Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, February 13, 2016

UCHAMBUZI, SIASA: Hamu ya ‘rais dikteta’ imekinai?



By Angetile Osiah, Mwananchi
Ilikuwa ahueni kuwa alitamka mwenyewe hadharani neno ‘dikteta’, baada ya wengi kulizungumza chinichini wakiogopa kupaza sauti zao kumuhusisha kiongozi wa nchi na sifa hiyo.
Lakini haikuwa ajabu kwamba Rais John Magufuli alikuwa anajua kuwa neno hilo linazungumzwa kila kona kwa kuwa vita na kasi aliyoanza nayo lazima ishtue wengi.
Kuzuia safari za nje isipokuwa kwa kibali cha Ikulu, kuzuia malipo holela ya posho kwa watumishi wa umma, kuzuia kufanya mikutano au semina za taasisi za umma kwenye mahoteli, kuzuia matamasha ya sherehe za kitaifa, kubana wafanyabiashara wakubwa katika masuala ya kodi, kusimamisha au kutimua watumishi waandamizi wa taasisi za Serikali ni baadhi ya mambo ambayo hayakutegemewa kufanywa na kiongozi mpya ndani ya miezi mitatu tangu aapishwe.
Hakuna shaka kwamba mambo hayo yaliinua kope za wengi ambao sasa macho yao yaliweza kumuona Rais Magufuli kwa darubini kali zaidi, wakijikita kuangalia jinsi anavyofanya maamuzi yake; ni shirikishi au binafsi, anasikiliza ushauri au haambiliki. Na bila shaka darubini hiyo ndiyo imewapa picha ya kutumia neno hilo.
Baada ya uchunguzi wa darubini hiyo, minong’ono ikaanza kusambazwa kutaka kuaminisha wengi zaidi kuwa kiongozi wa nchi hajali watu, hasikilizi ushauri, analotaka ndilo linafanyika na anatumia mabavu kuhakikisha kitu chake kinakwenda.
Hawa walizunguka wakikwepa kutumia neno moja ambalo wakilisema wanalitamka kwa kunong’ona; ‘huyu ni dikteta’.
Ni rahisi kuhalalisha neno hilo; wananchi wamebomolewa nyumba zao bila ya kupewa muda wa kutosha kujiandaa kuhama, wengine wamebomolewa wakati wakiwa na kesi mahakamani na watumishi waandamizi wa umma wanafutwa kazi kwa njia ambayo inaaibisha (mabalozi waliotakiwa kukabidhi ofisi mara moja baada ya muda wao kuisha, badala ya kuagwa kistaarabu).
Hata pale alipofanya uamuzi mzuri kama kupeleka fedha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kwenye ujenzi wa barabara, kwenye Idara ya Mahakama na sehemu nyingine, bado ilionekana anafanya maamuzi peke yake.
Suala jingine linaloweza kuhalalisha matumizi ya neno hilo ni hali inayoendelea Zanzibar, ambako upinzani unasisitiza Rais aingilie kati, lakini badala yake ulinzi ndiyo umeimarishwa kwa askari jeshi kuongezwa huku ikisisitizwa kuwa njia ya kumaliza mgogoro ni kurudia uchaguzi uliofutwa kwa njia ambazo CUF wanaamini si za kisheria.
Hadi sasa Ikulu haijatoa tamko madhubuti kuhusu hali hiyo na badala yake viongozi wanaomtembelea Rais ndiyo wanazungumza kuwa mkuu wa nchi hawezi kuingilia kati kwa kuwa atakuwa anaingilia uhuru wa Tume ya Uchaguzi (ZEC). Hayo na mengine machache lakini yanayoonekana makubwa yanawafanya baadhi ya watu wampe Rais jina tofauti.
Ile hamu ya baadhi ya wananchi kuwa na “Rais dikteta” iliyokuwa ikizungumzwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kutokana na kuona mambo yanaendeshwa kiholela bila ya kuwapo mkemeaji, imewakinai siku chache tu baada ya Rais kuonekana imara na mwenye kusimamia maamuzi yake.
Ile dhana kuwa kulikuwa na ombwe la uongozi na hivyo nchi kuhitaji rais anayefanya maamuzi, sasa imepotea.
Neno ‘dikteta’ ambalo watu walitaka lihusishwe na rais imara, shupavu na mzalendo, sasa linahusishwa na ubaya wa kiongozi anayeiendesha nchi kwa mwendo huo.
Imefikia wakati imekuwa kama watu hawajui wanataka kiongozi wa aina gani. Kiongozi mkali, imara kwenye maamuzi yake, mfuatiliaji na anayepambana na ufisadi? Au mpole, mwenye kauli za kukemea maovu, anayepambana na ufisadi bila ya kuchukua hatua kali na anayebadilika haraka baada ya kushauriwa?
Kwa kuingia kwenye jamii, binadamu wa mtazamo wa kati. Hapendi mtazamo mkali wa kitu chochote au kwa maana nyingine, hapendi mpole sana, hapendi mkali sana, hapendi mchapakazi sana, hapendi mvivu sana, hapendi mwizi sana na hapendi asiye mwizi sana.
Lakini utakuwaje kiongozi ukiwa mtu wa msimamo wa kati? Ni vigumu, lazima kutakuwa na ombwe la uongozi. Kwa hiyo ni lazima kiongozi awe na msimamo na awe na hoja kwa anayoyasimamia ili mradi yawe kwa masilahi ya wananchi.
Lakini hata sehemu ndogo ya wananchi inapolalamika, lazima kiongozi wa nchi awe tayari kusikiliza, hata kama wanalolalamikia ni gumu kulikiri hadharani. Ushupavu ni pamoja na kuwa tayari kukubali waziwazi udhaifu na kuufanyia kazi.
CUF wanapolalamika kuwa ZEC haikuwa sahihi kufuta uchaguzi na kuitisha uchaguzi mwingine kabla ya kukaa na vyama vya siasa kujadiliana udhaifu huo na jinsi ya kuumaliza ili kujenga hali ya kuaminiana, wana hoja ya msingi ambayo inaweza kufanyiwa kazi kwa mazungumzo kabla ya kwenda kwenye uchaguzi unaosimamiwa na Tume na mwenyekiti yule yule anayelalamikiwa.
Kutumia vifungu vya sheria vinavyoonyesha kuwa Rais hawezi kuingilia kati uchaguzi, ni kama kuitangaza Jumapili kuwa Jumapili, kitu ambacho ni dhahiri. Juhudi za ziada zinatakiwa, ndicho CUF na wadau wengine wanachokisema.
Jukumu la Serikali ni kulinda watu wake na mali zao. Hili jukumu lilifumbiwa macho wakati wa operesheni bomoabomoa. Ilikuwa ni kama “shauri yao, watajua wenyewe wataishi wapi”. Nyumba zilibomolewa bila ya wananchi kupewa muda wa kutosha. Watoto walilala juu ya vifusi na hakuna shaka kwamba wanawake na wasichana waliathirika zaidi ingawa ripoti hazijaanza kutoka.
Ni kweli kuishi mabondeni ni kuhatarisha maisha, lakini unaokoaje maisha kwa kubomoa nyumba za watu bila ya kujua wanaenda wapi? Kubomoa ni kuhatarisha zaidi maisha ya watu. Hapa vifo vinaweza kuwa si vya ghafla pekee, bali vingine vinatokana na magonjwa kama ya muda mrefu, madhara kwa watoto, wanafunzi na wazee.
Haya yalitokea bila ya Ikulu kutoa tamko madhubuti. Badala yake waliotembelea Ikulu, ndio waliolalamikia kuwa kufanya hivyo kunamchafua Rais.
Yako mambo mengi ambayo yalihitaji kasi ya kuyafanyia kazi mapema kabla ya neno ‘dikteta’ kunoga. Hatutaki Rais dikteta kwa maana ile mbaya inayokuzwa na wachache walioathirika na hatua zinazochukuliwa sasa, bali tunataka neno hilo liwe chanya.  

No comments :

Post a Comment