dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, September 2, 2018

Balozi Seif atembelea eneo la ujenzi wa nyumba kwa wananchi walioathirika na mvua!



Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kuanzisha Miji Mipya katika maeneo mbali mbali nchini ni kuwapatia fursa wananchi kuishi kwenye makazi bora pamoja na kupunguza ongezeko kubwa la Idadi ya watu wanaohama na kuhamia sehemu moja.

Hayo aliyaeleza wakati alipotembelea Eneo la ujenzi wa nyumba za makaazi ya kudumu kwa wananchi walioathirika na mvua za masika mwaka uliopita ambapo nyumba hizo zinatengenezwa katika kijiji cha Nungwi mkoa wa kaskazini unguja.

Balozi Seif alisema hatua hiyo ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha miji mipyaya inakuja kwa lengo la kutambua thamani ya wananchi waliokutwa na maafa ya kubomolewa nyumba zao kwa mvua za masika mwaka jana lakini pia kuboresha makazi ya wananchi hususani wale wanohama hama kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Pia Balozi aliwaambia Wananchi walioathirika na Mvua za Masika kutambua kwamba wakati ukiwadia kuhamia katika Makaazi Mpya Nyumba zao za zamani zitalazimika kuvunjwa kwani zipo vile katika maeneo hatarishi kwa Maisha na Ustawi wa Viumbe.

Aidha Balozi Seif Alisema maeneo mengi ya nyumba zilizoathirika ni yale  yenye vianzio vya Maji kama chem Chem,Visima  na sehemu za mabondeni zilizotengwa kwa shughuli za Kilimo mabazo hazipaswi kutumiwa kwa ujenzi wa Nyumba za Makaazi kwa vile zinahatarisha uchafuzi wa mazingira na afya za Wanaadamu.

Mapema Mshauri Elekezi wa Ujenzi wa Nyumba hizo za Makaazi ya Waathirika wa Mvua za Masika za Mwaka uliopita kutoka Kampuni ya Samkay Consult Cooperation Lilited Bwana Amour Hamad Omar alisema Awamu ya kwanza ya ujenzi huo utazingatia Nyumba 15 za Makaazi.

Mhandisi Amour alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Kwamba Majengo hayo ambayo kila Nyumba itakuwa na Familia Mbili utaambatana na uwepo wa njia za kupitishia Maji ya Mvua kila baaba ya Nyumba Nne ili kuufanya uwe Mji wa Kisasa.

Alisema Awamu ya Pili ya Ujenzi wa Nyumba hizo utakamilisha Majengo ya huduma za Msikiti, Kituo cha Afya, Soko, Maduka pamoja na uwepo wa huduma zote muhimu anazopaswa kuzipata Mwanaadamu katika harakati za Maisha yake ya kila siku.

Mshauri Muelekezi huyo wa Usimamizi wa Ujenzi wa Nyuma hizo alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Ujenzi huo utazingatia muda halisi uliokubalika katika Mkataba wa Ujenzi ambao kwa mujibu wa hali halisi ya kuepuka msimu wamasika ujao mradi huo umepangwa kukamilika ndani ya Kipindi cha Miezi Minane badala ya ule wa mwanzo wa Mwezi Machi Mwaka 2020.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Haji Makame alisema eneo hilo tayari limeshapimwa na kuthibitisha kuwa na ukubwa wa Square Meter 9,315 Hata hivyo Ndugu Makame alimueleza Balozi Seif  kwamba kutokana na shauku ya Wafadhili ya kuonyesha nia ya kusaidia miradi ya Kiamii  katika maeneo mapya, maombi ya Uongozi wa Kamisheni hiyo umezingatiwa na kumepelekea Wataalamu wa Idara ya Ardhi kuongeza ukubwa wa Square Meter 2,400 ili liwe na ukubwa unaofanana na lile liliopo Tumbe Kisiwani Pemba.

Ziara kama ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi tayari ameshaifanya katika Kijiji cha Tumbe Mkoa wa Kaskazini Pemba kuangalia maandalizi ya Ujenzi wa Nyumba 30 za Makaazi ya Wananchi walioathirika na Mvua za Masika Kisiwani Pemba.

Ujenzi wa Makaazi ya kudumu ya Nyumba za Wananchi walioathirika na Mvua za Masika za Mwaka uliopita katika Kijiji cha Tumbe Kaskazini Pemba na Nungwi Kaskazini Unguja unafadhiliwa  na Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Umoja wa Falme za Kiarabu{ Red Cresent}.

Mradi huo Mkubwa wa utakapokamilika unatarajiwa kugharimu jumla ya Dola     Laki 850,000 za Kimarekani sawa na Shilingi za Kitanzania zipatazo Bilioni  Moja Nukta Nane, Tisa, Saba.{ 1,897,200.000/-}.

No comments :

Post a Comment