NA THOBIAS MWANAKATWE
23rd April 2013
.jpg)
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alishindwa kutaja majina ya watu waliohusika katika matukio mbalimbali likiwamo la Kibanda ingawa alisema uchunguzi wake umeanza muda mrefu.
Mngulu akizungumzia tukio la kutekwa na kuteswa kwa Kibanda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, alisema uchunguzi wa matukio hayo bado unaendelea.
Hata hivyo, kauli ya Mngulu kuhusu tukio la Kibanda inatofautiana na ile aliyoitoa Aprili 8, mwaka huu alipodai kuwa kati ya Aprili 15,16 na 17 jeshi hilo lingetoa ripoti ambayo ingewataja watu waliohusika na tukio la kutekwa kwa Kibanda.
Alitoa ahadi hiyo katika mahojiano na kipindi cha ‘Kumepambazuka’ kinachorushwa hewani na Radio One Stereo.
Mngulu alisema ripoti hiyo ndiyo itakayobainisha kama kuna watu wanaostahili kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na sakata hilo au la.
Akijibu swali kwa nini upelelezi wa sakata hilo umechukua muda mrefu, Mngulu alisema hakuna muda maalum uliowekwa na sheria wa kupeleleza jambo. Kutokana na hali hiyo, alisema upelelezi unaweza kuchukua hata miaka 10 na zaidi.
Mngulu alisema hata katika kumsaka aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden, ilichukua zaidi ya miaka 10 ndipo alipokamatwa. Hata hivyo, Mngulu jana hakuweka wazi ripoti ya uchunguzi wala kuwataja waliohusika na tukio la Kibanda badala yake aliishia kusema uchunguzi unaendelea na uko katika hatua mbalimbali za kiupelelezi.
“Kesi ya kuvamiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Kibanda,tukio la kutekwa na kujeruhiwa Dk. Ulimboka, matukio yaliyotokea Zanzibar, uchunguzi wa matukio haya bado unaendelea na uko katika hatua mbalimbali za kiupelelezi ambazo si vema kuziweka wazi kuepusha kuharibu upelelezi,” alisema Mngulu.
Machi 5, mwaka huu Kibanda alifanyiwa unyama wa kutisha baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana waliomteka na kuanza kumpa kipigo na kumejuhi vibaya sehemu kadhaa za mwili wake na kisha kumng’oa meno na kumtoboa jicho. Dk. Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana Juni mwaka jana ambao walimngo’a meno na kucha. Matukio haya ya kinyama yamewatia hofu wananchi ambao wamekuwa wakihoji upelelezi wake kuchukua muda mrefu ukilinganisha na matukio mengine.
Mngulu alisema matukio hayo yakiwamo yaliyotokea visiwani Zanzibar uchunguzi wake bado unaendelea na umefikia katika hatua ambazo haziwezi kuwekwa wazi kuogopa kuharibu upelelezi.
Kuhusu kesi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na anayeshitakiwa sambamba naye Ludovick Joseph, alisema upelelezi umekamilika na jalada limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi.
Lwakatare na Ludovick wamefunguliwa kesi katika Mahakama ya Kisutu wakikabiliwa na tuhuma za kuhusika na vitendo vya kigaidi.
Kuhusu tukio la kumwagiwa tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha, lililotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora Septemba 2011, alisema upelelezi wake upo katika hatua za mwisho na watuhumiwa wawili tayari wamefikishwa mahakamani. Mngulu alisema katika tukio hilo kama watabainika watuhumiwa wengine nao watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliomuuliza kwanini upelelezi wa matukio hayo unachukua muda mrefu, aliwataka kuisoma taarifa aliyoitoa. Kuhusu kwanini jeshi hilo halijakamata mtuhumiwa mwingine katika tukio la Dk. Ulimboka zaidi ya yule aliyejisalimisha kanisani, Joshua Mulundi, Mungulu aliwarejesha waandishi kusoma nakala ya tamko la jeshi hilo ambayo nayo haikusema lolote.
Mngulu alisema umma na waandishi wa habari lazima watambue kuwa zipo sheria na taratibu za kutoa habari za matukio yanayoripotiwa katika vituo vya polisi.
Alisema ieleweke kwamba taarifa zinaporipotiwa vituoni kwa mujibu wa sheria ni za siri kwa faida ya wahanga wa kesi na kwa ajili ya kufanikisha upelelezi wa kesi yenyewe.
Aliongeza kuwa, kanuni za Jeshi la Polisi zinamruhusu Kamanda wa Polisi wa mkoa husika kutoa taarifa za tukio hilo na siyo kujadili ushahidi wa kesi ili kuepusha kuathiri mwenendo mzima wa kesi zinapokuwa mahakamani.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment