenzi wa makanisa kwa sababu ya kusaka madaraka.“Hatujiulizi ni kwa nini wanajitokeza wakati huu kuna uchaguzi?” alihoji Sumaye na kuongeza kuwa hata makanisa yanapokea fedha hizo bila kujiuliza.
 
Alinukuu maneno kutoka kitabu cha Kutoka 23: 8 akisema: “Nawe usipokee rushwa kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao na kuyapotosha maneno ya wenye haki.”
 
Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa kanisa hilo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, Sumaye alizidi kunukuu Biblia akisema je; kwa kupokea fedha hizo hakuhalalishi kutupwa nje na kukanyagwakanyagwa kwa kuwa chumvi imepoteza utamu wake?”
 
Alihoji kama mambo hayo ndiyo ya kusheherekea miaka 50 ya kanisa au ni lazima kuyatazama na kujirekebisha.
 
“Kama tunapokea fedha ambazo tunajua tunahongwa, bado tunajiuliza tuna macho?” alihoji Sumaye ambaye alikuwa mwasiasa wa ngazi ya juu pekee miongoni mwa walioalikwa  katika sherehe hizo ambazo zilihudhuriwa na  maaskofu wote 21 wa dayosisi za KKKT isipokuwa mmoja, wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao ambaye yuko safarini.
 
Ingawa Sumaye hakumtaja Lowassa kwa jina katika hotuba yake, lakini Lowassa amekuwa ndiye kiongozi wa kisiasa ndani ya CCM ambaye amekuwa akishiriki kuongoza harambee kadhaa za kuchangia shughuli za makanisa pamoja na kuchangia fedha.
Lowassa ameendesha harambee hizo kwa ufanisi mkubwa kuanzia ndani ya KKKT na nje ya kanisa hilo. 
 
Mbali na kuongoza harambee za makanisa mbalimbali, Lowassa pia ameshiriki katika shughuli nyingine za kijamii kama kusaidia kutunisha mifuko ya Saccos sehemu mbalimbali nchini.
 
Licha ya Sumaye kumhusisha Lowassa na mbio za kusaka urais wa mwaka 2015 baada ya Rais Jakaya Kikwete kustaafu kwa mujibu wa Katiba, na yeye (Sumaye), anatajwa kuitaka nafasi hiyo.
 
Wanachama wengine wa CCM wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea nafasi hiyo ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. 
 
Sitta mara kadhaa amesema kuwa yeye ni msafi kimaadili na kwamba anazo sifa zote za kuwa Rais.
Lowassa hajawahi kutamka rasmi kwamba atagombea urais badala yake amekuwa akisisitiza kuwa muda mwafaka ukifika atasema.
Aidha, Lowassa hivi karibuni alisema kuwa hana fedha isipokuwa ana ushawishi mkubwa wa makundi mengi ya jamii na kwamba ndiyo maana amekuwa akialikwa kuongoza harambee za kuchangia fedha na zinafanikiwa kwa kiasi kikubwa. 
 
Kwa upande wake, Membe kwa mara ya kwanza alitamka kwamba anasubiri kuoteshwa na Mungu ndipo atakapotangaza nia yake ya kugombea nafasi hiyo. Hivi karibuni alisema ataamua kama wananchi wakimtaka awanie nafasi hiyo.
 
Naye Sumaye ambaye mwaka 2005 aligombea na kushindwa ngazi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), hajawahi kutamka kuwa atagombea, lakini amekuwa akitoa kauli kadhaa ambazo zinaonyesha kuwa anakusudia kigombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.
 
Wiki iliyopita wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV, Sumaye aliikosoa utaratibu unaotumiwa na CCM wa kuwazuia wanachama wanaotaka kugombea urais kutojitangaza mapema.
 
Badala yake alikishauri chama chake kuwaruhusu wanaoutaka urais kujitangaza mapema ili wananchi wawafamu mapema iwe rahisi kwao wakati wa kupiga kura.
 
MAKAMBA: WABANENI KWA MASWALI MAGUMU
 
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, January Makamba, amewataka vijana waliopo vyuoni kuwauliza maswali magumu wanachama wa CCM walioanza harakati za chini chini za kuwania urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao. 
 
Makamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, alitoa wito huo jijini hapa  juzi usiku alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) tawi la Mwanza ambao ni wanachama, wapenzi na mashabiki wa CCM. 
 
Alisema ni jukumu la wasomi waliopo vyuoni kuwauliza maswali magumu wale wote ambao wameanza harakati za kuusaka urais ili kuwapima kama kweli wanastahili kupewa dhamana ya kushika hatamu za uongozi wa nchi na CCM. 
“Nadhani mnaona harakati zinazoendelea na bila shaka mmetembelewa na watu ambao huko nyuma hawajahi kuja hata siku moja. Ambacho nawaomba, muwaulize maswali magumu, wana mipango gani kuhusu nchi yetu kwa miaka 30 au 50 ijayo,” alisema Makamba. 
Aliongeza kwamba pamoja na maswali hayo magumu, vijana wasikubali majibu rahisi ambayo yamezoeleka kutolewa na wagombea mbalimbali waliopita, badala yake wawapime kwa umakini mkubwa wagombea hao kama kweli majibu yao ni ya dhati au ni ya funika kombe mwanaharamu apite. 
 
“Akija mgombea muulizeni mipango yake kwa vijana wasomi ni nini. Muulizeni kama anayafahamu matatizo ya Watanzania na katika majibu yake mtazameni usoni muone kama kweli matatizo hayo yanamkera. Msikubali majibu rahisi kwani anaweza kuja na majibu yaliyozoeleka kama vile nitaimarisha kilimo, nitaongeza ajira nakadhalika,” alisema Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga. 
 
Aliongeza kwamba ni muhimu vijana wasomi kuwauliza wagombea hao maswali ya msingi ambayo majibu yake yatatoa taswira ya jinsi walivyojiandaa kushughulikia matatizo ya msingi yanayowakabili Watanzania.
 
“Wakija, msiishie kuwapigia makofi kwa mfano, waulizeni kwamba tunalo Ziwa Victoria, lakini linajaa tope na samaki wanapungua, je, watafanya nini kushughulikia tatizo hili?” 
Mkiwauliza maswali ya namna hii na mengine magumu, ndiyo mtawapima na kuwajua kama kweli wanafaa kuwa viongozi.
 
Alisema haitoshi kwa wagombea hao kusema kwamba wana uzoefu wa uongozi, lakini ni muhimu waonyeshe upeo wa kuleta mabadiliko makubwa katika ustawi na uhai wa taifa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment