Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli
Musoma. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesema iwapo atachaguliwa kuingia Ikulu, atahakikisha nchi inapata mgao halali kutokana na uwekezaji kwenye rasilimali zilizopo.
Akizungumza uwanja wa Mkendo, mjini Musoma, Mara leo jioni, mgombea huyo amesema kuwa kuna wawekezaji ambao wameifanya nchi kama sehemu ya kuchuma tu, hivyo atapambana nao.
“Tunahitaji wawekezaji wote kutoka ndani na nje ya nchi lakini nitahakikisha madini, mbuga na rasilimali nyingine zinasaidia kuinua maisha ya Watanzania. Kuna wawekezaji wameifanya nchi kuwa shamba la bibi,wengine hawawi wawazi,” amesema mwanasiasa huyo.
Amesema, kwa kupambana na mafisadi ndani ya serikali na kuwabana wawekezaji, nchi itakuwa katika nafasi nzuri ya kugharamia elimu bure kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha nne nchi nzima pamoja na kuboresha utoaji wa huduma bora za afya.
Amewaahidi wananchi wa Musoma kuwa atahakikisha anaboresha barabara na mradi wa maji Musoma wa Sh44bn ambao kwa sasa umesimama.
“Kama nimeweza kusimamia miradi ya barabara na madaraja ya thamani ya sh9.5 trilioni, nitashindwa mradi wa maji wa sh44 bilioni?” amehoji Dk. Magufuli na kuahidi kuhakikisha mradi huo unaendelea kujengwa na kumalizika ndani ya miezi mitatu ya utawala wake.
Ameahidi kuinua viwanda vya samaki na nguo na nyama, sekta ambazo anaamini zitaongeza ajira kwa wingi na kuinua maisha ya wakazi hao.
No comments :
Post a Comment