NA MWANDISHI WETU
27th December 2012
.jpg)
Habari zinasema kuwa Padri Mkenda alipigwa risasi juzi majira ya majira ya usiku nyumbani kwake na watu wawili wasiojulikana waliokuwa katika pikipiki aina ya Vespa kupitia kioo cha mbele ya gari yake aina ya Toyota Rav4 wakati akirejea nyumbani kwake baada ya kutoka kanisani kuhudhuria misa.
Taarifa ambazo zimethibitishwa na Jeshi la Polisi Zanzibar, zinaeleza zaidi kwamba kiongozi huyo wa kiroho alipigwa risasi akiwa nje ya lango la nyumba yake wakati akisubiri kufunguliwa na mlinzi.
Padri huyo alitokwa damu nyingi na kuulazimu uongozi wa Kanisa Katoliki Zanzibar kumpeleka katika Hospitali ya Alrahama na baadaye Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambako alifanyiwa upasuaji mdogo katika eneo la taya na baadaye kumsafirisha kwenda dare s Salaam na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Tukio la kupigwa risasi kwa Padri Mkenda limekuja miezi mitatu tangu msaidizi wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, amwagiwe tindikali na watu wasiojulikana na kupelekwa kwenye matibabu nchini India.
Matukio ya vurugu katika siku za karibuni yameiandama Zanzibar huku viongozi wa dini wakitishiwa na kushambuliwa. Kwa mfano kabla ya tukio la kumpiga risasi Padri Mkenda, yalitokea matukio 12 ya kuchoma moto baa pamoja na matukio 25 ya kuchoma makanisa katika maeneo tofauti visiwani Zanzibar.
Habari zilizosikika kabla ya tukio hilo kwamba vilitolewa vitisho kutoka kundi la Uamsho kwamba kama Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) isingewaachia huru viongozi wao ambao wako rumande kwa tuhuma mbalimbali za kuvunja amani, lingetokea tukio kubwa Zanzibar kabla ya sherehe za Krismasi.
Taarifa hizo za vitisho kupitia vipeperushi, hatimaye zimekuwa za kweli kwa kuwa Padri Mkenda alipigwa risasi saa 1:30 jioni kabla ya maadhimisho ya Krismasi kuanza baadaye usiku.
Baadhi ya watu wanalihusisha tukio hilo na ujambazi kutokana na kiongozi huyo wa kiroho kuwa ni mhasibu wa parokia hiyo. Kwamba kajambazi walimpiga risasi kwa lengo la kumpora fedha.
Askofu wa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Cosmas Shao Shao, ametoa ufafanuzi kwamba tukio hilo lisihusishwe na ujambazi kwa kuwa Padri hatembei na fedha za miradi ya kanisa.
Kauli ya Askofu Shao inapunguza nguvu hoja za baadhi ya watu hao akiwamo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, ambaye alisema kuwa inawezekana padri huyo alipigwa risasi na majambazi kwa lengo la kumpora fedha kwa kudhania kuwa kanisa lilikuwa limekusanya fedha nyingi kutoka kwa waumini wakati wa Krismasi.
Jambo la msingi kwa sasa ni kwa SMZ kupitia vyombo vyake vya usalama ni kuchukua hatua za haraka kudhibiti vitendo vya uhalifu ambavyo vinaelekea kuwa tishio kwa usalama wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa kuwa visiwa hivyo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufuatia matukio kadhaa yaliyofanywa na watu wanaodaiwa kuwa nyuma ya Uamsho, SMZ ilionya kuwa uvumilivu sasa basin a kwamba haitasita kuchukua hatua ikiwamo kuifutia usajili taasisi yoyote itakayobainika kujihusisha na vitendo vya kutishia amani.
Ikiwa SMZ itakaa kimya bila kuchukua hatua kwa vitendo baada ya tukio la juzi, wananchi wengi watashindwa kuwaelewa viongozi wake wala kuwaamini.
Haiwezekani serikali yoyote duniani ikaviendekeza vikundi ambavyo vinafanya matendo ya uhalifu na kutishia amani ya nchi kama vinavyotaka.
Swali la kujiuliza nije, Jeshi la Polisi Zanzibar kwa nini halikuweka ulinzi wa doria katika maeneo yote ya Zanzibar kama hatua ya kuwahakikishia ulinzi wananchi na mali zao wakati wa Krismasi kabla ya tukio hilo kutokea?
Ndiyo maana Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidhi, alisema kwamba Jeshi la Polisi limeonyesha udhaifu wa kusimamia ulinzi dhidi ya raia na mali zao.
Ni matumaini yetu kuwa Jeshi la Polisi Zanzibar litawatia mbaroni waliohusika na uhalifu huo na SMZ itachukua hatua za kukomesha vitendo hivyo ili Zanzibar iendelee kuwa sehemu ya watu kuishi bila hofu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment