• WAMO PIA WALIOWAJERUHI VIONGOZI WENGINE
na Hassan Ali Ame, Zanzibar
SIKU chache baada ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kulisuta Jeshi la Polisi nchini, jeshi hilo Visiwani Zanzibar limetangaza kumkamata mtuhumiwa aliyemuua Padre Evalistus Mushi, Februari 17 mwaka huu.
Kardinali Pengo alilituhumu jeshi hilo akisema limekuwa kimya kuhusu uchunguzi wa matukio ya kushambuliwa kwa viongozi wa dini visiwani Zanzibar na badala yake serikali imekuwa ikidai vinafanywa na wahuni.
Padre Mushi wa Parokia ya Shangani Zanzibar aliuawa kwa kupigwa risasi muda mfupi baada ya kuwasili kanisani hapo kwa ajili ya kuongoza ibada.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamishna wa Polisi, Mussa Ali Mussa alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Omar Mussa Makame mkazi wa shehia ya Mwanakwerekwe Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Pia alisema kuwa jeshi hilo limewakamata watuhumiwa waliohusika na kitendo cha kumpiga risasi Padre mwingine wa Kanisa Katoliki, Ambrose Mkenda na kummwagia tindikali Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhili Soraga mwaka jana.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika mazingira tofauti na majalada yao ya uchunguzi yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka wa Zanzibar.
Taarifa za uchunguzi zinasema kwamba mbali na mtuhumiwa kuwa fundi seremala, pia ni mwanasiasa ambaye aliwahi kugombea nafasi ya uwakilishi katika Jimbo la Raha Leo kupitia chama kimoja cha upinzani visiwani Zanzibar.
Kamishna Mussa aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 17 mwaka huu, katika Mtaa wa Kariakoo nje kidogo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Alisema kwamba uchunguzi uliokuwa ukifanywa na makachero wa wa polisi kwa kushirikiana na wapelelezi kutoka Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) umefanikisha kumkamata mtuhumiwa huyo.
“Muhusika wa mauaji ya Padre Mushi tayari amekamatwa na ametambuliwa na watu walioshuhudia tukio hilo la kupigwa risasi na kusababisha kifo,” alisema.
Aliongeza kuwa picha ya kuchora ya mtuhumiwa huyo pamoja na taarifa za kiitelejensia zimesaidia kwa kiwango kikubwa kukamatwa kwake.
“Baada ya kuitoa picha ya mchoro katika vyombo mbalimbali vya kiulinzi, wananchi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, mtuhumiwa ametambuliwa,” alisema.
Kamishna Mussa alifafanua kuwa mtu aliyesaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo atakabidhiwa zawadi yake ya sh milioni 10 kimya kimya kutokana na sababu za kiusalama.
Tanzania Dima
No comments :
Post a Comment