Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, January 3, 2013

PADRE AMBROSE MKENDA: Mfano wa ajabu na dhihaka

Na Jabir Idrissa


KINACHOENDELEA sasa nchini petu ni mfano wa maajabu na dhihaka. Kila kiongozi wa ngazi ya juu ameharakia ubavuni mwa kitanda alikolala padre Ambrose Mkenda katika kitengo cha mifupa (MOI) cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Padre Mkenda, wa Kanisa Katoliki (RC) anayeongoza Parokia ya Mpendae, mjini Zanzibar, amelazwa hapo akiuguza majeraha aliyopata baada ya kupigwa risasi na wahalifu wasiofahamika. Ni katika tukio la majira ya saa 3 usiku wa Desemba 25, akiwa anasubiri kufunguliwa geti ili kuingia kwenye nyumba anayoishi eneo la Tomondo. Alikuwa anaingiza gari kwenye geti wakati aliposhtukia anavuja damu sehemu ya chini ya kidevu.
Walianza viongozi wachache wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar asubuhi ya siku ya pili alipokuwa anafanyiwa mipango ya kusafirishwa jijini Dar es Salaam baada ya madaktari wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kusalimu amri kuwa hawangeweza kutoa risasi zilizomganda mwilini.
Inasemekana padre huyo alipigwa risasi kadhaa na watu wawili waliokimbia kwa kutumia pikipiki.
Awali, padre Mkenda alipelekwa hospitali binafsi ya Al Rahma ambako baada ya kumpatia huduma ya kwanza, madaktari waliagiza apelekwe hospitali ya serikali kwa kuwa hawana ujuzi wa kumsaidia zaidi kwani alikuwa na risasi mwilini.
Alipofikishwa tu Muhimbili, viongozi wakuu wa dola katika Jamhuri ya Muungano wakaanza hamkani. Akaanza kinara wao anayesifika kwa safari za nje ya nchi, Rais Jakaya Kikwete. Akafika kumjulia hali.
Akafuata msaidizi wake namba moja, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambaye ni makamu wa rais.
Akaruka ndege msaidizi mkuu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi, ambaye ameendelea kuitia gharama nyingi serikali kwa kuruka mara kwa mara kati ya Zanzibar, Dar es Salaam na Dodoma wakati wa vikao vya Bunge na vile vya ngazi ya juu vya CCM, chama kilichompa ulwa akianzia na ubunge jimboni Kitope, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mvumo wa viongozi wakuu wa nchi kuharakia kumkagua padre Mkenda ulishaanzwa mapema. Jeshi la Polisi lilishatoa msimamo wa kuhakikisha litawatia nguvuni wahalifu waliohusika kutaka kumtoa roho padre Mkenda.
Jeshi hili lenye historia mbaya ya kushindwa kupeleleza kitaalamu yanapotokea matukio ya kutatanisha kama hili la kujeruhiwa padre, limetuma wapelelezi maalum kutoka makao makuu Dar es Salaam kusaidiana na waliopo Zanzibar ili kusaka wabaya wa kiongozi huyu wa dini inayostahiwa sana na dola ya Tanzania.
Shaka ya kwanza: Iweje mara tu baada ya padre mkatoliki kujeruhiwa kwa risasi, Polisi itume makachero mahsusi kusaka wahalifu wakati haifanyi hivyo kwenye matukio mengi yanayowasibu wananchi?
Mpaka sasa chombo hichi cha ulinzi na usalama wa raia hakijakamata mtu hata mmoja kuhusiana na tukio la kujeruhiwa kwa tindikali (acid) Sheikh Fadhil Soraga, Katibu wa Mufti wa Zanzibar. Sheikh Soraga, kijana mbichi, alimwagiwa acid akiwa anakakamua mwili (jogging) kwa kupita pembeni mwa barabara ya Kiembesamaki/Mwanakwerekwe-Amani/Mtoni, mapema mwezi Novemba uliopita eneo la Nyerere.
Ingawa amerudi matibabuni nchini India kiasi cha siku kumi hivi zilizopita, walio karibu naye wanaieleza hali yake kama isiyoridhisha kutokana na majeraha ya usoni na kifuani kuendelea kumsumbua.
Hakuna makachero maalum waliotumwa kusaka mhalifu wake na wendaji wa viongozi wakuu wa Zanzibar na wale wa dola ya Tanzania kumkagua haufanani na unaoonekana kwa padre Mkenda. Mwezi kabla, askari polisi wa FFU, Koplo Said Abdulrahman Juma aliyekuwa akitoka kazini alipigwa na kuuliwa eneo la Bububu katika tukio lililohusisha makumi ya vijana waliokuwa na hasira baada ya kupotea kwa kiongozi wa Jumuia ya Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed siku mbili kabla.
Hakuna viongozi waliochakarika na kuagiza upelelezi maalum ufanywe kukamata wahusika. Badala yake, kilichofanywa ni dola kutuma askari wa vikosi visivyo nidhamu vya Zanzibar na kuamuru kupiga na kudhalilisha wananchi usiku na mchana majumbani na mitaani.
Taarifa za karibuni kabisa za Polisi zimethibitisha kuwa hakuna mtu aliyefikishwa mahakamani ingawa mamia ya watu walikamatwa katika ile hali ya kukurupuka baada ya tukio. inatoa matamko yanayoashiria kutuhumu makundi ya wanaharakati wa Uamsho kuhusika nayo. Hawa sasa ndio taulo la dola kila kunapotokea uhalifu.
Hali kama hii maisha haitaleta tija katika kazi ya vyombo hivi vya kutunza usalama wa wananchi. Badala yake, vitakuwa vinachochea chuki dhidi ya askari wenyewe na dola kwa ujumla wake. Hapatakalika.
Kama polisi wamekosa watuhumiwa wa matukio mawili ya awali kwa kuwa hawakujishughulisha kitaalamu kuwatafuta, inakuaje watoe ahadi na kutunisha misuli leo kufuatia kujeruhiwa kwa padre Mkenda?
Mtu atakuwa na kosa gani akisema anaona mienendo ya kibaguzi, kidini na kiasili ya mtu atokako, katika utendaji kazi wa vyombo hivi vya ulinzi na usalama nchini? Hana kosa lolote. Matarajio ya wananchi ni kuona matukio ya uhalifu yanachukuliwa kwa uzito unaowiana hata kama mazingira yake yaweza kutofautiana. Uhalifu ni uhalifu tu; hakuna uhalifu mkubwa na uhalifu mdogo hasa pale unapokuwa umehusisha kuhatarisha maisha ya mtu.
Nilidhani Polisi wajisikie aibu kwa kushindwa kukamata mtu katika matukio mawili ya awali na wajiulize kwanini wameshindwa kubaini mbinu za wahalifu husika? Sijui kama wanajiuliza. Basi niseme kuwa umefika wakati sasa Polisi warudi kwenye mstari ulionyooka kwa kutenda kazi yao ngumu ya kulinda raia kwa kuzingatia misingi ya weledi na mbinu za kisasa za kipelelezi. Wasikurupuke.
Vinginevyo taasisi hii itaendelea kugeuzwa chombo cha mzaha mtupu kinachotenda kazi kwa kufuata amri za wanasiasa watawala ambao kwa Tanzania wameendelea kuthibitisha kuwa wanaongoza kwa woga wa kubanwa na kanisa.
Chanzo: ZanzibariYetu

1 comment :

  1. rafiki yangu ulieandika hii habari nafikiri una uhaba wa kufikiri? Wanaofanya uhalifu ni dini gani? nafikiri ungeshirikisha ubongo vizuri ndio ungeandika hii kitu. rais au makamu wake kusafiri sio kitu kibaya kila mara, padre kutembelewa na viongozi pia sio kitu cha ajabu, after all waliofanya uhalifu ni waislam na viongozi wa nchi pia ni waislam. waliommwagia sheikh acid pia ni waislam sababu tu ni BAKWATA na wao wanataka mabadiliko. Usiamini kila unachoambiwa na viongozi wetu wa dini. wengi elimu hawana wanatujaza ujinga na kuharibu amani ya nchi. ni kweli nchi yetu ina matatizo ila akili na busara ndizo zinahitajika kuyatatua na si upanga kama tunavyofundishwa.

    ReplyDelete