
Rais wa nne wa Kenya Uhuru Kenyatta (kulia) akipokea upanga kama ishara ya nguvu ya kimamlaka na kiutawala kutoka kwa Rais anayemaliza muda wake Mwai Kibaki (wa pili kushoto) baada ya kuapishwa Aprili 9 jijini Nairobi.
UCHAGUZI Mkuu uliopita nchini Kenya umenifungua macho kwa mengi. Kadhalika ulikuwa na mengi ambayo wanasiasa wa Tanzania na Watanzania kwa jumla wanabidi wayazingatie hasa pale taifa hili linapousogelea Uchaguzi Mkuu ujao 2015…Kwanza sikuwahi kufikiria kabisa kwamba Raila Odinga mwenye uzito aliojaaliwa nao —wa mwili na wa kisiasa — atakuja kununa kama alivyonunua.
Alifikia hatua hadi ya kususia sherehe ya kitaifa ya kuapishwa hasimu yake mkuu Uhuru Kenyatta kuwa Rais wanne wa Kenya.
Raila alikhiyari atoweke asiwepo katika ardhi ya Kenya siku Uhuru alipokabidhiwa hatamu za kuliongoza taifa. Yeye na mwenza wake Kalonzo Musyoka waliona bora wapae, waivuke mipaka na watue Afrika ya Kusini.
Walisema walikwenda huko kupumzika wakiwa na mwenzao Moses Wetangula. Hakuna aliyewaamini.
Hakuna aliyewaamini kwa sababu kila mtu akijua kwamba hawakukubali kwamba kweli Uhuru alishinda.
Kuna wasemao kwamba Raila alifanya ndivyo kwa sababu lau angehudhuria sherehe ya kuapishwa Uhuru, angeweza kuvunjiwa heshima yake. Wanasema pengine angelizomewa na washabiki wa Uhuru.
Miye sidhani kama angelitiwa kwenye nazaha hiyo. Ninavyoamini ni kwamba angepigiwa makofi na kushangiliwa kwa kuwa mshindani aliyebobea, aliyekubali kushindwa. Hadhi yake ingezidi kupanda.
Kuna wanaofikiri kuwa sababu hasa iliyomfanya Raila asiwepo Kenya ni hofu ambayo labda alikuwa nayo kwamba angemshuhudia Uhuru anaapishwa asingeliweza kujizuia kuangua kilio mbele za watu — Wakenya wanzake na wageni.
Wenye fikra hizo wana chuki zao na Raila. Lakini yangelitokea hayo basi hiyo kweli ingekuwa fedheha kwake Raila ambaye karibuni ameanza kujifananisha na Nabii Issa (Yesu Kristo) na anayetunisha kifua na kutafahari unapomwita ‘Tinga’ kwa sababu ya ushujaa wake. Na Raila ni shujaa.
Juu ya kufungwa na kuteswa gerezani katika enzi za Rais Daniel arap Moi na utawala wake wa kimabavu Raila hakutetereka. Alisimama kidete kupigania kupatikana kwa mageuzi ya kidemokrasia nchini mwake.
Mchango wake si mdogo katika jitihada za kuifikisha Kenya ilipofika. Hamna shaka yoyote kwamba jina lake halitobanduka katika historia ya kuleta mageuzi nchini Kenya.
Hata hivyo, Raila ambaye pia anajulikana kuwa ni ‘kitendawili cha siasa za Kenya’ nusura anikanganye. Juu ya uzoefu wake wa kisiasa alikuwa akifanya mambo yasiyoelekea siku za awali baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Nitatoa mifano miwili. Kwanza, alihutubia mikutano miwili mikubwa ya hadhara kana kwamba bado yumo kwenye kampeni za uchaguzi ilhali uchaguzi ulikuwa umekwisha.
Pili, akisema mambo kwa lugha isiyolingana na hadhi yake. Baadhi ya matamshi yake yakitisha na yangaliweza kulitumbukiza taifa katika maafa.
Mfano mzuri ni yale aliyoyasema Machi 4 alipokuwa akihojiwa na BBC. Alisema kwamba ushindi wa Uhuru “ulikuwa umekwishapangwa kabla” na ulikuwa sawa na yaliyotokea 2007. Alichokuwa akisema ni kwamba kulifanyika ghiliba katika uchaguzi huo.
Shutuma kama hizi zimekuwa zikitolewa pia na taasisi zisizo za kiserikali pamoja na asasi za kiraia kwa jumla. Inasemekana kwamba chini chini zimekuwa zikishadidiwa na baadhi ya balozi za nchi za Magharibi.
Mikono ya serikali za nchi za Magharibi ilijitokeza mapema katika uchaguzi wa Kenya. Ni wazi kwamba ilikuwa na nia ya kukoroga mambo.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema kwa niaba ya wengi wetu alipoikebehi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na baadhi ya nchi za Magharibi kwa kuwaelekeza Wakenya nani wasiwachague na hivyo kuwashurutisha wawachague akina nani.
Huo ni mchezo mbaya na haukubaliki katika karne hii popote pale Afrika. Watanzania lazima wahakikishe kwamba hali kama hiyo haitozuka nchini wakati wa uchaguzi ujao. Lazima tuuzuie ukoloni mamboleo usiingie kwa mlango wa nyuma kwa kupitia asasi za kiraia.
Hatusemi kwamba asasi za kiraia ziminywe au zikabwe. Tunachosema ni kwamba ziwekewe kanuni ili zisije zikatumiwa na wenye kuzifadhili.
Tunavyotaraji ni kwamba itapofika Oktoba 2015 Tanzania itakuwa na Katiba mpya. Kwa sasa hatujui Katiba hiyo itakuwa na sura gani. Wala hatujui itasema nini kuhusu dhima au nafasi ya taasisi zisizo za kiserikali na asasi za kiraia katika jamii, hasa katika michakato ya kisiasa kama vile uchaguzi.
Nchini Kenya asasi za kiraia zimekuwa za kisiasa na za kikabila. Nyingi zimeonekana kuwa zinaupendelea upande mmoja katika siasa za huko na wengi wanazishutumu kuwa ni vibaraka wa ubeberu kwa vile zikicheza ngoma kwa kujidengua zikifuata midundo ipigwayo na balozi za nchi za Magharibi.
Nchini Kenya tunaweza tukazigawa taasisi zisizo za kiserikali katika mafungu matatu. La kwanza ni lile la jumuiya au taasisi zilizojikita kwenye jamii mashinani. Aghalabu hizi huwa ni ndogo na hutekeleza miradi mingi iliyo na manufaa vijijini.
Jumuiya aina hizi hujigharimia zenyewe na huwa hazina bajeti kubwa. Hujishughulisha na shughuli kama za kuipatia mikopo miradi midogo midogo, mambo ya usafi, afya, Ukimwi, uangalizi wa wazazi, haki za watoto na biashara ndogo ndogo.
Nyingi za jumuiya aina hii wakati wa uchaguzi wa Kenya zilikuwa zikisaidiwa na Idara ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) chini ya kitengo chake kiitwacho ‘Amkeni Wakenya’ ili kuwaelimisha Wakenya kuhusu haki zao za kiraia.
Jumuiya hizi hazikuwazikiungwa mkono na balozi za kigeni na kwa jumla zikipuuzwa na wafadhili wa Kimagharibi jijini Nairobi. Lakini kama nilivyokwishadokeza zikifanya kazi mashinani, zikishirikiana na wanavijiji na zikivisaidia ama vikundi vya wanavijiji au wanavijiji binafsi.
Fungu la pili ni la taasisi zisizo za kiserikali zilizo za wastani. Aghalabu hizi pia huwa hazina bajeti kubwa lakini ziko imara, hazina shida za fedha. Hujipatia fedha zake kutoka kwenye kikapu cha zile taasisi zisizo za kiserikali zinazosaidiwa na ‘Amkeni Wakenya’ ili kuleta mageuzi ya ile iitwayo Ajenda 4.
Haya ni mageuzi ya kikatiba, ya kisheria na ya kitaasisi, ya kuondosha umasikini na kutokuwako usawa, ya kuwapatia ajira vijana pamoja na mageuzi yanayohusika na umilikaji wa ardhi.
Taasisi hizo pia zinasaidiwa na ‘Amkeni Wakenya’ kuufahamisha umma kuhusu mfumo wa utawala wa ugatuzi na kuwaelimisha kuhusu haki zao za kiraia. Nyingi ya taasisi hizi zinapiga sana kelele kuhusu masuala ya utetezi wa kisiasa, utekelezwaji wa Katiba na masuala ya Ajenda 4.
Taasisi hizi zinapendelea kupigania haki za binadamu, zinaunga mkono mchakato wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ingawa si kwa nguvu sana kama zile asasi za kiraia nitakazozitaja katika fungu la tatu.
Wafadhili kutoka Marekani na nchi za Ulaya walio Nairobi hawazipendi taasisi hizi zilizo katika fungu la pili kwa sababu hazina funganisho na balozi za nchi zao.
Miongoni mwa jumuiya zilizo katika fungu hili ni pamoja na jumuiya ya wanawake ya Women’s Empowerment Link (WEL) na jumuiya za vijana kama Youth Agenda na za haki za binadamu kama Kituo cha Sheria.
Taasisi zote hizi zilizo katika hili fungu la pili hazipendelei chama au vyama vyovyote vya kisiasa nchini. Zinafanya kazi na wadau wake ili kuwawezesha.
Fungu la tatu ni lile la asasi za kiraia zilizo na makao yao makuu jijini Nairobi. Miongoni mwao mna halmashauri za kimataifa kwa mfano Tume ya Kimataifa ya Wanasheria (ICJ).
Pia kuna nyingine kadhaa za kienyeji zikiwa pamoja na Kituo cha Afrika cha Utawala Wazi (AfriCog), Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, InformAction (inayoongozwa na Maina Kiai) na Inuka Trust (inayoongozwa na John Githongo).
Zote hizi ni asasi babu kubwa. Zina uhusiano maalum na wa moja kwa moja na balozi za nchi za Magharibi. Kwa kawaida huwa hazipendi kupewa misaada ya fedha kutoka kwenye vikapu vinavyofadhiliwa na wafadhili kwa sababu zinasema zikifanya hivyo zinakuwa zinanyimwa fursa ya kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na maafisa wa balozi za kigeni. Ila ya asasi hizi ni kuwa zina upendeleo wa kisiasa.
Balozi za nchi za Magharibi zinazifadhili asasi hizi kwa sababu zinawapenda wale watu walioziasisi ijapokuwa asasi hizo aghalabu huwa hazina taratibu za kuwajibika, hazina fungamano na wananchi wa kawaida hasa wa mashinani na vijijini na haziwaathiri kwa njia yoyote ile.
Asasi hizi zimekuwa zikisaidiwa kwa hali na mali na balozi za nchi za Magharibi wakati wa kampeni za uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Asasi hizi ndizo zilizofikisha kesi katika Mahakama ya Juu ya Kenya kuishitaki Tume ya Uchaguzi na kutaka kuubatilisha ushindi wa Uhuru Kenyatta.
Kadhalika hizi ni asasi zenye kuunga mkono kwa dhati mchakato wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) dhidi ya Uhuru na mwenza wake William Ruto. Wala hazikuwa zikificha ndoto yao ya kumtaka Raila Odinga, mgombea urais wa Muungano wa CORD, aibuke mshindi.
Source: Raia Mwema
No comments :
Post a Comment