dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, September 7, 2015

Magufuli na ufisadi, waasisi wakionea aibu!

Image result for magufuli
  • Matumizi ya muda, anaenda moja kwa moja kwenye hoja, hana porojo
  • Utendaji wake amiwa waziri wambeba
  • Mbeya wavutiwa na msimamo wake kuhusu ufisadi
“SIMMONILE ndiye mtawala mkuu (paramount chief) wa jamii ya kabila la Wanyakyusa, katika kizazi cha leo amekuwa maarufu kwa jina la Mwakyembe!”

WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiipa kisogo ajenda ya ufisadi, iliyowabeba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hivi sasa ndiyo yenye kumbeba mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.

Dk. Magufuli, akiwa wilayani Kyela alitunukiwa heshima ya mtawala mkuu (paramount chief) wa jamii ya kabila la Wanyakyusa wilayani humo na kupewa jina la Simmonile. Katika kizazi cha sasa cha mtawala huyo, limetawala zaidi jina lake la Mwakyembe, likitumika kama jina la ukoo wa kizazi chake cha sasa.

Msingi wa kupewa heshima hiyo ni imani waliyonayo wananchi hao kwa mgombea huyo, ambao kwa hulka yao ni watu wenye misimamo na wenye kusimamia kile wanachokiamini kuwa ndio ukweli, wanamuona Magufuli kuwa kiongozi mwenye kusimamia kile anachokiamini kuwa ni kweli na haki.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Livingston Mwakipesile, alimwelezea mgombea huyo kama kiongozi mwadilifu sana, mtu makini, mnyenyekevu, mchapa kazi na sio fisadi.
Lakini kubwa lililowavutia wengi kuhusu Mzee Mwakipesile ni pale alipotoa ya moyoni akisema; “Katika miaka kumi, leo ndio nimecheka, leo nimefurahi sana, tunataka kukuhakikishia, Kyela imekaa vizuri, wewe ni Rais, tunakupa kijana wetu, Dk. Harrison Mwakyembe.”

Hatua ya Dk. Magufuli kuizungumzia ajenda hiyo katika mikutano yake ya kampeni hivi karibuni akiwa mkoani Mbeya, ilionekana kuwavutia zaidi wananchi mkoani humo. Lakini lililoteka hisia za hadhara yake zaidi ni msimamo wake wa kuanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi na wahujumu wa uchumi wa nchi.

Ajenda ya vita dhidi ya ufisadi ndiyo iliyokibeba Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambapo mgombea wake, Dk. Wallbrod Slaa alifahamika kama kinara wa vita dhidi ya ufisadi na kukipa heshima kubwa chama chake akikivika joho la uadilifu.

Hatua ya wananchi kuvutiwa zaidi na mgombea mwenye msimamo wa kuwashughulikia mafisadi, wabadhirifu wa mali za umma na wahujumu uchumi, inaelezwa kuwa ujumbe uliojitosheleza kwa viongozi wa kisiasa nchini, kwamba wananchi wamechoshwa vitendo hivyo, kwa kuelewa fika kuwa ndiyo kiini cha umasikini wao.

Pamoja na msimamo huo wa kuunda mahakama maalumu kwa ajili ya mafisadi na wezi, wananchi walivutiwa pia na msimamo wake kuhusu viwanda, ambapo anabainisha kuwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa na kutoendelezwa kama ilivyo mikataba yake, basi vitarudishwa haraka.

Kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya, bado wanayo kumbukumbu mbaya kuhusu viwanda vya Highland Soap (HISOAP), Zana za Kilimo (ZZK) na kiwanda cha nguo Mbeya, ambavyo vilitengeneza ajira na kuzalisha bidhaa zilizokuwa na mchango mkubwa katika maisha ya wananchi mkoani humo.

Pamoja na kubinafsishwa, viwanda hivyo hivi sasa havizalishi tena bidhaa ilizokuwa vikizalisha awali na baadhi kugeuzwa kuwa maghala ya bidhaa waliovinunua.


