Maofi sa wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na maofi sa Taasisi ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) wakiwamo madaktari, wakifanya uchunguzi wa Faru John baada ya kufa katika eneo la Sasakwa Grumeti.
SAKATA la kutoweka kwa faru John lililoibuliwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika mikoa ya Arusha na Manyara linazidi kuchukua sura mpya kila kukicha.
Taarifa zilizolifikia MTANZANIA baada ya kufanya uchunguzi wa sakata hilo kwa wiki kadhaa sasa, zinaonyesha kwamba uamuzi wa kumhamisha faru huyo kutoka Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro ulihusisha mamlaka za kitaifa za Serikali.
Habari kutoka vyanzo vya kuaminika zinaeleza kwamba mchakato wa kuhamishwa kwa faru John kutoka Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro kwenda Grumeti, ulianza katika eneo la Nyasirori ndani ya Hifadhi ya Serengeti Aprili 17, 2015.
Uamuzi huo kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika serikalini, ulianza siku hiyo hiyo wakati wa tukio la kuwafungulia mbwa mwitu waliokuwa wamehifadhiwa katika eneo maalumu huko Nyasirori.Vyanzo vya uhakika vya habari vinaeleza kwamba mjadala kuhusu kuhamishwa kwa faru John ulifanyika wakati watendaji wakuu wa taasisi za uhifadhi za Serikali zinazounda Kamati Maalumu ya Kuwalinda Tembo na Faru (National Elephant and Rhino Steering Committee) wakiwapo.
Miongoni mwa watendaji wanaotajwa kuwapo wakati wa mjadala kuhusu kuhamishwa kwa faru huyo kutoka katika Bonde la Ngorongoro kutokana na sababu za kitaalamu, ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro (NCAA), Dk. Fadhili Manongi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi.
Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), Dk. Simon Mduma na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori aliyefahamika kwa jina la Alex Choya.
Taarifa kuhusu kuwapo kwa haja ya kuhamishwa kwa faru huyo zilipelekwa hadi Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kufikishwa kwa suala hilo wizarani kulifuatiwa na hatua ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Adelhem Meru, kuwaandikia barua watendaji wa Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro kutekeleza uamuzi huo ifikapo Desemba 31, 2015.
Alipoulizwa kuhusu uwapo wa barua hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema ni kweli barua hiyo ipo kwenye kumbukumbu za wizara.
“Ni kweli hiyo document ipo, lakini hili suala la faru John linafanyiwa kazi na vyombo vya dola. Nadhani si vizuri kulijadili kwa undani sasa, tusubiri matokeo ya uchunguzi,” alisema Waziri Maghembe.
Wahifadhi kadhaa waliozungumza na gazeti hili kutoka Serengeti na Ngorongoro juu ya sakata hilo, walieleza kwamba kiini cha kufikiwa kwa uamuzi huo kulitokana na mabadiliko makubwa ya kitabia aliyokuwa nayo faru John tangu mwaka 2002.
“Faru John alizaliwa ndani ya Ngorongoro, na alianza kuonyesha tabia za ukorofi dhidi ya faru wengine madume mwaka 2002,” alieleza mhifadhi mmoja anayefanya kazi Ngorongoro.
Mhifadhi mwingine alimweleza mwandishi wetu kwamba hali hiyo ilisababisha Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro kufanya mawasiliano na TAWIRI kuhusu hatua za kuchukua.
Alisema kuwa hali ilizidi kuwa mbaya na mwaka 2005 kiliitishwa kikao kingine kujadili matatizo ya faru John ambaye tabia yake ya kuwapiga faru wengine ilisababisha wanyama hao kutoka ndani ya Ngorongoro na hivyo kusababisha ugumu wa kuwalinda.
“Tatizo jingine lililotokana na ubabe wa faru John, ni gharama kubwa za ulinzi wa faru waliokimbia vipigo, na kutawanyika hadi kwenye mashamba ya watu.
“Faru wana tabia moja, pindi wanapopigana, yule aliyeshindwa huondoka eneo husika,” alieleza mhifadhi mwingine aliyezungumza na MTANZANIA.
Taarifa kutoka Ngorongoro zinaeleza kuwa mwaka 2013 tatizo la faru John lilizidi kuwa baya zaidi pale kreta, baada ya faru huyo kuua wenzake wawili.
Katika tukio hilo, faru John anatajwa aliua ndama (jike) kwa kumchoma na pembe na kisha akaua dume mwenzake katika mapigano.
Mhifadhi huyo aliliambia gazeti hili kwamba faru John ndiye aliyekuwa na watoto wengi katika Bonde la Ngorongoro kuliko faru mwingine yeyote.
Tukio la faru John kumuua ndama kwa pembe lilitokea wakati alipokuwa akijaribu kumpanda mama yake.
“Faru John alianza kuwapanda watoto wake, jambo ambalo kitaalamu si salama kwa uhai wa faru, hivyo kuendelea kumwacha pale kreta lilikuwa jambo la hatari.
“Baada ya matukio hayo ya 2013, kikao kilikaa tena ambapo TANAPA pia walihudhuria, swali kubwa likiwa ni wapi ambako faru John alipaswa kupelekwa?” alisema mhifadhi mwingine.
Kwa mhifadhi huyo, uamuzi wa kwanza ulikuwa ni kumtoa faru John na kumpeleka katika Hifadhi ya Mkomazi ambako kuna makazi maalumu ya faru (rhino sanctuary).
Hifadhi ya Mkomazi ambako hata hivyo uamuzi huo ulikwama, iko chini ya uendeshaji wa mwekezaji Tony Fitz John.
Kukwama kwa uamuzi huo wa kwanza pia kunaelezwa kulisababishwa na taarifa kwamba katika Hifadhi ya Mkomazi kulikuwa na uwiano sawa kati ya faru madume na majike.
Taarifa nyingine zinasema mwaka huo huo wa 2013, ulifikiwa uamuzi mwingine wa kumkata pembe faru huyo kama njia ya kupunguza madhara aliyokuwa akisababisha katika hifadhi, jambo ambalo lilifanyika.
Wakati wahifadhi wakiumiza vichwa kuhusu nini kifanyike, faru wawili waliokuwa Grumeti, waitwao Limpopo (dume) na Laikipya (jike) walipoteza maisha.
Taarifa zinasema Limpopo aliuawa wakati akipigana na tembo, wakati sababu za kifo cha Laikipya hazikutajwa.
Upungufu huo wa faru wawili ndiyo sababu ambayo baadaye ilisababisha kuzaliwa kwa hoja ya faru John kupelekwa Grumeti kupanda na kuzalisha majike.
Hali hiyo inatajwa kuwa ndiyo iliyosababisha uongozi wa Grumeti inayomilikiwa na tajiri wa Marekani, Paul Tudo Jones, waandike barua ya kuomba faru dume kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, jambo ambalo lilifanyika.
Vyanzo vya habari kutoka serikalini vinaeleza kuwa baada ya maombi hayo, kilikaa kikao cha Kamati ya Tembo na Faru mjini Dodoma ambacho kilitoa mapendekezo yake kuwa faru John anafaa kwenda Grumeti.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na usalama wake, gharama kubwa za kumhamisha na suala zima la siasa kuhusu hatua hiyo.
Kwa hiyo taratibu zikaanza, ikiwamo kutafuta madaktari watakaoshiriki kumkamata, ambao miongoni mwao walikuwa kutoka Kenya.
Hatua ya kwanza ya kumhamisha kwa mujibu wa taarifa za wataalamu wa uhifadhi, ilikuwa ni kujengwa kwa banda maalumu ambalo faru John aliingizwa Novemba 7, 2015.
“Unajua kuna taratibu za kuhamisha faru, hamuwezi kumdunga sindano ya usingizi na kumbeba, unaweza kumjeruhi na hata kusababisha kifo, kwa hiyo tulimuacha azoee lile banda kwanza kwa kumuwekea miwa, wanapenda sana miwa.
“Kwa kawaida mkishabeba banda alimo na kuliingiza kwenye gari maalumu, ndipo mnamdunga sindano.
“Kwenye banda hilo alikuwa akiingia na kutoka kwa mwezi mmoja, ilipofika Desemba 8, 2015, ndipo akapelekwa eneo la Sasakwa, Grumeti,” alieleza mmoja wa wahifadhi aliyeshiriki kumhamisha faru huyo.
Mhifadhi huyo alilieleza gazeti hili kwamba kazi ya kumhamisha faru John ilifanywa na watu 56 na magari 15, na baada ya kumfikisha, timu ya madaktari ilibaki Sasakwa kwa siku saba kufuatilia maendeleo yake.
