NA WAANDISHI WETU
4th January 2013
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete, mtalii huyo alifariki dunia juzi, akiwa na wenzake 21 wakati wakipanda mlima huo kupitia njia ya Londorosi wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.
Alisema mtalii huyo mwanaume, alikutwa na umauti hayo wakati akiwa njiani kuelekea kituo cha Kibo Moir na alifika nchini kwa shughuli za utalii wa kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika mwishoni mwa Desemba, mwaka jana.
“Walianza safari ya kupanda mlima Desemba 30, mwaka jana, kwa kampuni ya utalii ya mkoani Arusha kutokana na ajali hii wageni wengine 21 wamesitisha safari ya kupanda mlima huo,” alisema.
Shelutete aliongeza kuwa Tanapa kwa kushirikiana na kampuni ya utalii aliyotumia mzungu huyo, wanaendelea na taratibu mbalimbali za kushughulikia ajali hiyo pamoja na matibabu kwa waliojeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alipoulizwa juu ya tukio hilo, alisema hana taarifa na kuomba apewe muda zaidi wa kufuatilia.
Katika hatua nyingine, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Nyabichenguche Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Nyarero Marwa (20), amekufa papo hapo baada ya kupigwa na radi akiwa amejikinga na mvua katika kijiji cha Rebu.
Ndugu yake, James Omahe, alijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime/ Rorya, Justus Kamugisha, alisema kuwa mwanafunzi huyo alipigwa na radi jioni akiwa amejikinga mvua na wenzake akiwamo ndugu yake, James Omahe kijijini hapo.
Alisema mwanafunzi huyo alikufa wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.
BASI LA NEW FORCE LAUA
Wakati huo huo, watu watatu wamekufa papo hapo na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya New Force kuacha njia na kupinduka katika kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Basi hilo aina ya Youtong, lenye namba za usajili T 465 BBH, linalofanya safari zake kati ya Mkoa wa Mbeya na Dar es Salaam, lilipata ajali hiyo jana saa 4:50 asubuhi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, basi hilo lilianza kuyumba na kisha kuacha njia kabla ya kupinduka kutokana na mwendo kasi.
Mmoja wa maofisa wa Jeshi la Polisi aliyekuwapo eneo la tukio ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa msemaji, alithibitisha vifo vya watu hao watatu.
“Watu waliokufa hapa ni watatu na wengine zaidi ya 50 wamekimbizwa katika Kituo cha Afya cha Nyololo na ambao hali zao ni mbaya walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi kwa matibabu,” alisema.
Miili ya watu waliokufa katika ajali hiyo imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi ikisubiri kutambuliwa na ndugu zao.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment