Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, November 25, 2013

Mnyika, Ndesamburo wakosoa gesi

NA WAANDISHI WETU

25th November 2013


Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika
Waziri  Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, ameikosoa sera ya gesi iliyotolewa wiki iliyopita kwa kueleza kuwa haiwezi kuwa jibu kamili kwa kuwa serikali ilitakiwa kuandaa kwanza sera ya sekta pana ya mafuta na nishati ndipo sera ya sekta ndogo ya gesi iandaliwe.

Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), alisema masuala yote yaliyomo kwenye sera ya gesi iliyotolewa ya sekta ndogo, yatagongana na misingi ya kisera na kisheria ya sekta mama na hivyo kusababisha kushindwa utekelezaji wake.

Alibainisha kuwa hata kama ingekuwa ni kwa sekta ndogo ya gesi, mnyororo wa gesi una hatua mbalimbali za kupitia ambazo unaanzia kwenye utafutaji, uvunaji, usafirishaji, usambazaji na hatimaye kwenye utumiaji, hatua ambazo uendelezaji wake unatofautiana.  

Mnyika alifafanua kuwa sera hiyo ya gesi imejikita zaidi katika hatua ya kati (mid stream) na hatua ya chini (down stream), na hatua muhimu ya juu (up stream) haijapewa uzito.

Alisema kutokana na sera ya gesi kutojikita katika hatua ya juu ambayo ndiyo ya muhimu zaidi, imekuwa na mtazamo finyu kuhusu sekta ndogo hii muhimu hatua ambayo itaweka msingi mbovu kama taifa.

“Kwa ujumla sera hii haiwezi kuwa jibu kamili kwa kuwa tulipaswa kuandaa kwanza sera ya sekta pana ya mafuta na nishati kabla ya na kutokana na sera hiyo ndipo sera ya sekta ndogo ya gesi ingeandaliwa,” alisema.

Aliongeza kuwa Sera ya Nishati ya mwaka 2013 na sheria zote zinazohusu utafutaji na uchimbaji wa mafuta za toka 1980 na zile za biashara ya mafuta, zote haziendani na mahitaji ya sasa.

Wiki iliyopita, serikali iliweka hadharani sera hiyo ya mwaka 2013. Miongoni mwa  mambo yanayoelezwa katika sera hiyo ni kuwa wakati kampuni za kigeni zitakuwa zinazalisha gesi kwa wingi zikiangalia soko la nje, serikali itahakikisha inakuwa na mgawanyo wa kutosha wa gesi kwenye kampuni hizo kama hatua madhubuti kuhakikisha nishati hiyo inatosheleza mahitaji ya ndani kabla ya kuuza nje.

Pia, imeeleza mapato yatokanayo na gesi yatumike kuwekeza katika uwekezaji endelevu ambao utaleta maendeleo endelevu hata kabla ya akiba ya rasilimali hiyo kuanza kupungua nchini.

Kadhalika, sera hiyo inaeleza kuwa rasilimali hiyo ni mali ya wananchi wa Tanzania na itasimamiwa kwa namna ambayo itainufaisha jamii hiyo.

Pia sera hiyo inasema kwa kuwa gesi asilia ni rasilimali ya taifa na ambayo Watanzania wanaweza kuitumia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji viwandani na majumbani,  serikali itahakikisha inaweka mifumo itakayohamasisha matumizi mapana ya gesi kwenye shughuli za uzalishaji mali kama njia ya kukuza uchumi wa wananchi wake.

Aidha, sera hiyo inasema serikali itahakikisha inahamasisha kuanzishwa kwa viwanda vingi vya ndani vya gesi asilia ambayo itatumika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa wananchi wa kawaida ili kukuza vipato vyao.

Vile vile, inaeleza bayana maendeleo ya miundombinu ya gesi kuanzia ya uzalishaji, usindikaji, uhifadhi, usafirishaji na usambazaji.
Inabainisha kuwa serikali itahamasisha uwekezaji kwenye miundombinu ya usindikaji ardhini na siyo baharini.

NDESAMBURO ATETEA WAZAWA

Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo, amesema hoja ya serikali kwamba wazawa hawana uwezo wa kununua vitalu vya gesi na mafuta kwa ajili ya uwekezaji, mantiki yake ni kulinda maslahi ya wawekezaji wa kigeni na kuua ari ya Watanzania kuwekeza.

Ndesamburo alisema hakuna ukweli kwamba wafanyabiashara wakubwa wa Tanzania akiwamo Mwenyekiti Mtendaji wa IPP ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TSPF), Dk. Reginald Mengi, Mohamed Dewji na wengineo wengi, hawana uwezo wa kufanya hivyo na badala yake uwezo wa kiuchumi unaotafsiriwa na Wizara ya Nishati na Madini ni ule unaolenga kumilikisha wageni rasilimali za nchi badala ya kuwawezesha wazawa kuumiliki uchumi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara mjini Moshi, alisema wafanyabiashara hao wanastahili kupewa haki ya kununua vitalu vya uvunaji wa gesi na mafuta kutokana na uwezo wao kiuchumi ambao unaonekana katika makundi ya jamii na taifa kwa ujumla.

“Mengi ni mtetezi wa Watanzania katika mambo mengi zaidi hata ya wanasiasa tuliochaguliwa na wananchi kwa kura, lakini kwa uwezo wake wa kiuchumi, wanaelezwa eti wafunge mikataba na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wakati hata wasipofanya hivyo bado Watanzania na hasa hawa wafanyabiashara wakubwa wana uwezo wa kuungana na kuvuna gesi au kuchimba mafuta kwa maslahi ya Watanzania wenzao,” alifafanua.

Alisema Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyetoa kauli ya kuwabeza Watanzania, ameshindwa kuelewa kuwa baadhi ya wawekezaji hao hao wa kigeni watatumia ardhi hii ya Tanzania kutafuta mitaji.

“Muhongo anasahau kuwa ni Serikali hii hii ya CCM ambayo mwaka 1998 ilimpa Chavda shamba kubwa la katani kule Tanga kwa maelezo kuwa ataliendeleza na badala yake akatumia hati za shamba lile kukopa mabilioni ya fedha benki  na kisha kuingia mitini…mimi nafikiri Waziri Muhongo alitakiwa awajengee Watanzania mazingira bora ya kuwekeza katika sekta hiyo kwa kutumia vitalu hivyo hivyo vya gesi kutafutia mitaji,” alisema Ndesamburo.

Alipoulizwa na wananchi iwapo kauli hiyo ya serikali inaashiria nini wakati huu taifa likivuna rasilimali zake; Ndesamburo alisema umma hautaki porojo za kuingia mkataba na TPDC kwa kuwa huko ni kulenga kuwabana mbavu wazawa ambao serikali haitaki wapewe vitalu vya uvunaji wa gesi na uchimbaji wa mafuta.

Alisema hoja ya Dk. Mengi ya kutaka wazawa wapewe kipaumbele, ni msingi wa mawazo unaoakisi mahitaji ya Watanzania wa kawaida na hasa ambao wamekuwa wakiwekeza hapa hapa nyumbani na faida yake ikaonekana kwa sababu matunda yao yanaliwa na Watanzania wote.

“Kuwakumbatia wawekezaji wa kigeni na kuwabeza wazawa ambao uchumi wao unaonekana wazi wazi, ni kukubali ukoloni kurudi kimya kimya.

Tatizo letu limebaki lile lile la kukubali maagizo ya mababa zetu waliopo Amerika na Asia ambao wanasigana kiuchumi na kiviwanda duniani.

Badala ya kuwabeza, kwanza Serikali ilitakiwa kukaa na wawekezaji hawa wa kizalendo na kujua uwezo wao na kisha kufanya tathmini kama hawawezi kuwekeza kwa asilimia 100 basi pajengwe mazingira ya kuwawezesha kuwekeza,” alifafanua.

Alisema anachokiona yeye kwa umri wake katika siasa za nchi ni viongozi kujenga kasumba kwamba mwekezaji ni lazima awe ni kutoka nje na kwamba wawekezaji wengi wa kigeni wamelifanya taifa hili kama shamba la bibi huku wakija bila mitaji na kuichuma hapa nchini, lakini serikali haioni haja ya kuwawezesha Watanzania.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment