NA WAANDISHI WETU
24th May 2013
Mjamzito auawa kwa kupigwa risasi tumboni
Msako mkali wafanyika nyumba kwa nyumba
Machafuko katika mkoa wa Mtwara jana yaliingia siku ya pili huku mwanamke mjamzito akiuawa kwa madai ya kupigwa risasi na polisi, watu 18 wakijeruhiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likiingilia kati kulinda maeneo muhimu.
Kifo cha mwanamke huyo kimeongeza idadi ya waliokufa kufikia wawili baada ya mtu mmoja Karim Shaibu, kuuawa kwa risasi juzi katika machafuko hayo.
Aidha, watu waliojeruhiwa 18 wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula.
Vurugu hizo jana ziliwalazimisha baadhi ya wakazi wa mji huo kukimbilia porini huku wanawake na watoto wakikimbia katika Hospitali ya Ligula kunusuru maisha yao.
Pia, idadi ya ofisi za serikali za kata katika Manispaa ya Mtwara zilizochomwa moto imeongezeka kutoka tatu hadi nane na hadi kufikia jana jioni hali ya mji wa Mtwara ilikuwa haijatulia.
Polisi walikuwa wanaendelea kufannya msako wa nyumba kwa nyumba huku habari zikisema kuwa walengwa katika msako huo ni wanaume ambao inadaiwa wengi wamekimbilia porini.Kifo cha mwanamke huyo kimeongeza idadi ya waliokufa kufikia wawili baada ya mtu mmoja Karim Shaibu, kuuawa kwa risasi juzi katika machafuko hayo.
Aidha, watu waliojeruhiwa 18 wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula.
Vurugu hizo jana ziliwalazimisha baadhi ya wakazi wa mji huo kukimbilia porini huku wanawake na watoto wakikimbia katika Hospitali ya Ligula kunusuru maisha yao.
Pia, idadi ya ofisi za serikali za kata katika Manispaa ya Mtwara zilizochomwa moto imeongezeka kutoka tatu hadi nane na hadi kufikia jana jioni hali ya mji wa Mtwara ilikuwa haijatulia.
NCHIMBI ATUA MTWARA
Wakati hayo yakiendelea,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi na Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mngulu, waliwasili jana jioni mjini Mtwara kuangalia athari zilizotokana na machafuko hayo.
Dk. Nchimbi aliwasili saa 11:15 jioni mjini Mtwara kwa helkopta ya Jeshi la Polisi na kukuta askari wa JWTZ wakiwa wameimarisha ulinzi katika uwanja wa ndege.
Katika uwanja huo kulikuwa na gari la jeshi na polisi wenye silaha. Baada ya kuwasili walikwenda kutembelea maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na vurugu hizo na baadaye walitarajiwa kukutana na uongozi wa serikali ya mkoa wa Mtwara.
Kwa kuanzia, Dk. Nchimbi alianza kukutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na maofisa wa JWTZ katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mtwara.
Hali ya mji wa Mtwara ilionekana kutawaliwa na ukimya bila kuwapo watu mitaani zaidi ya malori ya polisi yaliyokuwa yamebeba wanajeshi.
JWTZ ZAIDI WAWASILI MTWARA
Wanajeshi zaidi wa JWTZ waliendelea kuwasili mjini Mtwara. Saa 11:52 ndege ya jeshi yenye namba JWTZ 9034 iliwasili katika uwanja wa ndege wa Mtwara ikiwa na wanajeshi kadhaa.
Mara baada ya wanajeshi hao kuwasili, walipokelewa na maroli matatu ya JWTZ uwanjani hapo.
Taarifa zaidi ambazo NIPASHE ilizipata kutoka Mtwara zinaeleza kuwa kutokana na vurugu hizo, idadi ya watu waliokamatwa imefikia 107 hadi jana jioni kutoka 91 waliokamatwa juzi.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile, akizungumza na NIPASHE jana alisema kufuatia machafuko hayo, vikosi vya JWTZ vimewasili mjini humo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi maeneo muhimu.
Ndile ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, alisema wanajeshi waliowasili mjini humo wanatokea vikosi vilivyopo mkoani humo.
Alisema wanajeshi hao wamepelekwa mjini Mtwara kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwenye visima vya gesi, uwanja wa ndege, bandari, vituo vya umeme na taasisi nyingine kubwa za serikali.
Alisema vitendo vya uharibifu wa mali viliendelea kujitokeza katika mji huo na jana ofisi tano za serikali za kata zilizopo Mikindani mjini zilichomwa moto.
Mkuu huyo wa wilaya alisema watu 10 wamejeruhiwa wakiwamo askari polisi watatu ambao wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya Ligula.
“Machafuko yameingia siku ya pili na hali bado siyo nzuri na muda huu hakuna huduma zozote zinazopatikana mjini hapa,”alisema Ndile wakati akizungumza na NIPASHE majira ya mchana.
WANANCHI WAKIMBILIA PORINI
Baadhi ya wananchi wa mji huo wamelazimika kukimbilia porini kutokana na msako unaofanywa na askari polisi nyumba kwa nyumba katika mitaa ya mji huo.
Mkazi wa eneo Chibukuta Kagera B, alisema kutokana na msako huo yeye pamoja na familia yake alilazimika kukimbilia porini.
Wakazi wa mji huo walisema ujio wa wanajeshi umesaidia hali ya amani kurejea.
“Askari polisi walikuwa wanatupiga ovyo bila kujali hali na umri, watoto, wazee na wajawazito, ujio wa wanajeshi umesaidia sana sababu wao hawatupigi,” alisema mkazi mmoja wa Mikindani.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kutokana na machafuko hayo, vituo vya kuuza mafuta vimefungwa hali iliyosababisha upatikanaji wa nishati hiyo kuwa ngumu.
Lita moja ya mafuta ya dizeli inauzwa kwa Sh.4,000 na petroli Sh.5,000.
JWTZ LATOA TAMKO
Wakati huo huo, Msemaji wa JWTZ amesema kuwa watapeleka askari zaidi kuongeza nguvu kwa Jeshi la Polisi kukabiliana na wananchi wanaofanya vurugu mkoani Mtwara.
Akizungumza jana katika kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One, Msemaji wa jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe, alisema maamuzi ya kupeleka askari mkoani Mtwara yamechukuliwa kwa haraka na hayakuhitaji kibali cha rais.
Alisema kwenye dharura kama hiyo inakubalika kuchukua uamuzi na barua rasmi ya kukubali askari kwenda huko kupelekwa kwenye eneo la tukio.
“Rais ameruhusu kwenye dharura kama hii unapeleka wanajeshi, hatusubiri barua iandikwe na kujibiwa, si kweli kuwa polisi wamezidiwa nguvu bali ni utaratibu wa kawaida kwa vyombo vya usalama,” alisema Mgawe.
Alisema jeshi hilo lina askari wengi hivyo kufa kwa wanajeshi wanne na kujeruhiwa wengine 20 hakuwafanyi wabadilishe maanuzi ya kupeleza askari zaidi na kwamba wataongeza wengine kadri itakavyohitajika.
Kanali Mgawe hakuweka bayana ni idadi ya askari watakaopelekwa Mtwara na kusema kuwa kwa sasa wanajiandaa na utaratibu wa kupeleka askari zaidi kwa kuwa Jeshi la Poisi bado halijaonyesha kuwa limeshindwa.
“Katika masuala ya kijeshi idadi siyo muhimu sana, hata hivyo tunaamini Jeshi la Polisi bado lina nguvu ya kutuliza hizo ghasia, ila tunacho kifanya sasa ni maandalizi tu ya chochote kitakachotokea endapo tutaona wanahitaji msaada,” alisema Kanali Mgawe.
Alisema hali ya askari waliopata ajali hivi karibuni katika eneo la Kilimahewa wakiwa njiani kuelekea Mtwara wanaendelea vizuri na wamelazwa katika Hospitali ya Ndanda.
Akielezea ajali hiyo ilivyotokea, Kanali Mgawe alisema dereva wa gari la jeshi alishindwa kulizuia gari alipokuwa akitaka kukata kona baada ya kutokea kwa gari lingine lililokuwa katika mwendo kasi kukata kona hiyo kisha kutimua vumbi lililosababisha dereva wa gari la jeshi kushindwa kuona mbele na hatimaye kupinduka.
Alisema gari la Jeshi lilikuwa limebeba askari zaidi ya 40, na waliofariki ni wanne na waliojeruhiwa ni wawili.
MJAMZITO AUAWA
Taarifa zinasema kuwa mjamzito huyo alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi na polisi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Ligula, Mohamed Kodi, alithibitisha kupokea maiti ya mjamzito huyo.
“Ni kweli, nimepokea mwili wa mjamzito hapa, amepigwa risasi tumboni, lakini pia nimepokea mwanafunzi mmoja wa shule ya Sekondari Chuno, ambaye amevunjwa miguu kwa risasi,” alisema Kodi.
Habari zinasema kuwa mjamzito huyo alikutwa nyumbani kwake na kuvamiwa na polisi kisha kufanyiwa unyama huo. Kwa mujibu wa Dk. Kodi, mpaka sasa hospitali hiyo imepokea majeruhi 18, kati yao watatu ni polisi, wawili wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, nesi mmoja na mwanafunzi mmoja.
Baadhi ya polisi pia wanadaiwa kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika mtaa wa Magomeni na kupora baadhi vitu vya ndani. Licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa kutangaza kuwa hali ya usalama mjini hapa ni shwari, milio ya risasi ziliendelea kusikika hadi jana katika maeneo ya Magomeni A, Likombe. Paulina Iddi (35), Mkazi wa Magomeni “A” alisema kuwa polisi wamekuwa wakiingia katika makazi ya na kuwanyanganya vitu mbalimbali zikiwamo simu.
Aidha alisema kuwa nyumba tatu za wakazi wa Mtaa huo zilichomwa moto. Hata hivyo, Kamanda Sinzumwa alikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu madai ya polisi kuhusika kumuua kwa kumpiga risasi mjamzito huyo na kuwajeruhi watu wengine akidai Waziri Nchimbi amekwisha kuzungumza. Badala yake aliwataka waandishi wa habari kuwatangazia wakazi wa mji wa Mtwara kuwa hali ni shwari katika maeneo yao.
TAMKO LA MCT
Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesikitishwa na vurugu hizo na kusema walengwa ni wananchi na waandishi wa habari. Taarifa ya MCT ilieleza jana kuwa waandishi wa habari watatu wako mafichoni ambao ni Kassimu Mikongoro wa TBC ambaye nyumba yake, gari na pikipiki vilichomwa moto.
“Leo (jana) wamerudi kumalizia nyumba yake ndogo,” taarifa hiyo ilieleza. Mwingine ni Hassan Simba wa Habari Leo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara ambaye nyumba yake alinusuriwa na polisi isichomwe moto pamoja na Rashid Mussa wa Uhuru na Mzalendo. MCT iliitaka serikali iwape ulinzi mahususi kutokana na kuwa walengwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment