Nd. Absalom Kibanda
Tanzania Daima
Nov. 21, 2012.
Kwa mara nyingine tena, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeandika historia
mpya baada ya kufanya mabadiliko mazito katika safu yake ya uongozi wa
kitaifa.
Ni mabadiliko mazito si kwa sababu tu yamefanywa na CCM ambayo imekuwa
na rekodi ya kubadili sura za watendaji wake kwa namna na kwa njia
tofauti, bali kutokana na ukweli kwamba safari hii mabadiliko hayo
yamehusisha watu wazito, wenye historia ya kipekee katika medani ya
uongozi ndani na nje ya chama hicho.
Ingawa kwa mtazamo wa haraka haraka, mabadiliko hayo yanaweza
yakaonekana kuwa ni ya kuyabeza au kuyapuuza kama ilivyotamkwa na
baadhi ya wadadisi wa mambo wakiwamo wachambuzi wa masuala ya siasa na
hata wanazuoni, ukweli unabaki pale pale kwamba kile kilichofanywa na
CCM kinaweka alama ya kipekee katika mwenendo wa siasa za kitaifa za
siku zijazo.
Wasifu mzito na historia za kutukuka za baadhi ya wateule wanaounda
timu ‘mpya’ ya viongozi watendaji wa CCM kwa kiwango kikubwa ndicho
kitu kikubwa pekee kinachosababisha mtu yeyote makini ajikute akipata
shida kuyabeza yale yaliyofanywa na chama hicho tawala mwishoni mwa
wiki kule Dodoma.
Msuko mpya wa safu ya wakuu wa idara za CCM uliotangazwa na Rais
Jakaya Kikwete ukiwajumuisha wanasiasa wasiojua mizaha wawapo kazini
kama alivyo Philip Mangula, au makada wa muda mrefu wa chama hicho wa
kariba ya Muhammad Seif Khatib na Zakia Meghji una kila sababu ya
kutafutiwa dawa mahususi na makamanda wa kambi ya upinzani ambao kwa
muda mrefu wamekuwa wakipambana kuing’oa CCM madarakani.
Ni mtu asiyejali au mpuuzi asiyezijua vyema siasa za Tanzania
anayeweza akasimama na kuudharau uteuzi uliofanywa na Rais Kikwete
ambaye baada ya kushindwa mara kadhaa hatimaye amefanikiwa
kumshawishi, mmoja wa wanasiasa makini na wakongwe, mtumishi wa umma
wa muda mrefu, mwanadiplomasia na Kanali Mstaafu wa Jeshi,
Abdulrahaman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM.
Kwa muktadha wa makala ya leo na kwa kuzingatia nafasi kuu ya utendaji
aliyopewa, nitazungumzia kwa sehemu tu wasifu wa Kinana, mtu ambaye
naamini anapaswa kuangaliwa kwa jicho la karibu na wakati mwingine
kudhibitiwa ili kasi yake ya kukijenga chama alichopewa dhamana ya
kukinusuru isije ikasababisha kuyumba kama si mauti ya kisiasa kwa
baadhi ya vyama vya upinzani.
Ni wazi kwamba, kuteuliwa kwa Kinana kuwa Mtendaji Mkuu wa CCM Taifa,
akirithi mikoba iliyomshinda, Wilson Mukama, kumetutia ganzi baadhi
yetu ambao kwa muda mrefu tumekuwa ‘mashabiki’ au waumini wa kuchagiza
kwa njia ya kalamu na wakati mwingine katika mijadala ya wazi kwamba,
taifa lilikuwa na haja ya kutafuta mabadiliko ya uongozi kutoka nje ya
chama tawala.
Sitaki kuwa miongoni mwa wapenda mabadiliko ambao kwa njia za
kujifariji au za kujipa matumaini hewa wameingia katika mkumbo wa
jumla jumla wa kumbeza Kinana kwa namna wanayotaka kuuaminisha umma wa
Watanzania kwamba, mtu huyo anaweza akasukumwa kirahisi kwa namna ile
ile ilivyopata kuwa kwa watangulizi wake kadhaa waliopata kushika
wadhifa huo.
Hupaswi kuwa na akili nyingi kutambua kwamba, umahututi wa CCM
kisiasa, kulikokifikisha chama hicho tawala kufikia hatua ya kupoteza
dira na kuanza kuliona kaburi la kupoteza madaraka ya dola ndiko
kulikorejesha hekima za usikivu kichwani mwa Kikwete hata akalazimika
kuwarejesha akina Kinana, Mangula, Seif Khatib na Meghji katika
kilinge cha siasa za ushindani mkali ndani na nje ya CCM.
