NA MOSHI LUSONZO
3rd March 2013
.jpg)
Akitangaza majina 15 ya wajumbe walioteuliwa kwenye Tume hiyo, jijini Dar es Salaam, jana Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitaja adidu rejea itakayofuatwa na tume hiyo, ambapo sehemu kubwa inafanana na hoja ya Mbatia.
Kati ya majina yaliyotangazwa na Waziri Mkuu Pinda ni la Mbatia kuwa mmoja wa wajumbe wa tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Sifuni Mchome.
Pinda ametoa muda wa wiki sita kwa tume hiyo kufanya kazi ya kuchunguza anguko la ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani ya taifa kwa miaka miwili mfululizo kuanzia mwaka 2011.
Baadhi ya maeneo ambayo Mbatia alitaka yapitiwe upya katika hoja yake ni pamoja na mitaala ya elimu na muhutasari kwa kile alichoeleza kuwa imepitwa na wakati, udhaifu katika vitabu vya kiada na ziada, udhaifu wa mfumo rasmi wa elimu unaotokana na sera, mitaala na mihtasari ya elimu na kupitwa na wakati wa Sera ya Taifa ya elimu. Wakati akiongea na wajumbe wa tume hiyo, Pinda alisema katika adidu za rejea itawapa uwezo wajumbe kuangalia mitaala na mihutasari ya elimu, kuiangalia Taasisi ya kukuza mitaala kama inafanya uwiano wa vitabu na mitihani inayotungwa pamoja na kutathimini mazingira ya ufundishaji na matumizi ya vitabu vya kiada na ziada.
Wajumbe wengine waliotajwa kwenye tume hiyo ni ni Benardether Mshashu (Mbunge), Abdul Marombwa (Mbunge) Profesa Mwajabu (UDSM), Honorath Chitanda (Ofisi ya Makamu wa Rais), Mahamoud Mringo (Tamongsco) na Daina Matemu kutoka Tahossa
Wengine Rajan Rakheshi (Twaweza) Peter Maduki (CSSC) Nurdin Mohamed (Bakwata) Suleiman Hemed Khamis (Baraza la Wawakilishi), Abadallah Hemed Mohamed (Baraza la Elimu Zanzibar) na Kizito Lowa (Baraza la kukuza mitaala).
Tume hiyo itafanya kazi zake Tanzania Bara na Zanzibar kwa kubainisha sababu za matokeo mabaya kwa kipindi hicho na kushuka kiwango cha ufaulu.
Kazi nyingine itakayofanywa na tume ni kutathmini nafasi ya Halmashauri katika kusimamia elimu ya shule za sekondari, na kutoa mapendekezo ya hatua ya kuchukua mara moja kwa wanafunzi 240,903 waliopata sifuri.
"Tunaiagiza tume kupendekeza hatua ya kuchukua kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja, katika kipindi cha muda mfupi, kati na mrefu." alisema Pinda.
Tume hiyo itatathmini kiwango na mazingira ya ufundishaji kwa kuangalia jinsi walimu wanavyomudu maudhui ya masomo wanayofundisha na matumizi ya vitabu na zana za ufundishaji.
Pinda alisema serikali ipo tayari kupokea mapendekezo hayo kwa manufaa ya nchi na ndio maana ikaamua kuchukua watu mbalimbali waliobobea katika elimu kwa kufanya kazi hiyo.
"Serikali imechukua hatua hii baada ya kuona matokeo ya kufedhehesha, tumechagua watu makini waliobobea katika elimu ili watufanyie kazi hii. tupo tayari kupokea mapendekezo yao na kufanyia kazi," alisema Pinda.
Baadhi ya wajumbe wa tume hiyo walioongea na NIPASHE Jumapili waliomba Watanzania wawe na subira kwa sababu kazi waliyopewa ni ngumu na inagusa maslahi ya nchi.
Mringo alieleza jukumu walilopewa ni zito lakini kitu kinachompa faraja kuona timu iliyoteuliwa ina wataalamu wazuri.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Rakheshi alisema kama tume hiyo ikifanya kazi yake kwa misingi isio ya kisiasa itaibua mambo mengi yanayosababisha elimu kushuka kila siku na kuifanya Tanzania kuonekana kuwa na elimu dhaifu.
Alisema wanajipanga na kutafakari kwa kina namna bora ya kufanya kazi kisayansi ili malengo ya serikali yaweze kutimia kwa kuboresha sekta ya elimu nchini.
Kwa upande wake Mbatia alisema kuwa mpaka sasa bado hajapokea uthibitisho kuwa ameteuliwa na Waziri Mkuu kuwa mjumbe wa kufuatilia matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne cha mwaka 2012.
Taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam ilieleza kuwa akipata barua ya uteuzi huo atatafakari kwanza maudhui yake na kuyafanyia maamuzi sahihi kwa maslahi ya pamoja na watanzania wote.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment