FEDHA zilizopotea kutokana na usafirishaji wa mchanga wa dhahabu kwenda nje ya nchi kuanzia mwaka 1998 ni nyingi sana.
Hivyo ndivyo yeyote anaweza kusema kuhusiana na taarifa kwamba taifa limepoteza mapato ya jumla ya Sh. trilioni 380.5 kwa kiwango cha juu kutokana na usafirishaji wa makontena 61,320 ya bidhaa hiyo katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka huu wa 2017.
Kwa kutumia kiwango cha wastani, thamani ya jumla ya makontena hayo katika kipindi chote ni takribani Sh. trilioni 183.5.
“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi kati ya 1998 na 2017, kwa kutumia kiwango cha juu ni TZS 380,499,453,421,688 (380.499 trilioni), sawa na USD 144,772,478,828 (USD 144.77 bilioni),” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo iliyokabidhiwa kwa Rais Magufuli jana.
Uthibitisho juu ya wingi wa fedha hizo, kwa mujibu wa uchambuzi wa Nipashe, ni ukweli kuwa kiasi hicho cha fedha kingeweza kununulia magari zaidi ya milioni 25 aina ya Toyota Noah, hivyo kutosha kugawiwa moja kwa kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea na kisha magari mengine takribani milioni mbili kukosa wa kuyaendesha.
Makadirio hayo, yamehusisha taarifa za baadhi ya ‘show room’ za kuuza magari jijini Dar es Salaam jana kuonyesha kuwa bei ya Noah yenye hali nzuri na pia kuwa na kiyoyozi safi, ilikuwa ya wastani wa Sh. milioni 15 kila moja.
Aidha, makadirio hayo yamehusisha pia idadi ya watu itokanayo na orodha iliyotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyoonyesha kuwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, Watanzania waliojiandikisha baada ya kuwa na sifa ya kuwa na umri wa kuanzia miaka 18 walikuwa tarkibani milioni 23, kati yao Bara wakiwa milioni 22.7 na Zanzibar ni 503,193.
Hata hivyo, Nipashe inatambua kuwa makadirio haya yanaweza kutofautiana na uhalisia endapo kiasi cha fedha kilichobainika kupotea kingehusisha pia ukokotoaji wa gharama za uzalishaji na usafirishaji ili hatimaye kibaki kiasi kinachotumiwa kukokotoa kodi na pia wapo Watanzania wenye umri zaidi ya miaka 18 ambao hawakujiandikisha kupiga kura kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa ripoti ya kamati teule ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli na kukabidhiwa (kwa Rais) jana, ikihusisha uchunguzi wa wataalamu wa sheria na uchumi, ilibainika kuwa taifa limepoteza mapato mengi kutokana na taarifa potofu za usafirishaji wa mchanga wa dhahabu kwenda nje ya nchi kuanzia mwaka 1998.
Ripoti hiyo ambayo muhtasari wake ulisomwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Prof. Nehemia Osoro, mbele ya Rais Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam jana, ilionyesha kuwa jumla ya mapato ya kodi yaliyopotea kwa kipindi chote hicho kupitia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu ni Sh. trilioni 108.
Katika uchambuzi wake uliohusisha makadirio ya fedha ghafi pekee (bila kuhusisha gharama halisi zikiwamo za uzalishaji na usafirishaji), Nipashe imebaini kuwa mbali na kila Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 kuweza kununuliwa gari aina ya Toyota Noah endapo fedha hizo zingetumika kuwapatia vyombo vya usafiri, fedha hizo zingeweza pia kufanikisha mambo mengine mengi ya maendeleo na pengine kuiondoa Tanzania katika orodha ya nchi masikini sana duniani.
Kwa mujibu wa Prof. Osoro, mapato yaliyopotea yamehusisha kodi ya mapato ya makampuni; kodi ya zuio la kodi, mrahaba na pia gharama za meli kutia nanga na upakuaji.
Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaomalizika mwezi huu ni takribani Sh. trilioni 29.5 huku bajeti ya mwaka ujao wa fedha inayoendelea kujadiliwa bungeni mjini Dodoma ni Sh. trilioni 31.7.
“Jumla ya mapato (kodi) ambayo Serikali ilipoteza ni Shilingi trilioni 108.46, ambazo ni sawa na bajeti inayokaribia miaka mitatu ya Serikali kwa kigezo cha Makadirio ya Matumizi ya mwaka 2017/2018,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo iliyokabidhiwa kwa Rais Magufuli jana.
MAGARI YA WAGONJWA, MADAWATI
Uchambuzi zaidi wa Nipashe umeonyesha kuwa kama fedha hizo ghafi zilizopotea katika usafirishaji wa mchanga wa madini kuanzia mwaka 1998 zingetumika kujengea barabara za lami za kiwango cha thamani ya Sh. bilioni moja kwa kila kilomita moja, taifa lingekuwa na mtandao wa barabara hizo safi wa urefu wa kilomita 380,000.
Aidha, endapo fedha hizo zote zingeelekezwa katika kujenga zahanati za kiwango cha thamani ya Sh. milioni 200 kila moja, tatizo la zahanati nchini lingemalizwa kabisa kwa sababu taifa lingeweza kuwa na zahanati milioni 1.9 nchini kote.
Kiasi hicho cha fedha kwa kiwango cha juu (Sh. trilioni 380) kingeweza pia kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa.
Hilo linatokana na ukweli kuwa, endapo kila gari la wagonjwa lingenunuliwa kwa wastani wa Sh. milioni 100 kila moja, maana yake yangepatikana magari milioni 3.8 ya aina hiyo.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alizindua ujenzi wa awamu ya kwanza ya reli ya kisasa (standard gauge) yenye urefu wa kilomita 300 kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro.
Katika uzinduzi huo, ilielezwa kuwa gharama za kukamilisha mradi huo ni Sh. trilioni 2.7. Hivyo, endapo fedha zilizobainika kupotea kupitia usafirishaji wa mchanga wa madini kuanzia mwaka 1998 zingetumika kujengea reli ya kisasa ya aina hiyo, maana yake taifa lingekuwa na mtandao wa reli za kiwango na urefu huo wa Dar hadi Moro zipatazo 140.
Kama hiyo haitoshi, fedha hizo (Sh. trilioni 380) zilizopotea katika usafirishaji wa mchanga wa dhahabu kuanzia mwaka 1998 zingetosha pia kununulia jumla ya madawati bilioni 2.7 endapo kila moja lingepatikana kwa gharama ya Sh. 140,000.
“Kiukweli hizi ni fedha nyingi sana. Kama tusingezembea na kila mmoja mwenye dhamana ya kusimamia masuala hayo angekuwa makini, maana yake leo hii tungekuwa tumepiga hatua kubwa za maendeleo.
Sijui kama bado tungeitwa taifa maskini sana duniani, “mkazi wa Tandika jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Luqman Muzzammil alisema kuiambia Nipashe jana.
No comments :
Post a Comment