Siyo siri hata kidogo kwamba, hekima hii mpya ya Kikwete ya kumrejesha
Kinana ulingoni, ambaye siku chache tu zilizopita alitangaza kustaafu
siasa huku akisema alikuwa akikusudia kuwaachia vijana kusukuma
gurudumu la uongozi, inahusisha kichwa zaidi ya kimoja kutoka ndani na
nje ya CCM.
Kama ilivyo kwa wengi wengine nilianza kulisikia jina la Kinana
likihusishwa na ukatibu mkuu wa CCM miaka miwili au mitatu iliyopita
hali ambayo ilipata kusababisha nifikie uamuzi hata wa kumuuliza yeye
mwenyewe kuhusu taarifa hizo.
Jibu ambalo Kinana mwenyewe alipata kunipa kwamba alikuwa akipenda
kuona akiendelea kupata fursa ya kukitumikia chama chake kama mshauri
na kwa nyakati mahususi kama zile za kampeni na si kwa nafasi ya
ukatibu mkuu lilikuwa likinipa sana faraja.
Kilichokuwa kikinipa faraja si kingine chochote bali fikra zangu
(sahihi au potofu) ambazo siku zote zilikuwa zikinifanya niamini
kwamba, ukatibu mkuu kwa Kinana ilikuwa ni silaha moja ya maangamizi
kwa vyama vya upinzani ambavyo naamini vinapaswa kuendelea kupewa
fursa ya kuaminiwa na kukomaa.
Katika mazingira ambayo CCM imeweza kuepuka zahama ya kumeguka vipande
viwili kwa kuzingatia maono aliyokuwa nayo Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere, kwangu mimi Kinana wa zama hizo alikuwa na anaendelea
kubakia kuwa tishio kubwa kwa ustawi wa upinzani ambao ni rutuba
muhimu kwa maendeleo ya demokrasia na misingi ya utawala bora.
Hili ndilo ambalo naamini wapinzani wanapaswa kulitazama na
kulitafakari nyakati hizi wanapoendesha harakati zao za kukabiliana na
maguvu ya dola na haya mapya ya hoja ambazo aghalab zitaongozwa na
Kinana nyakati hizi taifa linapojiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa
miaka mitatu ijayo.
Haitoshi kwa kina Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, James
Mbatia, Dk. Willibrod Slaa na Zitto Kabwe kumbeza Kinana na timu ya
watendaji wake eti kwa hoja nyepesi na zisizo na mashiko za ufisadi au
uchafu wa jumla jumla wa CCM.
Wapinzani na wachambuzi wa mambo wanapaswa kujua na kutambua kwamba,
Kinana ni mwanasiasa wa vitendo, msomaji mzuri wa vitabu, ripoti,
taarifa, magazeti, msikilizaji na msikivu mzuri wa mambo mepesi na
mazito kuliko alivyokuwa ‘utopia’ Mukama anayeamini na kuzitetea
nadharia zisizotekelezeka.
Si hilo tu, wapinzani wanapaswa kutambua kwamba, historia yake ya
uaskari alioutumikia miaka 20 hadi mwaka 1972 akifikia cheo halisi cha
jeshi cha Kanali ikimhusisha na mafunzo mahususi ya kimkakati ni
sehemu ya mambo ambayo yanatawala nidhamu ya kazi ya aina ya kipekee
iliyomfanya Kinana akawa jemedari wa mapambano ya CCM tangu mwaka 1995
hadi leo.
Wachambuzi wa mambo, nikiwamo mimi mwenyewe ambao siku zote tumekuwa
tukiiona CCM kuwa chama kinachokufa kwa maana ya kuchungulia kaburi,
tunapaswa kuanza kutafakari upya mawazo yetu hayo, nyakati hizi Kinana
alipopewa dhamana ya kuwa mtendaji wake mkuu.
Tutakuwa wendawazimu iwapo tutamlinganisha Kinana na Mukama na kusahau
kwamba huyu aliye kilingeni leo ndiye aliyemuongoza Benjamin Mkapa
katika mapambano makali ya kisiasa mwaka 1995, zama Augustine Mrema
alipokuwa tishio la kwanza la kweli dhidi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Alikuwa ni Kinana aliyefanya kazi kubwa katika kipindi chote cha
kampeni akiratibu na kuongoza kampeni zote za Mkapa zilizomjumuisha
pia Mwalimu Nyerere katika mazingira ambayo wengi walikuwa wakiamini
CCM ilikuwa katika mwelekeo wa anguko la kihistoria.
Kinana ambaye kabla ya mwaka 1995 alikuwa tayari amepata kuwa Naibu
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Waziri wa Ulinzi alitumia vyema mbinu za medani na zile za
kidemokrasia na kiplomasia kumjengea uhalali Mkapa ambaye wakati huo
alikuwa mwanasiasa ambaye hakuwa akijulikana sana.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, siku chache tu baada ya kuingia
Ikulu kwa mara ya kwanza mwaka 1995, kwa sababu ama ya ulevi wa
madaraka au kwa kutingwa na kazi za kimamlaka, Mkapa alisahau kazi
kubwa aliyofanyiwa na Kinana.
Ni katika kipindi hicho cha kati ya mwaka 1995 na 2000 ndipo
nilipokutana kwa mara ya kwanza na mara kadhaa na Kinana nyumbani
kwake Masaki, jijini Dar es Salaam nikiwa nimeongozana na mhariri
wangu, Muhingo Rweyemamu, ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni
ambako nilipata fursa ya kumsikiliza na kuufahamu upeo mkubwa wa kuona
mambo aliokuwa nao mwanasiasa huyo.
Tangu wakati huo hadi wakati wa kampeni za mwisho za mwaka 2010,
niliendelea kukutana kwa nyakati fupi fupi na Kinana na mara kadhaa
nikawa mtu wa kufuatilia na kuzisikiliza kwa makini, habari zake
kutoka ama kwa marafiki au maadui zake wa kisiasa.
Sikushangazwa hata kidogo niliposikia tena kwamba, Mkapa alilazimika
kumuangukia tena Kinana na kumuomba aongoze tena kampeni zake mwaka
2000 kabla ya Kikwete naye hajafanya kile alichofanya mtangulizi wake
alipomuomba mwanasiasa huyo adhibiti joto la kiti cha urais mwaka
2010.
Uwezo wake mkubwa wa kisiasa, umakini wake na upeo mkubwa alionao
katika kuona na kuchambua masuala ya siasa, uchumi na jamii ndivyo
vitu ambavyo kwanza kwa nyakati tofauti vimepata kumfanya Kinana awe
Mbunge wa Jimbo la Arusha kwa miaka 10, Mbunge wa Afrika Mashariki na
Spika wa Bunge hilo.
Si ajabu hata kidogo kwamba, hata kabla ya kufikia huko, ni Kinana
huyo huyo ambaye alipata kuwa Mwakilishi wa Kidiplomasia wa Rais wa
Tanzania katika eneo la Maziwa Makuu na kabla ya hapo akiwa Mwenyekiti
wa Mawaziri wa Ulinzi wa Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC) zama akiwa
Waziri wa Ulinzi katika Serikali ya Awamu ya Pili iliyokuwa ikiongozwa
Rais Ali Hassan Mwinyi.
Uzoefu wake katika siasa za kiraia unaanzia mwaka 1972 wakati
alipostaafu jeshi akiwa Kanali baada ya kulitumikia kwa miaka 20 ndiyo
ambao amekuwa akiutumia kama silaha kubwa ya kukijua chama chake na
pengine kumfanya awe mmoja kati ya watu wachache ambao wamepata
kuwafanyia kazi marais wote wane wa Tanzania.
Anarithi mikoba ya Mukama akiwa mmoja wa wanasiasa wachache wa CCM wa
rika ile ile la kina Kikwete ambaye alilikimbia na kulikana kundi la
mtandao mwaka 2005 ambalo baadhi yetu tunaamini kuwa, ndilo
lilisababisha kuzaliwa kwa siasa mpya za kupakana matope, kuzushiana
na kuhujumiana ndani na nje ya CCM.
Lakini pengine kubwa katika yote hayo anaingia madarakani huku akiwa
na hazina ya uzoefu mkubwa wa kuongoza mapambano dhidi ya vyama vya
upinzani na kushinda katika mazingira ambayo aghalab yamekuwa yakiacha
vidonda visivyopona kwa wapinzani tangu mwaka 1995. Huyu si mtu wa
kumpuuza au kumbeza hata kidogo.
Chanzo: Tanzan Daima
No comments :
Post a Comment