Mbali ya ufisadi, akiwa jijini Mbeya mgombea huyo alikoga nyoyo za umati uliohudhuria mkutano huo kwa kuzungumzia suala la barabara kuu ipitayo katikati ya jiji hilo ikielekea nchini Zambia, ambapo aliwaahidi wakazi wake kuwa itapanuliwa ili iwe ya njia nne.

Barabara Kuu hiyo, ndiyo yenye kutumiwa pia na magari yaendayo nchi jirani za Kusini na Kusini Magharibi ya Afrika, na katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na msongamano mkubwa wa magari kutokana na kuzidiwa na wingi wa magari, mengi yakiwa yale makubwa ya mizigo yaendayo nje ya nchi.

Wasemavyo wakazi wa Mbeya

Makamu Rais wa TCCIA, Biashara, Julius Kaijage, anaitazama misimamo ya mgombea huyo kuhusu ufisadi na uwajibikaji kuwa ndilo suluhisho la matatizo ya kiuchumi yanayolikabili taifa kwa miaka mingi sasa, hivyo, kwa mtazamo wake mgombea mwenye dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko lazima awe niyule mwenye kuuchukia ufisadi kutoka ndani ya nafsi yake, na siye yule mwenye kuonea aibu.

“Tatizo la nchi hii sio sera au ilaani, tatizo hapa ni utekelezaji na usimamizi wa karibu wa utekelezaji huo,” anasema Kaijage.

Mwenyekiti wa APPT Maendeleo Mkoa wa Mbeya, Godfrey Mwandulusya anamuangalia mgombea huyo wa CCCM, tofauti na hata wanachama wa chama hicho wanavyomuangalia, kwamba msimamo wake unakibeba zaidi chama hicho kilichopoteza mvuto kwa wananchi, hususani vijana.

“Magufuli anajitahidi kurudisha imani ya umma juu ya chama chake,” anasema Mwandulusya katika mazungumzo yake na Raia Mwema.

Pamoja na kukibeba chama chake, Mwenyekiti huyo wa APPT Maendeleo anabainisha kuwa msimamo wake dhidi ya ufisadi, unamtofautisha na wanasiasa wengine wenye kuionea aibu ajenda hiyo ambayo wananchi walio wengi wanaionakuwa ndilo tatizo la msingi la taifa hili.

“Anajenga imani kwa wananchi, anajiweka mbali na wale waliohusika na kutuhumiwa ufisadi, lakini zaidi kwa mkakati huu anakiri uongozi ni tatizo kichama na kiserikali, ajenda yake ikitekelezwa itakisaidia chama chake kuendelea kuaminiwa.”

Baadhiya wachambuzi wa siasa jijini Mbeya wanauangalia msimamo wa mgombea huyo na athari zake kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakibainisha kuwa vyama hivyo vimepoteza imani kwa Watanzania makini.

“Ni dhahiri viongozi hao ni wachumia tumbo kwa kivuli cha siasa,kukimbia kwa Dk Slaa na Profesa Lipumba ni anguko kwa Ukawa, pia kukumbatia mafisadi ni dhahiri wameuza vyama,” anasema mchambuzi mmoja wa siasa za Mbeya, ambaye hata hivyo aliomba kutotajwa jina.

Ajenda ya ufisadi ndiyo inayobeba taswira ya kampeni za Magufuli ambapo wasemaji wake wote huibeba wasimamapo jukwaani kuzungumza.

Richmond bado ya moto

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza kashfa ya Richmond Dk. Harrison Mwakyembe, alivunja ukimya pale alipoizungumzia kwenye mikutano ya kampeni ya mgombea huyo wa CCM mkoani humo akionya kuwa hatonyamaza pale wahusika wa kadhia hiyo watakapojitokeza na kujisafisha kwenye mikutano ya kampeni zao za urais.

“wazalendo wa nchi hatutaruhusu watu wote waliodokoa mboga jikoni waingine Ikulu,” alisema Dk Mwakyembe akiwalenga wale wote waliohusikana ufisadi.

Miongoni mwa utetezi unaotumiwa hivi sasa na watetezi wa aliyekuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu kwa kashfa hiyo ya Richmond, Edward Lowasa, ni ule unaohoji kwa nini hajafikishwa mahakamani iwapo kweli alihusika na kashfa hiyo. Akitolea ufafanuzi utetezi huo, Dk. Mwakyembe alisema; “Kesi zote za jinai hazina ukomo, unashitakiwa wakati wowote.”

Pasipo kutaja jina, Waziri huyo wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisisitiza kuwa walichokisema bungeni, kwamba mzee hafai mpaka leo kinasimama, na kwamba walisimamia ukweli na wataendelea kuusimamia.

Hatua ya Dk. Mwakyembe kulitolea ufafanuzi suala hilo imekuja kutokana na hatua ya baadhi ya viongozi wa Ukawa, ambao ndio waasisi wa kashfa dhidi ya mgombea wao, Lowasa, kumsafisha wakidai aliwajibika kuipusha mamlaka ya juu na kashfa hiyo, wakati mjadala huo ulishafungwa na Bunge.

Kwa mujibu wa bingwa huyo wa sheria, iwapo wahusika watahitaji kujisafisha basi liombwe Bunge kufungua mjadala upya, vinginevyo wakiendelea, nao hawatakuwa na namna nyingine zaidi ya kutokahadharani na kuanika kila kitu.

Mjadala kuhusu kashfa hiyo uliendelea katika maeneo mbali mbali jijini Mbeya, huku baadhi ya wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa wakionekana wazi kumizwa na msimamo wa Dk Mwakyembe kuhusu sakata hilo, huku baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa jijini humo wakikubaliana naye juu ya kufanyika mjadala wa wazi iwapo kweli watetezi wa mgombea huyo wa Ukawa na yeye mwenyewe ni wakweli.

Hata hivyo, tofauti na ilivyosubiriwa kwa hamu na wananchi wengi, kumsikia mhusika huyo mkuu akilizungumzia suala hilo, mgombeahuyo wa Ukawa, kwa mara nyingine tena, alishindwa kulizungumzia katika uzinduzi wa kampeni zao pale Jangwani, Jumamosi iliyopita.

Mzungumzaji mwingine katika ule mkutano wa chama hicho uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Luanda Nzovywe, alikuwa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ambaye naye alielekeza mashambulizi yake kwa wanasiasa wenye kuhusishwa na kashfa za ufisadi, ikiwemo matumizi makubwa ya fedha ambazo vyanzo vyake havieleweki.

Nchemba alitahadharisha kuhusu uwepo wa wagombea ambao wanabembwa na watu aliowaita wapiga dili, kwa maana ya wafanyabiashara wenye malengo ya kuja kunufaika na ushindi wa mgombea huyo.

Anautaja uhalifu nyuma ya watu hao kuwa nipamoja na ukwepaji kulipa kodi hivyo kuwaachia mzigo wote wa kodi Watanzania wenye vipato vidogo pamoja na kupata mikataba ya kinyonyaji kutokana na kiongozi huyo atalazimika kulipa fadhila kwa waliomwingiza madarakani.

“Pelekeni mtu asiyedaiwa ili awatumikie, mkipeleka wapiga dili, watawatumikia wapiga dili waliowaingiza pale Ikulu,” alisema Nchemba.

Magufuli kapita tayari, akiwafanikiwa kuzungukia wilaya zote kwa gari, wanachokisubiri sasa wananchi mkoani humo ni ujio wa mgombea huyo wa Ukawa. Hata hivyo, haijafahamika iwapo atarudi tena mkoani humo.

No comments :

Post a Comment