dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, October 15, 2015

Oktoba 25 inaweza kubadili historia ya Tanzania?


Wananchi wakiwa katika foleni ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2010, visiwani Zanzibar ambapo CCM ilishinda. Picha ya Maktaba
By Julius Mathias, Mwananchi
Oktoba 25, inaweza kuwa ndiyo siku muhimu kuliko zote mwaka huu kwa Watanzania. Hiyo inatokana na ukweli kwamba ni siku ambayo wananchi 22.75 milioni wanatarajiwa kupiga kura kuchagua viongozi watakaoiongoza nchi yetu kwa miaka mitano ijayo. Si ajabu kwamba kila Mtanzania anajua umuhimu wa Oktoba 25 ingawa wapo wanaojua zaidi. Wachambuzi wa mambo wanabashiri uwezekano wa kubadilisha historia ya nchi ya Tanzania kwa kupata kiongozi kutoka chama mbadala, mbali na CCM kinachotawala sasa.   
Hata hivyo, zipo kumbukumbu zinazoonyesha mustakabali wa baadhi ya nchi ulibadilika baada ya uchaguzi mkuu wa kidemokrasia.
Wapo viongozi mashuhuri duniani wanaoendelea kukumbukwa kutokana na matukio ya vurugu waliyofanya baada ya uchaguzi kwenye mataifa yao.
 Hata hivyo, dalili zinaonyesha uchaguzi wa mwaka huu utakaokuwa wa 14 tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa vyama vingi kabla na baada ya uhuru utakuwa na ushindani mkubwa.
Historia ya uchaguzi
Kumbukumbu zinaonyesha uchaguzi wa vyama vingi umewahi kufanywa mara tatu katika awamu tofauti enzi za Tanganyika, mbili  kati ya hizo zikifanyika kabla ya uhuru, yaani mwaka 1958 na 1960  na wa tatu ulifanyika Novemba Mosi mwaka 1962, baada ya uhuru  na kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Baada ya hapo ilipita miongo mitatu ya utawala wa chama kimoja iliyoshuhudia chaguzi sita; mwaka 1965, 1970, 1975, 1980, 1985 na ule wa 1990.
Mfumo wa vyama vingi ulirejeshwa mwaka 1992 na kwa kipindi hicho chote, uchaguzi mkuu umefanyika mara nne zilizoendeshwa kwa utulivu na amani; mihula miwili ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin William Mkapa (1995- 2005) na miwili mingine ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete (2005-2015) ikiwa awamu ya nne.
Nguvu ya NEC
Historia hiyo ya mafanikio kwenye uchaguzi, inaipa nguvu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuamini hata mwaka huu hakuna litakalo haribika, bali historia itaendelea kutunzwa ili ulimwengu uendelee kujifunza kutoka Tanzania.
 Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva analithibitisha hilo kwa wadau wote waliokutana na taasisi hiyo nyeti katika maandalizi ya siku uchaguzi mkuu inayosubiriwa na Watanzania 22, 782, 558 wanaotarajiwa kupiga kura.
Ili kuwaandaa wapiga kura kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa amani na utulivu kwa wiki mbili mfululizo, NEC imefanya mazungumzo na makundi yote yanayowakilisha jamii. Ilianza na viongozi wa dini; maaskofu na masheikh wakafuata wawakilishi wa walemavu kisha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT).
Wahariri wa vyombo vyote vya habari nchini chini ya jukwaa lao (TEF), pia vijana na wanawake, mmoja kutoka kila mkoa wakiwakilisha asasi zinazohusika na makundi hayo ili wafikishe elimu stahiki kupitia taasisi zao.
Kundi la mwisho lilikuwa viongozi wote wa vyama vya siasa 22 vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Ni kundi muhimu zaidi ambalo kero zake ni lazima zisikilizwe na kutatuliwa kwa wakati kwani ndilo linaloweza kuamua uchaguzi huu uweje; wa amani au vurugu.
NEC pia ilikutana na wataalamu wa Tehama wa vyama vya siasa na waangalizi wa kimataifa, waliotanguliwa na kundi la waratibu (30) na wasimamizi (972) wa uchaguzi kutoka halmashauri zote  nchini na makamanda wa polisi kutoka mikoa na kanda maalumu zilizopo nchini.
NEC inawaagiza wajumbe wa mkutano huo kutenda haki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu ikikumbusha dhamana ya usalama wa taifa iliyo mikononi mwao na kutahadharisha kwamba kosa lolote linaweza kuliingiza taifa kwenye matatizo na kumtaka kila mmoja kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Jaji Lubuva anatoa rai hiyo huku akielezea falsafa ya uchaguzi ya Jonas Savimbi, aliyekuwa kiongozi wa vita vya msituni wa nchini Angola ambaye alifariki Februari 22, 2002.
Anasema: “Mwandishi mmoja wa vitabu anaielezea vizuri falsafa ya uchaguzi ya Savimbi; kiongozi huyo aliamini kuwa yeyote anayeshiriki uchaguzi ni lazima ashinde na asiposhinda basi ameibiwa kura. Hivyo hatakiwi kukubali matokeo, badala yake anatakiwa apambane kuhakikisha anashinda.”
Kwa miaka 27, Jonas Malheiro Savimbi aliendesha mapambano ya msituni dhidi ya Serikali ya Angola. Alianza kwa kujiunga na chama cha wapigania uhuru wa MPLA mwaka 1964, muda mfupi baadaye akajiunga na chama cha FNLA. Miaka miwili baadaye, 1966, alianzisha vuguvugu la Unita zikiwa harakati ya kuikomboa Angola kutoka ukoloni wa Ureno.
Lubuva anasema hakuna anayetarajia kuona falsafa ya Savimbi inatumika nchini baada ya Oktoba 25 kwani wadau wote walioshirikishwa wametoa uzoefu wao na kubainisha changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi kwa wakati kabla ya upigaji kura.
Pia wenye majukumu wameelezwa cha kufanya; kabla, wakati na baada ya mchakato huo. Kwa maandalizi hayo, kila mdau anatarajiwa kutosheka na kilichofanywa.
Waratibu, wasimamizi na polisi
Licha ya kuwakutanisha pamoja na kubadilishana uzoefu, NEC ilikabidhi mamlaka ya kutenda haki kwa wagombea ubunge na udiwani kwa Wakurugenzi wa Halmashuri husika chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi ikiwataka watumie weledi kuwahudumia wateja wao baada ya upigaji kura kufanyika.
Mwenyekiti wa NEC anawaasa watendaji hao kushirikiana kwa kila changamoto itakayojitokeza na kuitatua bila kusababisha madhara kwa jamii inayowazunguka na wafanye hivyo bila upendeleo.
“Hii ni mara ya kwanza kwa NEC kuwakutanisha watendaji na makamanda wa polisi kabla ya uchaguzi mkuu. Awali tulikuwa tunakutana na kila kundi kwa wakati wake. Leo tutapeana taratibu zote muhimu za uchaguzi kuanzia upigaji, kuhesabu, ujumlishaji wa kura mpaka utangazaji wa matokeo. Tutumie mkutano huu kujifunza makosa yote yaliyotokea kwenye chaguzi zilizopita.
Kumbukeni, kosa moja dogo linaweza kuleta uvunjifu wa amani kwenye maeneo yenu na hata kuliingiza taifa kwenye matatizo. Hivyo, fanyeni kazi kwa weledi, uadilifu na fuateni sheria, kanuni na taratibu za NEC,” anasema Jaji Lubuva.
Kiongozi huyo pia anabainisha mkakati wa tume yake kuufanya uchaguzi kuwa wa haki, huru na kuaminika zaidi akimtaka  kila mmoja kuzingatia maelekezo na makubaliano, wakiwamo mawakala wa vyama vya siasa.
 “Uzoefu wa chaguzi zilizopita na taarifa tulizonazo, kuna vikundi vya vijana wanaohusishwa na vyama vya siasa wanaowatisha wapigakura, hasa kina mama ili wasishiriki mchakato huu. Ni rai yangu mhakikishe hilo halijitokezi na Watanzania wote watapata haki yao ya kikatiba. Baada ya kupiga kura, endapo kutakuwa na ulazima watu wasimame zaidi ya mita 200 kutoka kituoni, vinginevyo warudi makwao wakasubiri kutangazwa kwa matokeo,” anahimiza Lubuva.
Kukiwa na wajumbe wote saba wa NEC, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Diwani Athumani, Mkuu wa Oparesheni wa Polisi, Paul Chagonja, Mkuu wa Polisi Jamii, Mussa Alli Mussa na Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na baadhi ya wakuu wa vikosi, watendaji hao waliaswa kuchukua tahadhari na kuepusha aina yoyote ya uvunjifu wa amani unaoweza kusababishwa na maamuzi yao. Kwa upande wake, IGP Mangu anaahidi jeshi lake litatumia busara kuendeleza utulivu uliopo na kuhitimisha mchakato wa uchaguzi kwa amani, huku akibainisha changamoto za kiusalama zilizopo mwaka huu.
Anaitaja ya kuwaweka watu umbali wa mita 200 kutoka kilipo kituo cha kupigia kura, akisema inahitaji busara kwa sababu vingi vipo karibu na makazi ya watu, hivyo askari wake watalazimika kuwa makini ili kutovunja haki wakati wakisimamia sheria hiyo.
“Mazingira ya kidemokrasia yamebadilika sana nchini. Ni tofauti na mwaka 2010 au kabla ya hapo, ndiyo maana hata matumizi ya nguvu yamepungua mwaka huu. Mara nyingi tunasikilizana na wanasiasa…kwa hali hiyo nguvu haijahitajika katika mikutano mingi ya kampeni zinazoendelea,” anasema Mangu.
Wanawake
Jaji Lubuva pia anawaambia wawakilishi wa wanawake kuwa NEC inatambua mchango wa asasi za kiraia zinazowakilisha wanawake katika kufanikisha uchaguzi nchini.
Anasema anatambua ushawishi, taaluma, vipaji na ujuzi walionao katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na uchaguzi.
“Tutahakikisha mchakato huu unafanyika kwa uwazi, uhuru na haki zaidi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kujenga demokrasia ya kweli na kuimarisha utawala bora,” anasema Lubuva.
Wawakilishi hao wanapewa jukumu la kufikisha elimu kwa jamii kwamba siku ya uchaguzi, vikongwe, wajawazito na wenye watoto wachanga hawapaswi kupanga foleni.
Wahariri
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Kailima Kombwey anaeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya NEC na wahariri wa vyombo vya habari, pia wadau wote wa habari akiwakumbusha kujiridhisha kwa kupata taarifa sahihi kabla ya kupeleka habari zao kwa wananchi.
Anasema: “Pamoja na umuhimu huo, mna jukumu kubwa la kuhakikisha habari mnazozitoa zinalenga kujenga amani ya nchi na kuepuka kutojiingiza katika ushabiki wa kisiasa kwa kusahau misingi ya uandishi wa habari.
Nchi nyingi zimeingia katika machafuko, hasa wakati wa uchaguzi kutokana na ushawishi wa vyombo vya habari, hasa pale kwa makusudi vinapoamua kuandika habari za uchochezi na ushabiki, badala ya mambo ya msingi ya sera na ilani za vyama pamoja na masuala ya maendeleo. ”
Wenye Ulemavu
Mbele ya wawakilishi wa watu wenye ulemavu tume inajinasibu kuhakikisha kila raia mwenye sifa anapiga kura, wakiwamo watu wenye ulemavu. Jaji Lubuva anasema tume yake inatambua watu hao wanahitaji msaada wawapo kwenye vituo vya kupigia kura.  Anasema kwa kuzingatia hilo imetoa maelekezo kwa wasimamizi wa vituo namna ya kuwahudumia.
“Watu wanaoishi na ulemavu watapewa nafasi ya upendeleo kuingia na kupiga kura pasipo kusimama katika mstari kwa muda mrefu. Kwa kushauriana na wawakilishi wa walemavu wasioona tumeamua kutumia kifaa maalumu cha “Tactile Ballot Folder” ili waweze kupiga kura wenyewe bila ya kusaidiwa na mtu, hivyo kutimiza lengo la usiri wa kura,” anasema.
Vijana
Kutokana na dalili za baadhi ya vyama na wagombea kuwategemea vijana kufanikisha malengo yao, NEC inaliasa kundi hilo kuwa makini na kuhakikisha elimu inafika kwa rafiki zao lakini pia kuepuka ushabiki.
“Upo mtego wa kuwatumia. Jiangalieni na muwe makini na gilba za kisiasa. Epukeni kufuata mkumbo…kesho yenu inategemea kwa kiasi kikubwa na mnachokifanya leo,” anasema Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC.
Vyama vya siasa
Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Himid Mahmoud Himid anawaasa viongozi wa vyama vya siasa nchini kujenga uzalendo na kutambua yapo maisha baada ya uchaguzi, hivyo licha ya kunadi sera wanapaswa kufikiria juu ya hatima ya wafuasi wa vyama vyao.

No comments :

Post a Comment