Gesi Mtwara: Ni moto tena
17th May 2013
Hali hii inatokea wakati Wizara ya Nishati na Madini ikitarajia kuwasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 wiki ijayo, vipeperushi vimesambazwa mkoani Mtwara vikiwataka wananchi wa mikoa ya kusini kusitisha shughuli zao kufuatilia mjadala wa Bunge kwa madai kuwa serikali haina nia njema nao kuhusiana na umiliki wa gesi inayopatikana katika mikoa hiyo.
Vipeperushi hivyo vinadaiwa kusambazwa na kikundi cha watu wasiofahamika katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani kuanzia juzi, hali ambayo imezua hofu kwa wakazi wa mji huo.
Vipeperushi hivyo ambavyo vimesambaa katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo, vina ujumbe mbalimbali unaosomeka kuwa:
“Kusini zinduka, kauli mbiu gesi haitoki, bado kilio chetu cha kupigania rasilimali yetu kipo pale pale hivyo tuungane pamoja maana dhamira ya serikali haieleweki kwa mikoa ya kusini kama mnavyoona.”
Vinasomeka zaidi kuwa: “Wote kwa pamoja Mei 17, mwaka huu siku ya Ijumaa (leo) tusikilizeni bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni ili kujua mustakabali mzima wa gesi yetu.”
Hata hivyo, bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini itawasilishwa bungeni Mei 22, mwaka huu na siyo leo kama vipeperushi hivyo vinavyoeleza.
Vipepeshi hivyo vinaendelea kueleza kuwa: “Ili kuonyesha kilio/msimamo wetu kwa serikali wa kutaka maendeleo kwa mikoa ya kusini, siku hiyo huduma zote za jamii zisimamishwe za maduka, masoko, daladala, bodaboda, bajaji, nk ili iwe ujumbe kwa serikali maana JK ameamua kutumia nguvu nasi tunataka tupambane naye, “kusini kwanza.”
Kutokana na kusambazwa kwa vipeperushi hivyo, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Mtwara wameanza kununua mahitaji mbalimbali kwa kuhofia hali ya usalama Jumatano ijayo bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini itakaposomwa bungeni.
POLISI WAZUNGUMZA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sunzumwa, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema vipeperushi hivyo vilisambazwa juzi vikiwa na ujumbe huo ambao alisema unaashiria kuwapo kwa uvunjifu wa amani.
Alisema kusambazwa kwa vipeperushi hivyo kumezua hofu kwa wakazi wa Manispaa ya Mtwara na vitongoji vyake.
Kamanda Sunzumwa alisema kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi limewatahadharisha watu au kikundi cha watu wanaosambaza vipeperushi hivyo kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni uchochezi na ni kunyume cha sheria na watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Nawaomba wananchi wawe na amani, wawe watulivu, wasiogope vitisho hivyo, lakini pia naomba watoe ushirikiano kwa Jeshi letu la Polisi pale ambapo hali ya uvunjifu wa amani inajitokeza ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Kamanda Sunzumwa.
Aliongeza kuwa ni haki ya kila mwananchi kwa mujibu wa katiba ya nchi kufuatilia mkutano wa Bunge, lakini siyo haki kuwalazimisha wasitishe shughuli zao kwani siku ya bajeti siyo kwa manufaa ya mkoa wa Mtwara peke yake.
WAZIRI AWASHANGAA
Akizungumza bungeni mjini Dodoma jana, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema vipeperushi hivyo wameviona.
Aliwashangaa wakazi hao kusema kuwa bajeti ya wizara hiyo itasomwa leo wakati kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, bajeti hiyo itawasilishwa bungeni Jumatano ijayo.
Hata hivyo, Simbachawene hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na vipeperushi hivyo.
Desemba mwaka jana, wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.
Maandamano hayo ambayo yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambalo gesi asilia inapatikana.
Waandamanaji hao walitoa maazimio kadhaa mojawapo likihoji sababu za mitambo ya kuzalisha umeme kutojengwa Mtwara ambako ni jirani na inakochimbwa gesi hiyo.
Wamesema serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo wakati serikali ikiwa tayari imeshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam na kutaka ujenzi huo usitishwe.
Pia alisema kuwa uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa kwenye ziara yake mkoani Mtwara mwaka 2009 kwamba mkoa huo ujiandae kuwa ukanda wa viwanda.
Aidha, walitaka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.
JKadhalika, walisema serikali haijaeleza athari zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa gesi katika eneo hilo na namna itakavyoweza kusaidia kuziondoa, huku wakitaka gharama za uunganishaji wa umeme wa nyumbani zisizidi Sh 50,000 ili kila mwananchi aone ananufaika na gesi hiyo.
Maandamano hayo yaliratibiwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, yakiwa na kaulimbiu ya “gesi kwanza vyama baadaye”.
Baada ya maandamani hayo na shinikizo la wananchi hao kuzuia gesi isisafirishwe kwenda dare s Salaam, Rais Kikwete, katika hotuba yake ya kuufunga mwaka 2012, alisema kuwa serikali inatambua madai ya wananchi wamikoa ya kusini, lakini alisema kuwa hakuna mkoa wenye haki ya kudai kumuliki peke yake rasilimali zinazopatikana katika mkoa huo kwa kuwa ni mali ya Watanzania wote.
Hata hivyo, mgogoro wa gesi uliendelea na kuzua vurugu zilizosababisha baadhi ya mali za serikali na viongozu wa serikali kuharibiwa.
Hali hiyo ilimlazimisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwenda Mtwara Februari mwaka huu kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Katika ziara hiyo, Pinda alikuatana na kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya jamii zikiwamo taasisi za dini, mashurika yasiyo ya kiserikali, vyama vya siasa na viongozi wa serikali ili kurejesha utulivu.
Pinda alifuatana na mawaziri kadhaa ambao walitoa ahadi mbalimbali za kupeleka huduma muhimu kama viwanda, ujenzi wa barabara, kuboresha hali ya mipango miji, upanuzi wa bandari na utengenezaji wa ajira.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment