Waziri wa Kilimo wa Uturuki Mchmet Mehdí Eker aliyekuwa ziarani kisiwani Zanzibar.
Waziri wa kilimo na chakula kutoka Serikali ya Uturuki Mchmet Mehdí Eker ameishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupanga mikakati ya kuifanya Sekta ya Utalii kuwa na manufaa moja kwa moja kwa Wazalendo badala ya Sekta hiyo kunufaisha wageni kutoka nje ya nchi…
Hayo ameyasema leo katika ziara yake ya kumtembelea Waziri wa Habari, Utalii,Utamaduni na Michezo Zanzíbar Said Ali Mbarouk Ofisini kwake Kikwajuni Mjini Zanzíbar.
Amesema wananchi ndio warithi wakubwa wa Serikali yao ilioko madarakani hivyo hakuna budi wao kufaidika mwazo na matunda ya utalii yaliyopo kabla ya kuwanufaisha wageni kutoka nje.
Amesema hali hiyo iwapo itafikiwa vizuri wananchi watapiga hatua kubwa kimaendeleo na kuepukana na umasikini unao wakabili.
Amesema maendeleo ya Sekta ya Utalii nchini Uturuki yanawanufaisha wananchi moja kwa moja kwa kuwapa kipaumbele wao badala ya wageni jambo ambalo limeifanya nchi hiyo kupiga hatua ya kimaendeleo na kuepukana na tatizo la ukosefu wa ajira. “Sisi nchi yetu kitu cha mwazo katika sekta ya utalii ni kuona kua wananchi wetu ndio wanaofaidika zaidi na baadaye kufuata wageni” alisema Waziri huyo.
Aidha Waziri huyo ameishauri Serikali kutilia mkazo kilimo cha mazao ya matunda ambayo yataweza kukidhi mahitaji ya Watalii ambao wanakuja kutembelea Zanzíbar jambo ambalo pia litachochea ongezeko la Watalii Zanzibar.
Waziri huyo amemuomba Waziri wa Habari na Utalii nchini kuweka mkazo katika kuulinda utamaduni wa Zanzíbar ili utalii usiwe kigezo cha kuharibu tamaduni na Silka za Zanzíbar.
Waziri Mchmet alimuahidi Waziri huyo kuwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zitafaidika zaidi kwa kupata wataalamu wa kilimo kwani Uturuki imeelekeza nguvu zake katika kuisaidia Tanzania katika Sekta ya kilimo
Kwa upande wake Waziri wa Habari utalii utamaduni na michezo Saidi Ali Mbarouk alimshukuru Waziri huyo kwa jinsi Uturuki ilivyojipanga kuisaidia Zanzíbar na Tanzania na kumuhakikishia kuwa Zanzibar itayafanyia kazi mawazo hayo hasa ikizingatiwa kuwa dhana ya “Utalii kwa wote” imeshazinduliwa ili kuwanufaisha wananchi.
Waziri Saidi alimuomba waziri huyo kuishauri nchi yake kuanzisha Safari za ndege za moja kwa moja kutoka Uturuki kuja Zanzibar na kuleta watalii wao ili kujionea vivutio vingi vya utalii vilivyopo Zanzibar.
Chanzo: ZanzibariYetu

No comments :
Post a Comment