
Mtwara
NA MWANDISHI WETU
28th December 2012
.jpg)
Maandamano hayo ambayo yaliwajumuisha wananchi kutoka baadhi ya wilaya za mkoa wa Mtwara, zikiwamo Tandahimba na Newala, yalifanyika kwa amani na utulivu huku yakisindikizwa na polisi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na waratibu wa maandamano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia, alipaswa kuyapokea lakini alikataa na badala yake yalipokelewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Siasa, Hussein Mussa Amiri.
Vyama vilivyounda umoja huo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi, Sau, Tanzania Labour Party (TLP), APPT- Maendeleo, ADC, UDP na DP.
Vyama hivyo vilikuwa na kaulimbiu ya `Gaesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.'
Soko Kuu la mjini hapa, lilifungwa kwa muda hadi maandamano hayo yalipomalizika kwa lengo la kutoa fursa kwa wafanyabiashara hao kushiriki maandamano hayo ambayo yalisababisha barabara kufungwa kwa muda.
Mabango yalitumika zaidi kuwasilisha ujumbe wa wananchi hao wa kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.
Baadhi ya mabango hayo yalisomeka `Bandari Bagamoyo, Viwanda Bagamoyo, Gesi Bagamonyo, Mtwara wapuuzi?...Gesi haitoki hata kama hatujasoma...Gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu...Kusini tumedharauliwa vya kutosha sasa baasi.'
Akisoma tamko la vyama vya siasa vya upinzani vilivyoungana kupinga gesi kwenda Dar es Salaam, Katibu wa umoja huo, Seleman Litope, alisema kwa muda mrefu mikoa ya Kusini imekuwa ikiondolewa fursa mbalimbali za maendeleo, akitolea mfano wa kung'olewa kwa reli, ukosefu wa usimamizi mzuri wa zao la korosho, ukosefu wa miundombinu ya barabara, kuondolewa kwa mradi wa maendeleo ya ukanda wa Mtwara (Mtwara Corridor ) na kuondolewa kwa gesi.
Alisema hali hiyo imesababisha Mikoa ya Kusini kuwa nyuma kimaendeleo na hawako tayari kuona historia ikijirudia.
Alisema umoja wao wa vyama vinane vya siasa unalenga kuhakikisha rasilimali yao hiyo haitoki kwenda kokote kabla ya kuwanufaisha.
"Ujenzi usitishwe...serikali hadi leo haiko wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo wakati Rais ameshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam...uwazi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais Jakaya Kikwete, alilolitoa kwenye ziara yake mkoani Mtwara mwaka 2009 kwamba mkoa wa Mtwara ujiandae kuwa ukanda wa viwanda," alisema Litope.li
Taarifa hiyo ilibainisha: "Tuna hofu kutokana na ilivyokuwapo kwa wakazi wa Songosongo kubaki maskini wakati gesi inazalishwa hapo, yasije yakatukuta sisi, hivyo ni lazima tusimamie rasilimali hii ili ilete maendeleo.”
Tamko hilo lenye kurasa mbili likiwa na maazimio tisa, linahoji kwanini mitambo ya kuzalisha umeme isijengwe Mtwara wakati eneo kwa ajili ya ujenzi huo linapatikana.
Aidha, waandamanaji hao wamemuomba Rais Kikwete, kumuondoa madarakani Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia, kwa madai amewatusi wananchi wa mkoa huo kwa kuwaita wapuuzi kutokana na madai yao ya kupinga gesi kwenda jijini Dar es Salaam.
“Tunamuomba Rais Kikwete amuondoe katika nafasi ya ukuu wa mkoa ndugu Simbakalia na kutuletea mwingine kwa sababu ametutukana hadharani, tumeshindwa kuvumilia...hatumtaki," ilisema sehemu ya tamko hilo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment