dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, September 9, 2015

Askofu Gwajima: Tatizo la Dk Slaa si Lowassa

Askofu Gwajima
Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alitumia takribani saa moja na dakika saba kujibu mashambulizi ya Dk Willibrod Slaa, akisema kilichomuondoa Chadema si uamuzi wa kumpa Edward Lowassa nafasi ya kugombea urais, bali mkewe Josephine Mushumbuzi.
Askofu Gwajima alisema hayo wakati Dk Slaa akiwa ameondoka nchini na familia yake kwenda nchi za Ulaya na Amerika, akisema kurudi kwake kutategemea mazingira.
Wiki iliyopita, Dk Slaa alimshambulia Askofu Gwajima akidai kuwa ni mshenga aliyefanikisha Lowassa kujiunga na Chadema na pia kumtuhumu kuwa alimhakikishia kuwa maaskofu 30 kati ya 34 wa Kanisa Katolini walilipwa kati ya Sh60 milioni na Sh300 milioni ili wamuunge mkono waziri huyo mkuu wa zamani.
Dk Slaa, ambaye mkutano wake na waandishi wa habari ulionyeshwa moja kwa moja na vituo vinne vya televisheni, pia alikanusha habari zilizokuwa zimeenea kuwa amewekwa mfukoni na mkewe na kwamba, ndiye aliyemfungia ndani tangu mchakato wa kumchukua Lowassa CCM ulipoanza.
Lakini jana, Askofu Gwajima mbali na kujibu tuhuma hizo, pia ‘alitega bomu’ aliposema kuwa iwapo Dk Slaa atajitokeza tena kuwashambulia viongozi hao wa kiroho, atazungumzia watu wanne alioenda kukutana nao Afrika Kusini na kile alichokiita kuwa ni “mzigo”.
Askofu Gwajima alisema kilichomuondoa Dk Slaa kwenye ulingo wa siasa ni shinikizo la Mushumbusi ambaye hakuupenda ujio wa Lowassa na badala yake alitaka Dk Slaa awanie urais ili aupate ‘u-first lady’.
“Dk Slaa ni muongo, nilimpenda na kumuheshimu lakini sasa kwangu huyu namuita muongo aliyekosea,” alisema.
Askofu Gwajima, ambaye wakati anazungumza alikuwa amezungukwa na mabaunsa waliokuwa wamesimama wakati wote, alisema ameamua kuweka wazi kila kitu kwa sababu anamfahamu Dk Slaa kwa kuwa yeye ndiye aliyempa hata walinzi wa nyumbani kwake pamoja na mpishi.
“Dk Slaa alipata vitisho mwaka 2010, kwa sababu ya ukweli wake, ndipo aliponiomba nimsaidie walinzi kwa sababu hakuamini walinzi wengine,” alisema huku akiwataja walinzi kuwa ni Edwin, Six, Colnely na Emmanuel na mpishi anayeitwa Maselina Mushi.
Akizungumza kwa kujiamini kwenye ukumbi wa Landmark uliofurika waumini wake, Askofu Gwajima alisema Julai 26 wakati Lowassa alipojiunga na Chadema, ndiyo siku ambayo Mushumbusi alimfukuza Dk Slaa kwenye nyumba yao kumshinikiza asikubali Lowassa kuingia chama hicho kikuu cha upinzani.
“Kwa sababu walinzi wangu ndiyo wanaomlinda walikuwapo wakati tukio hilo linatokea na walinipigia simu, wakanieleza kuwa Mushumbusi amemfukuza Dk Slaa ndani, amemtupia nguo nje na sasa amelala ndani ya gari,” alisema.
Baadaye, Gwajima alimuita mmoja wa walinzi hao, aliyemtambulisha kwa jina la Colnely William ambaye alisimulia tukio la Dk Slaa kulala ndani ya gari.
William, ambaye anadai alikuwa zamu kwa Dk Slaa siku hiyo, alisema baada ya kurejea nyumbani saa 6.30 usiku, ndipo mwanamke huyo alipogoma kumfungulia mlango na kutupa nguo za mwanasiasa huyo nje.
“Nilimsikia Mushumbusi akimwambia ‘Dk rudi unakotoka, kama utarudi Chadema sikutaki nyumbani’ na kumlazimisha aandike barua ya kujiuzulu,” alisema.
Meseji ya Dk Slaa
Baadaye, Gwajima alitoa simu yake ya mkononi na kuonyesha ujumbe mfupi aliodai alitumiwa na Dk Slaa ambao umeandikwa “binti yako amekataa, kuanzia leo nastaafu siasa”.
“Kwa ushahidi huu, ni uongo kusema kuwa Dk Slaa amestaafu siasa kwa sababu ya Lowassa, ni uongo,” alisema Gwajima.
Kadhalika, Gwajima alisema alijitahidi kuzungumza na Mushumbusi ili kumshawishi amruhusu Dk Slaa aendelee na siasa ndani ya Chadema, lakini hakufanikiwa na hata jitihada nyingine zilizofanywa na Philemon Ndesamburo na Askofu Zacharia Kakobe, hazikuzaa matunda.
Alisema mazungumzo hayo yote na mke huyo wa Dk Slaa ameyarekodi.
 Akiri kuwa mshenga
Askofu huyo alikiri kutumika wakati wa kumuingiza Lowassa ndani ya Chadema kwa kuwa ni rafiki wa Lowassa tangu akiwa CCM, lakini aliyeanzisha mchakato ni Dk Slaa.
“Neno la Mungu linasema, heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu. Mimi sikusimama pale kwa sababu ni bora kuliko wengine, bali kwa sababu nilikuwa mtu sahihi wakati ule,” alisema.
Kuhusu tuhuma kuwa maaskofu wa Kanisa Katoliki walipewa rushwa, Askofu Gwajima alikanusha kumwambia Dk Slaa kuwa maaskofu 30 kati ya 34 walipewa kati ya Sh60 milioni na Sh300 milioni ili wawe upande wa Lowassa, akisema kauli hiyo ya Dk Slaa inawatukanisha viongozi hao wa kiroho.
Alisema anashangazwa kuwa Idara ya Usalama wa Taifa inampa ulinzi Dk Slaa kwenda vituo vya televisheni kwa ajili ya kutukana viongozi wa dini, akisema iwapo ataendelea kufanya hivyo, atalipua bomu zito zaidi la katibu huyo wa zamani wa Chadema. “Usalama wa Taifa si kwa ajili ya mtu mmoja, au kikundi cha watu, ni kwa ajili yetu sote,” alisema Gwajima.
“Wakati huu, Usalama wa Taifa wanatakiwa wakae kati. Kama Lowassa akishinda waende naye, kama ni Magufuli, waende naye.”
Hata hivyo kila raia ana haki ya kulindwa na vyombo vya dola ikithibitika dhahiri kuwa anatishwa.
Wakati huohuo, Dk Slaa ameaga wananchi akisema anakwenda nje ya nchi kuishi na anaweza kurejea wakati wowote kutegemeana na mazingira.
Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyorushwa jana asubuhi na Televisheni ya Azam, Dk Slaa alisema: “Ninakwenda na nitarudi, mtu ambaye anatoroka harudi nchini. Nataka wananchi wajue kuwa nitarudi kwa hiyo kama kuna hoja zozote, zitajibiwa tu kwa sababu ninarudi hapa ni kwetu sina mahala pengine pa kuzikwa.”

No comments :

Post a Comment