NA DANIEL MKATE
30th March 2013

Marehemu Khamis (62), alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, baada ya kuanguka ghafla katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam wakati wa vikao vya kamati vikiendelea Jumatano iliyopita.
Kikwete aliwaongoza wabunge, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi mbalimbali katika kuaga mwili wa marehemu Khamis, huku Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa miongoni mwao.
Akizungumza baada ya kuuga mwili wa mbunge huyo, Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, alisema Bunge limepata pigo kwa kuondokewa kiongozi makini ambaye alikuwa akiifahamu siasa na mtu makini.
“Marehemu alikuwa kiongozi makini kwa wenzake, mcheshi, mstaarabu na mjenga hoja…ni pigo kwa taifa kutokana na kumpoteza mtu aliyekuwa akiifahamu ipasavyo siasa,” alisema Makinda.
Na Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa, alisema yeye pamoja na chama chake wamepokea kwa mshituko kifo cha mbunge Khamis.
Slaa alisema Khamis ametangulia wakati akiwa bado anahitajika kuipagania nchi yake katika masuala mbalimbali ya kitaifa, na pia alikuwa mstari wa mbele kushiriki kwenye mambo mbalimbali ya kijamii.
“Alikuwa rafiki yangu wa karibu, lakini kilichobaki sasa ni kumkumbuka katika utendaji wake wa kazi ili waliobaki waweze kuiga kizuri alichoacha,” alisema Slaa.
Akizungumzia salamu toka chama cha CUF, Naibu Katibu Mkuu, Julius Mtatiro alisema marehemu alikuwa mstari wa mbele katika vikao vya usuluhishi hususani katika chama chake.
Aidha, Mtatiro alisema marehemu Khamis licha ya kuwa mtaalamu wa kilimo, pia alikuwa mtafiti wa siasa Tanzania Bara na Visiwani.
Hata hivyo, alisema CUF kimepata pigo baada ya kupokea kwa masikitiko na mshituko taarifa za kifo cha mbunge huyo ambaye alikuwa mstari wa mbele katika masuala ya upatanishi, usuluhishi na ushauri ndani ya chama chake pamoja na jimboni kwake.
Spika Makinda aliwaongoza wabunge 34 wa bunge la Jamhuri katika maziko ya marehemu Khamis aliyezikwa jana huko Chambani, Pemba.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment