CUF wajiandaa kwenda mahakamani

Hussein Ibrahim Makungu (Bhaa)
- the winner of the by-election

Hussein Ibrahim Makungu (Bhaa)
- the winner of the by-election
Na Ameir Khalid
Thursday, September 20, 2012
CHAMA cha CUF kimeelezea nia yake ya kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo ya Uwakilishi jimbo la Bububu, yaliyompa ushindi mgombea wa chama cha Mapinduzi, Hussein Ibrahim Makungu (Bhaa).
Viongozi wa chama hicho wamesema hawakubaliani na matokeo ya uchaguzi huo kwa kile wanachodai kuwa haukuwa huru na ulikuwa na ubabaishaji mkubwa na wamepanga kwenda mahakamani katika muda wa siku 14.
Akizugumza na waandishi wa habari makao makuu ya CUF Mtendeni Zanzibar, Mbunge wa jimbo la Mtoni, Haji Faki Makame, alisema licha ya tume kutangaza matokeo, kamwe hawakubaliani nayo kwa sababu ilikibeba CCM.
“Kila mmoja alishuhudia ni nani ambae atakubaliana na matokeo yale wakati wenzetu walifanya kila hila ili kuhakikisha wanashinda, hivyo sisi CUF tunasema kuwa hatukubaliani na matokeo yale na hivi sasa tunajiandaa kwenda mahakamani kukata rufaa ndani vya siku 14,”alisema.
Alisema jopo la wanasheria wa chama hicho linafanaya mipango kuwasilisha pingamizi hilo mahakamani.
Hivyo alisema mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote na wanasheria wao kukamilisha kila kitu watakutana na waandishi wa habari ili kuweza kutoa tamko rasmi la siku ambayo watakwenda mahakani, kuwasilisha pingamizi yao.
Mbunge huyo moja kwa moja alielekeza lawama zake kwa Tume ya Uchaguzi kwa madai kuwa kwa kiasi kikubwa ndiyo iliyohusika kuvuruga uchaguzi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi wa chama hicho, Salum Bimani, alisema CUF kilifanya maridhiano ya kitaifa kwa lengo la kuhakikisha kuwa Zanzibar inaondokana na machafuko yanayohusiana na masuala ya uchaguzi, lakini bado inaonekana kuwa wengine hawakubaliani na jambo hilo.
Aliongeza chama chao kitahakikisha kuwa kinailinda serikali ya umoja ya kitaifa kwa nguvu zote, licha ya dalili ambazo zimeonyeshwa na vyama vyengine kutokuwa tayari kuisimamia serikali hiyo.
Chanzo: Mapara
No comments :
Post a Comment