“Kule Sasakwa kwanza aliwekwa kwenye eneo dogo ili iwe rahisi kumfuatilia, lakini ilipofika Januari 8, mwaka huu, alifunguliwa na kuachwa kwenye eneo kubwa la wazi, na afya yake ilikuwa vizuri na alikuwa na mahusiano mazuri na faru jike aliyekuwa eneo hilo,” alieleza mhifadhi mwingine.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa faru John alianza kuonekana amezubaa tofauti na uchangamfu wa awali na ilipofika Agosti 20, mwaka huu, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya kiasi cha kusimama kwa shida, jambo linalotajwa kuwashtua hata madaktari waliokuwa wakimwangalia.
Inadaiwa alipoteza maisha usiku wa kuamkia Agosti 21.
Mhifadhi huyo alisema kuwa faru John alikufa akiwa na umri wa miaka 38, miaka mitatu zaidi ya wastani wa maisha ya faru ambao ni miaka 35.
Alisema kuwa baada ya kifo chake uchunguzi wa kitaalamu kubaini sababu za kupoteza kwake maisha ulifanyika na kuhudhuriwa na madaktari kadhaa na wanafunzi zaidi ya 50 kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
Miongoni wa madaktari wanaotajwa kushiriki ni Dk. Morris Kilewo (TANAPA), Dk. Ernest Mjingo (TAWIRI), Dk. Emmanuel Macha (TANAPA), Dk. Justin Samanche (TAWIRI) na Profesa Donald Mpanduji wa SUA.
Taarifa nyingine zinasema kuwa baada ya uchunguzi huo, pembe mbili za faru John zilikabidhiwa kwa Mhifadhi wa Ikorongo-Grumeti, ambaye ni mtumishi wa wizara ili kuzipeleka Dar es Salaam ambako nyara za Serikali zinahifadhiwa katika jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House).
Pia pembe kubwa ya faru John ilikuwa imewekwa kifaa maalumu cha utambuzi (transponder), ambacho hadi sasa kipo ndani ya pembe hiyo, na kinachotakiwa ni kuweka betri na kupata taarifa kuhusu faru huyo, njia ambayo inatajwa kuwa bora kuliko vipimo vya vinasaba (DNA).
Baadhi ya wahifadhi ambao wamehojiwa na kikosi kazi maalumu kilichoundwa na Serikali kuchunguza kile kinachotajwa kuwa “utata kifo cha Faru John”, walisema suala hilo lilipaswa kufanywa na wataalamu wa wanyamapori.
“Jamani hili suala ni la kitaalamu zaidi, sasa tulitarajia iundwe timu ya wataalamu waliobobea katika masuala ya wanyamapori ifanye kazi kwanza, kisha kama kutaonekana kuna kosa la jinai, sasa kikosi kazi kingeingia kazini kuchunguza,” alisema mmoja wa wahifadhi waliohojiwa.
Desemba 6, mwaka huu akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru John kutoka hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba 8.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za Makao Makuu ya NCAA zilizopo wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hayo pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafugaji, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Saa 7 usiku Desemba 9, Waziri Mkuu alipokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko katika Hifadhi ya Grumeti.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu alisema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Profesa Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa, alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwapo ndani ya kreta.
“Kati ya faru 37 waliokuwapo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumwondoa John ulikuwa ni muhimu, ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.”
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, mwaka huu afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa Agosti 18, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru.
Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande, alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.
Mbali ya Waziri Mkuu kupokea ripoti na pembe za faru huyo, lakini siku tatu baada ya agizo hilo, maofisa watano wa NCAA wanaotuhumiwa kushiriki kumwondoa faru John kutoka katika kreta hiyo walikamatwa kwa mahojiano, ili kujua ukweli kuhusu mazingira ya kupotea kwake.
Pia Waziri Mkuu aliituhumu menejimenti na wafanyakazi wa NCAA kuwa imejaa vitendo vya rushwa na wizi na asingeweza kuvumilia sakata la faru John, ambaye alisema kuwa aliuzwa kwa Sh milioni 200 kwenye Hoteli ya Grumeti iliyo Hifadhi ya Serengeti na kuwa walipokea fedha za awali Sh milioni 100.
Waziri Mkuu alisema anataka kumwona faru huyo, nyaraka za kumhamisha na kama amekufa basi apelekewe hata pembe ofisini kwa kuwa anajua pa kuzipeleka.
Alisisitiza kuwa ikibainika kuna ambao wamekiuka taratibu watawajibika.
No comments :
Post a Comment