Kauli ya Simba imekuja baada ya kuwepo kwa tetesi zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ana mpango wa kukihama chama na kumfuata Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Simba alisema hana mpango wa kukihama CCM kwa sababu amelelewa na kukulia ndani ya chama hicho.
“Mimi ni mwanachama wa CCM na pia ni mwenyekiti wa UWT, hivyo sina mpango wowote wa kukihama chama changu na kile kinachozungumzwa ni uzushi,” alisema.
“Nafahamu kwamba CCM ndiyo iliyowezesha watu kunifahamu, naringa, natamba kwa sababu ya CCM.” Alisema amejipanga kuongoza timu ya wanawake wenzake ili kuhakikisha wanampeleka Dk. John Magufuli Ikulu.“Tumevunja kambi zetu zote tumebaki na kambi moja tu ya tingatinga,”alisema.
Akizungumzia kuhusu kuhama kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alisema kila mtu anahama chama kwa sababu zake na kwamba yeye (Simba) hana sababu ya msingi ya kufanya hivyo.
“Slogan (kaulimbiu) yetu wanawake ni ‘wanawake jeshi kubwa, Magufuli ushindi ni lazima,” alisema.
Wakati huo huo, akifungua Baraza Kuu Maalum la UWT, Simba alisema wawakilishi watakaoshinda kwenye uchaguzi wanatakiwa kwenda kufanyakazi na si kwenda kufanya maonyesho ya mavazi bungeni.
Pia, aliwataka wajumbe wa Baraza la UWT kuchagua wawakilishi wanaojiamini na watakaozungumza na kuwatetea wanawake bungeni.
Baraza la UWT limeanza vikao vyake jana kwa ajili ya kuwachagua wawakilishi na wabunge wa viti maalum.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment