dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, October 15, 2015

Nyerere na msimamo wa demokrasia katika uchaguzi!


Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo wa kuona mbali, hata alipopingwa baadaye waliompinga walikiri ukweli wa maono yake.
By Pius Msekwa
Ni dhahiri kwamba Mwalimu Nyerere anakumbukwa kwa mambo mengi ya msingi aliyoyapa kipaumbele wakati wa uongozi wake.  Jambo mojawapo alilisema Julai 29 Julai, 1985, kwamba: “Kazi iliyokuwa muhimu kuliko zote kwangu mimi, ilikuwa ni kujenga Taifa lenye umoja kwa msingi wa heshima na usawa wa binadamu”.
Lakini yapo mambo mengine mengi ya uongozi wake ambayo tunapaswa kuyakumbuka na kuyaenzi , hususan suala la uadilifu katika uongozi (au maadili ya uongozi), Azimio la Arusha, miiko ya uongozi,  mapambano yake dhidi  ya rushwa,  ufisadi na mengineyo.
Pamoja na hayo  kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, nimeona ni vyema nitoe mchango wangu kwa kukumbusha juu ya msimamo wake thabiti juu ya umuhimu wa demokrasia katika uchaguzi wa viongozi wetu.
Wosia wake kuhusu makosa yanayopaswa kuepukwa  wakati wa uchaguzi:
Katika kitabu chake alichokiandika mwaka 1962 kinachoitwa “Tujisahihishe”,  Mwalimu Nyerere aliorodhesha makosa ambayo alisema yanatokana na ubinafsi na akawaasa Watanzania wajiepushe na makosa hayo.
Alisema: “Kosa jingine linalotokana na ubinafsi tunalifanya wakati wa kuchagua viongozi. Wakati mwingine hufanywa na wanachama, wakati mwingine hufanywa na viongozi wenyewe. Viongozi wetu hawana budi watokane na watu, bila hila, vitisho, rushwa, au ujanja wa aina yoyote. Lakini mara nyingi wanachama huchagua viongozi bila kufikiri kwa makini kama viongozi hao wanaiweza, au hawaiwezi, ile kazi wanayochaguliwa kuifanya…’’
Mwalimu Nyerere alivyopigania demokrasia katika uchaguzi:
Enzi za ukoloni, utawala wa kikoloni ulipanga kwamba uchaguzi mkuu wa kwanza wa wajumbe wa baraza la kutunga sheria ufanyike  Septemba mwaka 1958. Katika kufanya maandalizi ya uchaguzi huo, utawala huo ulitunga sheria mahsusi, ambayo ilikiuka kabisa misingi ya demokrasia katika uchaguzi, kwa lengo eti la kujihakikishia kwamba Wazungu na Wahindi wanaingia katika baraza hilo kwa idadi iliyo sawa na Waafirika (ambao walikuwa ni wengi zaidi).
Sheria hiyo lijulikana kama “sheria ya kura tatu”, ambapo kila mpiga kura aliwekewa sharti kwamba ili kura yake iweze kuwa halali, lazima apige kura tatu kwa pamoja, yaani kura moja kwa mgombea Mzungu, kura ya pili kwa mgombea Mhindi au Singasinga na kura ya tatu kwa mgombea Mwafrika.
Demokrasia katika uchaguzi inataka kila mpiga kura awe na kura moja tu, ambayo atampigia mgombea yeyote yule atakayemuona yeye kuwa anafaa.
Kwa hiyo hili suala lakulazimisha kura tatu lilikuwa linakiuka msingi huo wa demokrasia. Kwa sababu hiyo, wanachama na  viongozi wengi wa TANU, waliipinga sheria hiyo kwa nguvu, na wakapanga kususia uchaguzi wenyewe, wakidhani kuwa njia hiyo ingeweza kuulazimisha utawala wa kikoloni kusikiliza madai yao ya kutaka sheria hiyo ifutwe.
Kumbe Mwalimu Nyerere alikuwa ‘kiona mbali’ zaidi kuliko wenzake wengi. Alitambua kuwa kususia uchaguzi kutawanyima Waafirika fursa ya kuingia kwenye Baraza la Kutunga Sheria na kwamba Wakoloni watatumia mwanya huo kupitisha sheria nyingine za kuchelewesha uhuru wa Tanganyika, kwa kisingizio kwamba kitendo chao cha kususia uchaguzi kinadhihirisha kwamba Waafrika hawajawa tayari kujitawala wenyewe.
Ndipo wajumbe walipokwenda kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa TANU uliofanyika Tabora mwezi Januari 1958, wakiwa wamejiandaa kupitisha azimio kali la kususia uchaguzi huo wa kura tatu.  Kwa upande wake, Mwalimu Nyerere naye alienda kwenye mkutano huo akiwa amejiandaa kujaribu kuwashawishi wajumbe wenzake wakubali kushiriki katika uchaguzi huo. Katika hali hiyo, kwa hakika alikuwa na kazi ngumu  mbele yake.
Lakini kwa kutumia vipaji vyake vya uwezo mkubwa wa kushawishi alivyokuwa amejaliwa na Mwenyezi Mungu, alifanikiwa kufanya hivyo;  na mkutano huo ukatoka na azimio  la kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Lakini ilikuwa kazi ngumu, kwani  aliyekuwa Katibu Mkuu wa TANU, Zuberi Mtemvu, hakuridhika na uamuzi huo, akajitoa kwenye TANU na kuunda chama chake kipya cha African National Congress (ANC).
Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi huo yalithibisha busara za Mwalimu Nyerere, kwani kutokana  na mkakati ambao Mwalimu Nyerere aliubuni wa kusimamisha wagombea Wazungu na Wahindi ambao walikuwa  wakiunga mkono juhudi za TANU za kudai uhuru, Chama cha TANU kilifanikiwa kushinda katika majimbo yote 10 yaliyokuwapo ya uchaguzi, na wagombea wake walipita bila kupingwa katika majimbo mengi.
Mfano mwingine wa kupigania uchaguzi wa kidemokrasia
  Uchaguzi huo wa kwanza ulifuatiwa na uchaguzi wa pili, ambao ulipangwa kufanyika Septemba mwaka 1960.  Katika uchaguzi huo wa pili, sheria ya kura tatu ilikwisha kufutwa, na idadi ya majimbo iliongezwa hadi kufikia 71.
Matokeo ya uchaguzi huo wa pili yalikuwa ni kwamba wagombea wa TANU walipita bila kupingwa katika majimbo 58 miongoni mwa hayo 71, na katika yale majimbo mengine 13 ambayo yalikuwa na ushindani, wagombea wa TANU walishinda katika majimbo yote, (mmoja wao akiwa ni mwananchama wa TANU aliyekuwa amejisimamisha kama mgombea binafsi).
Wagombea wanapopita bila kupingwa, maana yake ni kwamba hakuna uchaguzi unaofanyika katika majimbo husika. Maana yake nyingine ni kwamba wapiga kura wa majimbo hayo wananyimwa haki yao ya msingi ya kupiga kura. Ni dhahiri kwamba hali hii ya kunyima watu fursa ya kupiga kura, inadidimiza demokrasia katika uchaguzi.
Mwalimu Nyerere alitambua hivyo, na alitambua vile vile kwamba hali hiyo inasababishwa na vyama  vingine kutosimamisha wagombea wao, wakiogopa kupoteza muda wao huku wakijua kwamba kutokana na nguvu ya upendo kwaTANU ilivyokuwa kubwa , walijua kwamba hapakuwa na uwezekano wa kuwashinda wagombea wake.
 Kwa hiyo, ili kurejesha demokrasia ya ushindani katika uchaguzi, Mwalimu Nyerere alianza mchakato wa kutunga Katiba mpya ya mfumo wa chama kimoja cha siasa, ambayo ingewezesha wanachama wake kushindanishwa katika uchaguzi, na kwa hiyo kuwapatia wapiga kura fursa ya kutumia haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wao. 
Pius Msekwa ni kada mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika chama, Bunge na Serikali
/Mwananchi.

No comments :

Post a Comment