dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, October 11, 2012

HUU ULIKUWA SIO MUUNGANO BALI SHIRIKISHO!

KER0 ZA MUUNGAN0: CHANZ0 
NA SABABU
         Na Amar Bawaazir
 Dokezo: 
Katika Hati ya Muungano, kitu kilichofanyika ni kwamba, jina la Serikali ya Tanganyika likabadilishwa na kupewa jina la Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Baadae ikabidilishwa kuwa Tanzania, na kutaka kuufuta kabisa utaifa wa Zanzibar. Wako wanaosema kuwa hiyo haikuwa sawa. Hata Katiba ya Tanganyika ikatumika, baada ya kurekebisha mambo machache tu, kama kubadilisha jina na bendera.
Uhuru wa Kuujadili Muungano
Katiba ni makubaliano ya wananchi juu ya namna wanavyotaka kujitawala. Kwa hivyo wana haki ya kuijadili juu ya mambo yote yanayowahusu wao. Bila shaka, tutaona kuwa Muungano ni jambo muhimu sana linalowahusu waZanzibari zaidi ya mambo yote mengine yaliyomo katika katiba. Rais Shein tayari ametuhakikishia kwamba tunao uhuru kamili kuijadili Katiba Mpya.

 Shirikisho au Muungano?
Kabla ya kuujadili Muungano, inafaa tutazame chanzo cha dhana ya Umoja wa Afrika Mashariki. Tukumbuke kwamba kabla ya uhuru wa nchi zote za Afrika Mashariki, vyama vyote vya siasa hapa Zanzibar na Afrika Mashariki vilikubaliana na wazo la kuungana katika Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF).
Mw. Nyerere alikuwa tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika kama nchi zote za Afrika Mashariki zingeweza kupata uhuru kwa pamoja na wakaungana. Kwa bahati mbaya, hili halikuwezekana. Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake kamili.
Miezi 4 tu kabla ya uhuru wa Zanzibar, Agosti, 1963, Waziri Tom Mboya wa Kenya alipelekwa na Kenya, Uganda na Tanganyika, kuiuliza Serikali ya Zanzibar kama wako tayari kuanza mazugumzo juu ya EAF ya nchi 4. Zanzibar ilitafakari na ikajibu kwamba walikuwa tayari.
Zanzibar ilipata uhuru wake kamili Disemba 10, 1963. Kama tunavyojua, Mapinduzi yakatokea Januari 12, 1964, lakini Zanzibar bado ilibakia na uhuru na madaraka yake kamili, pamoja na bendera, nembo, na haki zote za kitaifa, pamoja na kiti chake Umoja wa Mataifa (UN) na OAU.
Kwa ghafla ilitangazwa Aprili 1964, siku 100 tu baada ya Mapinduzi, kwamba Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zinaungana katika Muungano wa nchi 2 tu. Kuna maswali mengi ya kujiuliza hapa. :
Suali la kwanza: Kwa kiasi gani watu wa Zanzibar walishauriwa kabla ya kubadilisha muundo mzima wa serikali, na kupoteza uhuru wetu tuliopigania kwa miaka mingi?
Tunajua kwamba watu wa kawaida hawakuulizwa;
Inajulikana kwamba Marehemu Mzee Karume hakupewa fursa ya kuwa na mshauri wa kisheria wake mwenyewe – Hati ya Muungano iliandikwa na washauri wakizungu 2 wa Mw. Nyerere, na wao walitumia mfumo wa kikoloni wa Ireland ya Kaskazini kutuandikia Hati ya Muungano.
Hati ya Muungano haikuridhiwa (ratified) na Baraza La Mapinduzi, na Mwanasheria Mkuu wa SMZ amesema katika Mahakama kwamba SMZ haina nakala ya Hati ya Muungano.
Suali la pili: Kwa nini tukaiacha dhana ya Shirikisho ya Afrika Mashariki ya nchi 4, na tukavumbuwa Muungano mwengine mpya wa nchi 2 tu?
Hata Afro-Shirazi Party (ASP), ilikuwa haijataja katika katiba na ilani yake kwamba dira yao ilikuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hebu na tujiulize, kama kweli Mw. Nyerere alikuwa anaheshimu utaifa wa Zanzibar sawasawa na wa Tanganyika, pale alipoamua kuimeza sehemu kubwa ya Zanzibar ili isiweze kusimama tena kama nchi kamili?
Ingekuwa kweli azma ilikuwa kuleta Muungano wa Afrika nzima, mbona hata marafiki wake, Obote wa Uganda na Kaunda wa Zambia, walishindwa kujiunga katika Muungano wetu?
Mw. Nyerere alikua anapenda kuueleza Muungano kutumia mfano wa makapu, na leo hii tutautumia mfano huo huo. Kama nilivyosema mwanzoni, Tanganyika ilipata uhuru wake kamili 1961, na Zanzibar vilevile ilipata uhuru wake kamili 1963. Kwa hivyo, nchi mbili hizi zilikuwa na madaraka na haki za kimataifa sawasawa pale walipopata uhuru wao, na hata baada ya Mapinduzi.
Imeelezwa na Balozi wa Marekani kwamba aliporudi kutoka Dar es Salaam, Mzee Karume alikuwa anaamini kwamba amesaini Mkataba wa Ushirikiano baina ya nchi mbili hizi, kama alivyokuwa anaifahamu. Alipoulizwa Mzee Karume kwa nini haipo serikali ya Tanganyika kama ya Zanzibar, alijibu kwamba hilo lilikuwa shauri lao wenyewe. .
Jibu hilo halikuwa sawa, kwa sababu imeipa fursa Tanganyika kubadilisha gamba na kuvaa gamba la Tanzania, na kumeza madaraka mengi ya Zanzibar, kama tutavyoona.

Hati ya Muungano
Katika Hati ya Muungano, kitu kilichofanyika ni kwamba, jina la Serikali ya Tanganyika likabadilishwa na kupewa jina la Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Baadae ikabidilishwa kuwa Tanzania, na kutaka kuufuta kabisa utaifa wa Zanzibar. Wako wanaosema kuwa hiyo haikuwa sawa. Hata Katiba ya Tanganyika ikatumika, baada ya kurekebisha mambo machache tu, kama kubadilisha jina na bendera.
SMZ ikabakia, lakini madaraka 11 ya serikali hiyo yalihamishwa na kupelekwa kwenye Serikali ya Muungano. Sasa, tukiweka serikali 2 hizi katika mizani, zitakuwa hazina usawa tena, kwa sababu Serikali ya Muungano sasa imekusanya madaraka yote ya Tanganyika na mambo 11 ya Zanzibar.
Mambo haya 11 ya Muungano si yote yana sura ya kimataifa, bali yanahusu mambo mengi ya uchumi wa ndani. Biashara ya Nje ni katika mambo hayo ya Muungano, lakini uchumi wetu wakati ule ulikuwa unategemea sana uuzaji wa karafuu nchi za nje.
Hali kadhalika, Kodi ya Mapato na Ushuru wa Bidhaa yote haya yamehodhiwa na Serikali ya Muungano, na SMZ inapewa ruzuku ya aslimia nne nukta tano (4.5%) tu. Vilevile, SMZ inakosa madaraka juu ya biashara na kodi, hivyo inakosa uwezo wa kupanga uchumi wa nchi moja kwa moja. SMZ imeachiwa kazi ya kuendesha serikali bila kupewa nyenzo ya fedha. Kwa hivyo, hata mgawanyo wa madaraka haukuwa wa usawa.
Hati ya Muungano ni mkataba wa kimataifa kama unavyojulikana katika sheria ya kimataifa, na haiwezi kubadilishwa kila mara. Iligawana madaraka kati ya SMZ iliobakia na mambo yote yasiokuwa ya Muungano, na Serikali ya Muungano iliokuwa na madaraka yote ya Tanganyika yasiyo ya Muungano, na Mambo 11 ya Muungano ya Tanganyika na ya Zanzibar.

Mambo ya Muungano ya Ziada
Lakini mambo hayakuishia hapo. Kila mwaka au miaka 2, madaraka mengine ya Zanzibar yalikuwa yananyakuliwa na kufanywa Mambo ya Muungano, haya ni pamoja na sarafu (1965), mafuta na gesi (1968), na hata Baraza la Mitihani (1973). Mpaka sasa, mambo mengine 11 yamehamishwa kutoka katika madaraka ya SMZ na kupelekwa Dodoma – wengine wanasema mambo haya ni 22. Maana yake ni kwamba ile mizani iliyoinama sana baada ya kuundwa Muungano, basi sasa imelala chini kabisa.
Hapa tunapaswa tujiulize suali, jee hii ilikuwa ni halali? Hapa hatuna budi kumnukuu Prof. Shivji, mwanasheria aliyebobea katika sheria ya katiba. Huyu sio Mzanzibari lakini ni Mtanganyika; yeye si adui wa Mw. Nyerere bali ni mpenzi wa mawazo ya Mw Nyerere, na sasa hivi anakalia kiti cha Uprofesa wa Mw. Nyerere kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; yeye hachukii umoja, bali ni mkereketwa wa Umoja wa Afrika, na kiti chake cha Uprofesa kinaitwa Kiti cha Muungano wa Afrika.
Mwaka wa 1990 alitoa hotuba yake muhimu sana kama tunataka kufahamu chanzo na sababu za ‘Kero za Muungano’:
Alieleza kwamba sehemu ya Hati ya Muungano inayotaja mambo 11 ya Muungano, ndiyo iliyogawana madaraka kati ya serikali mbili, na kwa hivyo haiwezi kubadilishwa bila kuvuruga muundo mzima wa Muungano.
Na anaendelea kusema kwamba, si Bunge wala Baraza la Wawakilishi, kwa kila mmoja peke yake, hawana madaraka ya kubadilisha sehemu hii ya Hati ya Muungano. Kwa hivyo, Bunge kubadilisha sehemu hii,
kama ilivyofanya mara 11, ni kuzidisha madaraka yake, na kuipokonya Zanzibar. Huu ni ‘unyang’anyaji na ubomoaji wa mfumo halisi wa Muungano.’ Mwisho wake SMZ itabakia na kete tupu.
Prof Shivji anamalizia kwa kusema kwamba, mabadiliko yote yaliyofanyiwa sehemu hii ya Hati ya Muungano ni ‘haramu na batili.’
Kwa bahati mbaya, Serikali ya Tanzania hawakujali onyo la Profesa Shivji, baada ya miaka miwili tu, waliporejesha mfumo wa vyama vingi, wakaendelea na mtindo wao wa kawaida. Wakachukuwa fursa ya kumnyima Rais wa Zanzibar, anaechaguliwa na watu wa Zanzibar, nafasi yake kama Makamo wa Rais wa Tanzania, iliyotajwa katika Hati ya Muungano. Yeye alikuwa kiungo muhimu kati ya SMZ na Serikali ya Muungano. Sheria hii ilipitishwa na Bunge bila kuhitaji kura ya Thuluthi Mbili (2/3) kwa pande zote mbili. Wabunge wengi wa Zanzibar waliogopa kupinga msimamo wa chama tawala, na wakihiari kwenda kunywa chai au kwenda kujisaidia chooni badala ya kupinga chama chao.
Baadaye tu wakazinduka na wakaamua kumuingiza Rais wa Zanzibar kama Waziri bila Kazi Maalum katika Baraza la Mawaziri la Tanzania, ambayo ni kumvunjiya heshima yake. Badala yake, wakaleta mfumo wa Makamo Mwenza anaechaguliwa na Watanzania wote, na anatakiwa awashughulikie Watanzania wote, lakini hana nafasi katika SMZ.
Kwa ufupi, ongezeko la Mambo ya Muungano baada ya 1964, na kumuondosha Rais wa Zanzibar kutoka nafasi yake ya Makamo wa Rais wa Tanzania, yamevuruga kabisa muundo wa Muungano. Vilevile, yamevunja Hati ya Muungano, ambayo ilikuwa mkataba wa kimataifa kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Hati ya Muungano ndio Katiba Mama ya Tanzania. Kwa kiasi kikubwa, mambo yaliofanyika baada 1964 kwa makusudi hayakutaka kuheshimu makubaliano kati ya Marehemu Mzee Karume na Mw. Nyerere, na kuheshimu utaifa wa Zanzibar. Sasa, hata Jaji Mkuu na Waziri Mkuu wanathubutu kusema Zanzibar si nchi.

Katiba ya Muungano, 1977.
Lakini mambo hayakuishia hapa. Tuangalie Katiba ya Tanzania ya 1977 inayoendesha nchi hii kwa sasa hivi. Nirudie maneno niliosema mwanzoni kwamba katiba ni makubaliano ya wananchi juu ya namna wanavyotaka kujitawala. Lakini, kabla ya katiba kupata uhalali, inahitaji kupata ridhaa ya wananchi walioshirikishwa katika uundaji wa katiba ile, kama sasa tunavyoshiriki katika kuandika Katiba Mpya – hi ndio maana ya uhalali (legitimacy) tunapofikiria katiba.

Tukumbuke vipi Katiba ya 1977 iliandikwa. Mwaka ule vyama viwili vya ASP na TANU viliamuwa kuungana na kuunda chama kimoja, yaani CCM. Wenyeviti wawili waliteua kamati ya watu 20 chini ya Marehemu Thabit Kombo kuandika Katiba ya CCM – hiyo haitahusu sasa hivi.

Walipomaliza kazi ile, palepale, tarehe 16 Machi, 1977, Mw Nyerere, kama Rais wa Tanzania, aliteua kamati ileile kuandika Katiba Mpya ya Tanzania. Baada ya wiki moja tu, Tume ya Katiba ikawasilisha Muswada wa Katiba kwenye NEC ya CCM kupata baraka zake. (Hapa tufahamu kwamba muswada ule ulikuwa umeshatengenezwa hata kabla ya kuundwa Tume). Baada ya wiki 4 tu, na bila wananchi kupata fursa kuisoma na kuujadili muswada ule, ikapelekwa katika Bunge la Katiba.
Bungeni, watu watatu tu walijaribu kuijadili, lakini palepale Waziri Mkuu Sokoine akawambia kwamba muswada ule ushakubaliwa na Chama tawala chini ya mfumo wa chama uliokuwepo, kwamba Chama kimekamata hatamu, kwa hivyo haina haja kuujadili tena. Iliyobaki ni kupigiwa makofi.

Sasa tujiulize kama katiba iliyopitishwa namna hii bila kuwapa fursa wananchi kuijadili katiba yao, kama sisi sasa tunavyoijadili, inastahiki kukubaliwa kama ni takatifu na halali– kwa maana tuliotaja hapo mwanzoni?
Kuna matatizo mengi katika Katiba ya 1977, na ndio maana hata Serikali ya Muungano imekubali kuandika Katiba Mpya badala ya kutia viraka juu ya viraka. Lakini kuhusu Muungano, mimi nataka kuongea juu ya mambo 2 tu.

Jambo la kwanza ni kwamba nchi 2 ziliungana 1964, na kitu kilichowaunganisha ni Hati ya Muungano, na ndio inahisabika kama Katiba Mama ya Tanzania. Hio Hati ndio iliyozaa Katiba ya Serikali ya Tanzania na ya Serikali ya Zanzibar kama watoto wawili pacha. Katiba ya Tanzania haikuzaa Katiba ya Zanzibar, kwa sababu Serikali ya Tanzania haina madaraka juu ya mambo yasio ya Muungano ya Zanzibar.
Katiba ya Zanzibar inapata uhalali wake kutoka wananchi wa Zanzibar tu. Sasa, kwa nini Katiba ya Tanzania ya 1977 imeingiza sura nzima juu ya Serikali ya Zanzibar? Katiba ya Muungano haina madaraka yoyote juu ya rais wa Zanzibar, BLM au SMZ kwa ujumla, wala juu ya Baraza la Wawakilishi linalochaguliwa na watu wa Zanzibar tu chini ya Katiba ya Zanzibar.
Sasa kwa nini katiba ya Tanzania imetaka kujiingiza katika madaraka ya Zanzibar? Hii ni kutaka kujidai tu kwamba Katiba ya Zanzibar inatokana na Katiba ya Muungano, ambayo si kweli. Katika Katiba Mpya tunayotaka kuandika sasa, tusikubali kabisa kuwa na sura kama hii.

Mlango wa Nyuma wa Kuzidisha Mambo ya Muungano
[Katiba ya Tanzania kulipa Bunge mamlaka hata katika mambo yasiyo ya Muungano kwa Zanzibar.] Baya zaidi ni Ibara 64 ya Katiba ya Muungano ya 1977. Tunavyofahamu, Katiba ya Muungano inatakiwa ishuhulikie Mambo ya Muuangano na Mambo ya Yasio ya Muungano ya Tanganyika tu, na Katiba ya Zanzibar inatakiwa ishuhulikie Mambo yasio ya Muungano kwa upande wa Zanzibar. Lakini Ibara 64 kwa makusudi imeweka mlango wa nyuma wa kuzidisha mambo ya Muungano kinyemela.
Kifungu cha 4 kinasema kwamba:
(4) Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote haitatumika Tanzania Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo-
(a) Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar
29. Huu ni udanganyifu mtupu. Kama jambo ni la Muungano, haihitaji kusema kwamba itatumika Zanzibar vile vile; lakini kama si la Muungano, basi Bunge haina madaraka ya kusema itafanya kazi Zanzibar, full stop.
Lakini ndugu zetu wa damu waliendelea kutumia njia hii kutunyonya damu, na kuipora madaraka Zanzibar kila mwaka kutoka 1977. Kati ya 1977 na 2011, wamepitisha sheria ***? juu ya mambo yasio ya Muungano, na wakabandika bango kusema itatumika Zanzibar. Kwa mfano:
Siasa na vyama vya siasa sio mambo ya Muungano, lakini Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992 inasema kwamba sheria ile itatumika Bara na Zanzibar.
Bahari na uvuvi sio mambo ya Muungano, lakini Mwaka 1989 Bunge lilipitisha sheria ya Mamlaka ya Bahari na Maeneo ya Uchumi wa Bahari (Territorial Sea & Exclusive Economic Zone), ambayo ilisema kwamba hata maili 12 ya bahari wanamovua wavuvi wetu iko chini ya Muungano; na mwaka 1998 ikapitisha sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, na yote yalitamka kwamba yatatumika Zanzibar.
Juzi juzi Waziri wa Bara alikwenda New York kutaka kuzidisha maeneo ya Tanzania katika Bahari Kuu bila kushauriana na kukubaliana na SMZ. Wiki mbili zilizopita, Wachina waliokamatwa wakivua kwa njia ya haramu Mashariki ya Zanzibar 2009, walitozwa faini ya Sh. 20 billion na Mahakama ya Dar es Salaam – pesa hizi zitaishia Bara kama wale samaki wa Magufuli.
Kupora mamlaka ya Zanzibar ni suala la kikatiba, lakini Bunge halikuhitaji ata kura ya 2/3 kupitisha sheria hizi. Ni dhahiri kwamba hii ndio ilikuwa njia ya siri ya kuitekeleza sera iliomponyoka Mhe. Ali Hasan Mwinyi katika Bunge mwaka 1994[?].
G55 waliposema kwamba bora kulifikiria suala la Serikali Tatu kutatua kero za Muungano, Mzee Mwinyi aliteleza ulimi na akasema kwamba sera ya CCM ilikuwa kutoka Serikali Mbili na kuenda kwenye Serikali Moja, sera ambayo haikuwahi kutangazwa kabla ya hapo. Ajabu ni kwamba Mw. Nyerere alilaumu sana G55 na Waziri Mkuu Malecela kwamba Serikali Tatu haikuwa sera ya CCM, lakini hakukataa na hakumlaumu Mzee Mwinyi kwamba yeye vilevile aliokosea.
Bila shaka tuhakikishe kwamba Ibara kama hii isiwepo katika Katiba Mpya, na sheria zote zilizopenyezwa chini ya ibara hii zifutwe mara moja.
Hitimisho:
Kabla ya Uhuru tulikubaliana vyama vyote Zanzibar na nchi zote za Afrika Mashariki kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini lilioundwa 1964 haikuwa shirikisho lakini ni Muungano wa Serikali moja na nusu (1 ½).

Wananchi hawakuulizwa juu ya suala la Muungano. Hati ya Muungano haikupata ridhaa (ratification) ya BLM, na Mwanasheria Mkuu wa SMZ alisema Mahakamani kwamba haijulikani iko wapi. Kwa ufupi, inakosa ridhaa na uhalali kutoka kwa wananchi;
Hati ya Muungano ilitaja mambo 11 ya Muungano, lakini mambo mengine, kama biashara za nje na kodi, yanaathiri uchumi wa Zanzibar moja kwa moja;
Mambo mingine 11 yamezidishwa kinyemela, pamoja na mafuta na gesi, na Profesa Shivji anasema yanavuruga mfumo wa Muungano wa 1964, na ni haramu na batili;
Ibara 64 ya Katiba ya Muungano wa 1977 imefunguwa mlango wa nyuma ya kuipora mambo mengine mengi ya Zanzibar, kama Bahari Kuu.

Tukiendelea na mfumo huu wa Muungano, mwisho wake Serikali ya Zanzibar itakuwa kete au kapu tupu
– tutabakiwa na bendera na wimbo ya Taifa,
- BLW itakuwa halina kazi ya kupitisha sheria;
- SMZ itakuwa haina kazi ya kutawala nchi yetu;
- tutakuwa na mawaziri wanaopunga upepo tu;
- tutakuwa na rais wa pambo tu.
Basi na tujiulize kwamba, Huko ndiko tunakotaka kwenda?
Suala ni tuende wapi kutoka hapa kutatua ‘kero za Muungano’ zote.
Ni dhahiri kutokana na uchambuzi wetu tutaona kwamba hizi sio kero za juu juu tu; lakini ni matatizo na hata migogoro iliyosababisha kulazimishwa Rais Jumbe ajiuzulu. Matatizo haya yanatokana na:
§  Muundo (structure) wenyewe wa Muungano,
§  Tafauti kubwa ya kiwatu na ya kieneo kati ya nchi yenye watu milioni moja na nchi yenye watu milioni 45,
§  Maslahi na uchumi tafauti kati ya pande mbili,
§  Makosa yanayotokana na dharau wanayoionyesha Serikali ya Muungano tunapolalamika,
§  Udanganyifu na kutoaminiana pande zote mbili, n.k., n.k.
Hatuwezi kuendelea hivi. Lazima tukubali kwamba kuna matatizo mengi sana. Katika miaka 48 ya Muungano tumeunda tume na tumeandika ripoti zaidi ya 40, bila kutatua matatizo ya maana, na kila siku yanajitokeza matatizo mengine.
Sasa na tuwe majasiri kuandika Katiba Mpya ambayo itaweza kufikiria muundo muafaka na itakayoweza kukidhi mahitaji ya Zanzibar: serikali moja, mbili, tatu, Muungano wa mkataba, au nchi mbili hizi ziungane katika Shirikisho la Afrika Mashariki.
Pia jambo la msingi ni kuwashirikisha wananchi Wazanzibari juu ya suala la Muungano pekee. Wazanzibari hawajapata kushiriki kwa kuulizwa kuhusu Muungano, hivyo ni wakati muafaka kwa SMZ na Baraza la Wawakilishi kuwauliza Wazanzibari kuhusu Muungano. iIkiwa tunania njema na Zanzibar na Muungano wenyewe hili linawezekana na Katiba ya Zanzibar inaturuhusu kuwauliza jambo lolote la kitaifa wananchi kupitia Kura ya Maoni kabla ya kuingia kujadili na kupiga Kura ya Maoni kuipitisha hio Katiba Mpya ya Tanzania.


No comments :

Post a Comment